Wanne wafariki kwa kufukiwa na kifusi Morogoro

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama.
Muktasari:
- Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Mei 8, 2024 na kusababisha vifo vya watu wanne kati ya wanane waliofukiwa na udongo kwenye mgodi huo.
Ulanga. Watu wanne wamefariki dunia baada ya kudondokewa na gema la udongo wakati wakifanya shughuli za uchimbaji katika mgodi wa Alcaeda uliopo kata ya Nawenge, Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 9, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Mei 8, 2024 na kusababisha vifo vya watu wanne kati ya wanane waliofukiwa na udongo kwenye mgodi huo.
“Ni kweli Mei 8, 2024 tulipokea taarifa ya watu wanane kufukiwa na udongo wakati wakichimba madini huko Ulanga na watu wanne walifariki dunia, bado tunachunguza kama ule mgodi unafanya kazi zake kihalali
“Waliofariki kwa kuangukiwa na gema la mgodi ni pamoja na Ishiwa Kagege (30) mchimbaji na mkazi wa Tabora, Ismail Bashiri (35), mchimbaji na mkazi wa Arusha, Stephen Mpiondi (34), mchimbaji na mkazi wa Masasi, Mtwara na miili yao imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhiwa maiti kwenye Hospitali ya Ulanga,” amesema.
Mkama amesema bado jeshi hilo linachunguza chanzo cha tukio hilo, pamoja na mambo mengine ikiwemo kujua uhalali wa eneo hilo kuchimbwa madini.
Bentoni Matambala ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa mgodi huo, amesema ajali hiyo ilitokea Mei 8, 2024 saa 10 jioni baada ya kukatika kwa gema la mwamba na kuanguka chini ambako kulikua na watu wanane lakini wanne wakafariki papo hapo
“Kilichotokea ni mtikisiko uliojitokeza kwenye mwamba na ukakatika na kuanguka chini na bahati mbaya ulikuta kuna watu na wakafariki dunia na asili ya ile miamba ni kwamba ili uzalishe lazima utumie vilipuzi. Walipokuwa wale watu ni chini na miamba iko juu, wakifanya kazi ya uchorongaji na kipande cha jiwe ndicho kilikatika na kuwaangukia na kusababisha vifo vyao,” amesema.
Bishota William ambaye ni mkazi wa Ulanga, amesema mgodi huo umekuwa ukiendesha shughuli zake kwa muda mrefu lakini ajali kama hiyo haijawahi kutokea kabla
“Huu mgodi nimeufahamu kwa muda kidogo na wachimbaji hawa wamekuwa wakifanya kazi zao bila kupata madhara kama haya ambayo yamejitokeza kwa watu wanne kufariki kwa wakati mmoja. “Ushauri wangu ni kwamba tahadhari zichukuliwe wakati wa uchimbaji ili madhara zaidi yasitokee,” amesema.
Gerge Ismail, mkazi wa Ulanga ameiomba Serikali kuweka mkazo kwa wamiliki wa migodi kuhakikisha wanasimamia usalama wa wafanyakazi wao, ili kuepusha vifo vinavyotokea kwenye migodi hapa nchini.
“Wenye maeneo ya kuchimba madini mara nyingi huwa hawazingatii usalama wa wafanyakazi wao pale wanapokuwa wanatekeleza majukumu ya kiuchimbaji, na kwenye ule mgodi huwa wanalipua kwanza kabla ya kuchimba.
“Sasa, hiyo ni hatari maana wanaweza kulipua miamba na watu wako ndani, ile miamba ikadondokea kwenye mashimo na kusababisha watu kufariki, hivyo usalama wa wafanyakazi mahala pa kazi ni kitu muhimu cha kuzingatia,” amesema.