Wakulima Nachingwea waiomba Serikali kuwaondoa wafugaji

Muktasari:
- Wananchi wa Kijiji cha Ngunichine wilayani Nachingwea wameiomba Serikali kuwaondoa wafugaji kijijini kwao.
Nachingwea. Wananchi wa Kata ya Ngunichile wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi wanaiomba Serikali wawaondoe wafugaji katika kata hiyo ili kuepusha migogoro ya wananchi na wafugaji inayosababisha uvunjifu wa amani.
Matukio ya uvunjifu wa amani yamedumu kwa zaidi ya miaka mitatu sasa bila kupata suluhisho na kuwaacha wakulima wakiwa masikini kwa sababu mifugo inakula mazao yao.
Diwani wa Kata ya Ngunichile, Saidi Makayola Amekiri Kutokea kwa Tukio la Wananchi Kijijini humo la Kufunga Barabara Kushinikiza Serikali ya Ngazi za Juu Kufika Kijijini Humo.
Kamishina wa Oparesheni Maalumu wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Awadhi na manaibu wawili Jumanne Sagini Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mifugo, Davidi Silinde walifika kijijini hapo juzi ili kujionea hali halisi.
Diwani wa Kata ya Ngunichile, Saidi Makayola amesema wananchi walifunga barabara kushinikiza Serikali ya juu wafike kutatua mgogoro wa Wananchi na Wafugaji.
“Kilichotokea askari walifika wamebomoa nyumba na kukamata wannachi ambao wapo mahabusu hadi leo," amesema Makayola.
Makayola ameongeza kuna msiba wa mwananchi moja aliyeshambuliwa na wafugaji, juzi tumezika mwanachi mwingine na mwalimu aliyejeruhiwa yupo hospitalini.
"Yanayofanyika siyo makosa ya kifugaji ni uhalifu wanapiga watu wanachoma mikuki na hata kina mama wakienda mashambani wanawabaka," amesema Makayola.
Asha Kabege na Mfaume Mfaume wakazi wa Kijiji cha Ngunichile wameiomba Serikali iwasaidie kuwaondoa wafugaji ili amani ipatikane.
"Hatuna cha kufanya watoto wetu wakienda shuleni, walimu wanashambuliwa na kujeruhiwa. Tumeanza kutaabika na tembo, wakala mazao yetu yote,” amesema.
“Tukahamia kwenye mbaazi kwa kuwa hawali lakini wamekuja wafugaji wamelisha mbaazi zote, hatuna la kufanya. Tuna njaa tunaomba Serikali itusaidie hasa kina mama tunateseka,"amesema Asha Kabege.
Naye Mfaume Mfaume amesema pembejeo zinazotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kazi bure, wafugaji wanalisha mazao yao na wanawaambia bado korosho zenu.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamedi Moyo amekiri kutokea kwa tukio la wananchi kufunga njia na watu kumi na tatu kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi pia amethibitisha kutokea kifo cha mtu mmoja.
"Jeshi la Polisi lina washikilia wananchi kumi na tatu kwa tuhuma za kufunga barabara na simu zao zinafatiliwa kuna taarifa za awali zimebainika wananchi hao kufanya mawasiliano wakitoa taarifa ya mauwaji ya Mmang'ati mmoja watakaobainika kukutwa na hatia watafikishwa mahakamani na wasio na hatia wataachiwa," amesema Moyo.