Wanaodaiwa kusafirisha kilo 332 za 'unga' waiangukia Serikali

Muktasari:

  • Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukamatwa wakisafirisha dawa za kulevya, Aprili 16, 2024 karibu na Hoteli ya White Sands, iliyopo Kinondoni.

Dar es Salaam. Washtakiwa tisa wanaokabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini na methamphetamine zenye uzito wa kilo 332, wameiomba Serikali kukamilisha upelelezi wa kesi yao ili iweze kuendelea na hatua nyingine.

Ombi hilo limetolewa na mshtakiwa Ally Ally (28) maarufu kama Kabaisa kwa niaba ya mwenzake, leo Juni 21, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Kabaisa ambaye ni mvuvi, ametoa ombi hilo, muda mfupi baada ya upande mashtaka ukiongozwa na Eric Davies kudai bado unaendelea na uchunguzi dhidi ya shauri hilo, hivyo kuomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya Davies kutoa maelezo hayo, Ally ambaye kesi dhidi yao ilisikilizwa kwa njia ya video wenyewe wakiwa mahabusu, amenyoosha mkono na alipopewa nafasi ya kuongea na hakimu, ameomba upelelezi uharakishwe.

"Mheshimiwa hakimu, tunaomba mahakama yako iwaelekeze upande wa mashtaka wakamilishe upelelezi wao kwa wakati ili kesi iweze kuendelea, maana tangu tumekamatwa mpaka leo upelelezi tunaambiwa bado," amesema Ally.

Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini anayesikiliza shauri hilo, amekubaliana na ombi hilo na kuelekeza upande wa mashtaka ukamilishe haraka upelelezi wa shauri hilo.

"Naelekeza, upande wa mashtaka mkamilishe haraka upelelezi wa shauri hili, ili washtakiwa wajue hatima yao," amesema Hakimu Mhini.

Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 2, 2024 itakapotajwa na washtakiwa wanaendelea kuwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Kabaisa, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni Bilal Hafidhi (31), Mohamed Khamis (47) na Idrisa Mbona (33).

Wengine ni Rashid Rashid (24), Shabega Shabega (24), Saadan Kasulu, Dunia Mkambilah (52), Mussa Husein na Hamis Omary (25)