Wananchi wagomea fidia ujenzi wa barabara Tarime

New Content Item (6)
Ujenzi wa uwanja wa ndege Musoma ukiwa unaendelea. Mradi huo utaogharimu zaidi ya Sh35 bilioni umefikia asilimi 47 za utekelezaji. Picha Beldina Nyakeke

Muktasari:

Wananchi wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara wanadaiwa kugomea fidia kwaajili ya kuachia vifusi vinavyotakiwa kwenye utekelezaji wa mradi wa barabara ya Mogabiri- Nyamongo wakidai malipo ni madogo.

Tarime. Mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa  barabara ya Mogabiri -Nyamongo Wilaya ya Tarime mkoani Mara amesema moja ya changamoto anayokumbana nayo katika utekelezaji wa mradi huo ni wananchi kugomea fidia wanayolipwa kwaajili ya kuachia vifusi vinavyotakiwa kwenye ujenzi huo.

Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 25 unatekelezwa na kampuni ya Nyanza Road Works Limited kwa gharama ya zaidi ya Sh34.6 bilioni.

Akitoa taarufa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya alipofanya ziara ya kukagua mradi huo Machi 26, 2023 Mhandisi Mkazi, Joshua Rusohoka amesema hali hiyo inarudisha nyuma kasi ya kutekeleza mradi huo.

“Unakuta tunafanya thamnini katika eneo fulani kwaajili ya kuchukua vifusi kuleta kwenye mradi baada ya tahmini tukitaka kuwalipa wanagoma wakidai hela ni kidogo tunalazimika kufanya sehemu nyingine tena hili ni tatizo kubwa na ni kama kuna watu wanawachochea wakatae,”amesema 

Amesema endapo wananchi wataendelea na msimamo huo upo uwezekano wa gharama za mradi kuongezeka kwani mkandarasi atalazimka kutoka nje ya eneo la mradi kwaajili ya kutafuta vifusi vinavyofaa kwenye ujenzi huo.

Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini ( Tanroads) Mkoa wa Mara, Vedastus Maribe amesema mradi huo uliofikia asilimia 15, umeanza kutekelezwa Julai 2022 na utakamilika Januari 2024.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya amewataka wakazi wa wilaya ya Tarime kutoa ushirkiano wakati wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi kwakuwa wanufaika wakuu wa miradi hiyo ni wananchi wenyewe.

“Hapa niwaombe viongozi wa kisiasa kuongea na wananchi ili wajue kuwa wao pia wana wajibu wa kuwezesha miradi itekelezwe kwa wakati na ufanisi na ikumbukwe kuwa fidia hizo zinalipwa kwa mujibu wa sheria,”amesema 

Katika hatua nyingine, Kasekenya amekagua na kuridhika na utekelezaji wa  mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege Musoma ambao unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh35 bilioni hadi kukamilika.

“Ingawa mradi umechelewa lakini kwasasa mabadiliko ni makubwa sana sio kama nilivyokuja hapa mara ya mwisho kazi zilikuwa hazifanyiki niwapongeze Tanroads kwa usimamizi mzuri, endeleeni hivyo hivyo tunataka kabla ya mwisho wa mwaka huu  ndege za abiria zianze kutua hapa,”amesema

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa uwanja huo, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mara, Vedastus Maribe amesema hadi sasa mkandarasi wa mradi huo amelipwa zaidi ya Sh1.9 bilioni na utekelezaji umefikia asilimia 47.