Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wamiliki wa hoteli za kitalii walia na tozo za Dola

Muktasari:

  • katika kikao kilichoitishwa na Benki ya Tanzania( BoT) kikilenga kuelezea mabadiliko ya kanuni mpya za uendeshaji wa maduka ya kubadili fedha za kigeni, wamiliki na waendeshaji hao wa hoteli za kitalii, wameiomba Serikali kuondoa baadhi ya tozo zinazotozwa kwa Dola.

Arusha. Wadau wa sekta ya utalii wameiomba Serikali kuondoa tozo mbalimbali za utalii ambazo zinatozwa kwa fedha za kigeni, hususani Dola za Marekani.

Wametoa ombi hilo leo Jumamosi Machi 23,2024 jijini hapa na wamiliki na waendeshaji wa hoteli za kitalii Arusha na mikoa ya Kanda ya Kaskazini katika kikao baina yao na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba.

Katika kikao hicho kilicholenga kuwaeleza wamiliki wa hoteli kuhusu utaratibu mpya utakaowaruhusu wenye mahoteli kuendesha biashara ya ubadilishaji wa fedha, wadau hao wamesema wako tayari kuchangamkia fursa hiyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), William Chambulo, amependekeza kuwa mifumo ya malipo ya shughuli za utalii ziendeshwe kuwa kutumia mifumo ya kidijitali badala ya fedha taslimu, kwani baadhi ya watumishi katika hoteli siyo waaminifu.

Amesema baadhi ya tozo ambazo wamekuwa wakilipia kwa fedha za kigeni hasa Dola za Marekani huku risiti wakipewa za fedha ya Tanzania, hivyo kuiomba Serikali kuangalia baadhi ya tozo wanazowatoza.

 “Mimi ni mmiliki wa hoteli, nina hoteli 32, binafsi sitaki fedha taslimu kwenye hoteli yangu kwani ni wizi wa ajabu, tunafukuza mameneja, wafanyakazi kwa sababu ya wizi, mimi nimeshafukuza mameneja 13 kwa ajili ya wizi na kwa sasa kinachosaidia kukomesha huo wizi ni matumizi ya kadi,” amesema Chambulo.

Amesema kuwa wazo la kuwaruhusu wenye hoteli za kitalii kupewa leseni ya kuendesha maduka ya fedha za kigeni haitakuwa mwarobaini wa kukomesha biashara haramu ya fedha za kigeni na inaweza kuhatarisha usalama wao, kulingana na maeneo hoteli zao zilipo.

“Nilikuwa nakuomba Tanzania tuwekeze kwenye kadi, yaani hata wanafanya kazi muwekee fedha yake benki, kadi itasaidia wizi hakuna na fedha za Serikali kodi haipotei, angalieni Kenya.”

 Kitu kingine tujaribu kujiuliza fedha taslimu zinatoka wapi lakini ukiangalia hizi duka za kubadilishia fedha mnataka tuuwawe na wageni wetu, mimi siwezi nikaweka duka la kubadili fedha pale Karatu watakuja kuniua watafikiria nina mamilioni ya fedha ya kubadilishia fedha,” amesema.

Naye Titus Muruve, amesema suala hilo linapaswa kuangaliwa zaidi kwani katika baadhi ya mazingira siyo salama kufanya biashara ya kubadili fedha.

Naye Cyril Ako, amesema ni muhimu kuendelea kusisitizwa kwa matumizi ya fedha kwa njia ya kielektroniki badala ya kutumia taslimu  ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa biashara haramu ya fedha za kigeni.

Hata hivyo akizungumza katika kikao hicho, Tutuba amesema hoteli za kitalii zitakazoruhusiwa kufungua maduka hayo ni zenye  nyota tatu hadi tano na hazitakuwa na masharti magumu kama inavyolalamikiwa.

 Amesema wafanyabiashara  watakaokuwa tayari mchakato wa kupata leseni zao utachukua muda wa wiki mbili.

Tutuba amesema utaratibu huo mpya umelenga kuondoa kero inayowapata watalii na wageni wengine kutoka nje ya nchi, ambao hufika hotelini muda ambao siyo rafiki kutafuta mahali pa kubadilisha fedha za kigeni.

"Wageni wengine hufika usiku, siku za sikukuu au mwishoni mwa wiki ambapo maduka ya kubadilishia fedha za kigeni yamefungwa. Ili kuondoa kero hiyo, tumeruhusu wamiliki wa hoteli za kitalii kufungua maduka hayo", amesema.

Kwa mujibu wa Garava, huduma hiyo pia inalenga kudhibiti biashara haramu ya fedha za kigeni ambayo imekithiri kutokana na ukosefu wa maduka halali ya kubadilisha fedha.