Wageni zaidi ya 1,000 wazuiliwa kuingia Tanzania

Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni akizungumza wakati kijibu maswali kwenye kikao cha 40 cha mkutano wa 15 wa Bunge la bajeti unaoenndelea jijini Dodoma leo Juni 4,2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Jumla ya wageni 1,223 kwa kipindi cha kuanzia Januari 2022 hadi Mei 2024, Tanzania kupitia mfumo wa elektroniki wa mipaka.

Dodoma. Jumla ya wageni 1,223 wamezuiwa kuingia nchini kwa kutumia Mfumo wa kielektroniki wa mipaka (e – border) kwa kipindi cha kuanzia Januari 2022 hadi Mei 2024.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ameyasema leo Juni 4, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda.

Mbunge huyo amehoji nini mpango wa Serikali kudhibiti wahamiaji haramu mipakani kabla hawajaingia nchini. 

Akijibu swali hilo, Masauni amesema Serikali inaendelea kusimika mfumo wa kielektroniki wa mipaka (e – border) ambao unasaidia katika kudhibiti wageni wasio na sifa kabla hawajaingia nchini.

Amesema kwa kutumia mfumo huo, Serikali imefanikiwa kuwazuia kuingia nchini jumla ya wageni 1,223 kwa sababu mbalimbali, kuanzia Januari 2022 hadi Mei 2024.

 “Serikali inaendelea kufanya vikao vya kikanda, kimataifa na ujirani mwema kwa lengo la kupanga mipango ya pamoja ya kudhibiti uhamiaji haramu,” amesema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Silvia Sigula amesema wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni, ikiwemo mikoa ya Kigoma wamekuwa wakipitia changamoto za unyanyasaji wakati wa misako ya uhamiaji haramu.

Amehoji Serikali haioni ni wakati wa kutoa mafunzo kwa askari ili kuwawezesha kushughulika na changamoto hiyo bila unyanyasaji.

Akijibu swali hilo, Masauni amesema wanao utaratibu wa kutoa elimu na mafunzo kwa maofisa uhamiaji ili kuhakikisha wanatenda haki inayostahili bila usumbufu.

Mbunge wa Buhigwe, Felix Kavejuru amesema wahamiaji wengi wamekuwa wakikamatwa katikati ya nchi katika mikoa ya Morogoro, Mbeya na Dodoma.

Amehoji kama Serikali imeshafanya uchunguzi ili kubaini wahamiaji hao haramu wanapita wapi kuingia nchini.

Akijibu swali hilo, Masauni amesema wanapita katika maeneo yasiyo rasmi.

Amesema miongoni mwa mambo wanayoyafanya katika kukabiliana na wahamiaji haramu ni kuongeza idadi ya askari wa uhamiaji, kutoa magari, kuendeleza msako wa wahamiaji haramu.

Masauni amesema wengi wao wanatoka katika nchi Ethopia na kwamba hivi karibuni wameweza kufanya marekebisho katika utaratibu wa viza rejea.

Amesema kwa kufanya hivyo changamoto hiyo imepungua na kwamba wameweza kupata wahamiaji 3,500 ambao wamepita katika njia halali badala ya njia haramu.

Amesema hali hiyo imewawezesha kukusanya Dola za Marekani 170, 000 na kwamba mikakati ni mingi wanayoendelea nayo katika kudhibiti changamoto hiyo.

Mbunge wa Kalambo, Josephat Kandege amesema katika hali ya kawaida kumekuwa na ruhusa ya umbali fulani kwa wananchi wanaotoka Kenya kuingia Tanzania au kinyume chake, kakini kwa upande wa Kalambo imekuwa na tatizo kubwa.

Hivyo amehoji ni umbali gani kutoka nchi moja kwenda nyingine ambayo mwananchi anaruhusiwa kusafiri bila shida.

Akijibu swali hilo, Masauni bila kutaja umbali, amesema atakwenda kulifuatilia jambo hilo ili kuepusha usumbufu kama huo kutokea tena.

“Hakuna tofauti ya watu wanaopakana iwe wanapakana na Burundi au Kenya. Utaratibu wa sheria unaruhusu watu kutoka ndani ya mipaka ya nchi na kuingia kwa kibali maalumu,” amesema.