Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wafanyabiashara Soko la Samunge wagoma, wafunga barabara

Muktasari:

  • Miongoni mwa malalamiko yao ni pamoja na usumbufu wanaoupata kutoka kwa mgambo na mazingira wanayofanyia biashara kuwa na miundombinu mibovu ikiwemo ya majitaka.

Arusha. Wafanyabiashara ndogondogo, wakiwemo wauza mbogamboga wa Soko la Samunge, wamefunga barabara ya Fire, wakidai kunyanyaswa na mgambo na kutaka kusikilizwa kero zao.

Wafanyabiashara hao pia wanadai kunyanyaswa, kunyang’anywa bidhaa na kuondolewa maeneo yao bila suluhisho mbadala.

Mmoja wao, Nembris Paulo (70), amesema mgambo wamekuwa wanawanyang’anya bidhaa zao.

"Presha inapanda, sukari inapanda, nafika nyumbani sifai, mzigo umechukuliwa," amesema.

Mwingine, Rose Isack ameongeza kuwa licha ya kulipa ushuru, bado wanapokonywa bidhaa na kudaiwa Sh10,000 ili  kuzirejesha.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amefika na kuwatuliza wafanyabiashara hao, akikiri eneo walilopewa halifai kwa biashara kutokana na uchafu.

Amewaruhusu kutumia eneo mbadala kwa wiki moja wakati halmashauri ikitafuta suluhisho la kudumu.

Pia ameahidi kupitia nyaraka za soko na kushirikiana na wataalamu wa halmashauri kupanga mipango ya kudumu ili wafanyabiashara wapate maeneo salama.

Kuhusu mgambo, amesema jukumu lao ni kulinda usalama, lakini kuondoa wafanyabiashara bila mpango mbadala si sahihi.

Ameahidi kulijadili suala hilo na mamlaka husika ili kuhakikisha haki inatendeka.

 “Nitoe wito kwa wafanyabiashara, tunapopata changamoto tuna uongozi kuanzia kwenye soko namna ya kuwasilisha taarifa hata tunapokuwa na taharuki, hayo yalikuwa maeneo muhimu ya kufika kabla ya lolote,

“Kwa bahati mbaya walikataa maelekezo ya viongozi wao mpaka mimi nimefika ila ninashukuru tumesikilizana. Nitaenda kukaa na wataalamu wa halmashauri wakiwemo wa mazingira na biashara ili kupanga mipango inayotekelezeka ili wananchi wafanye biashara maeneo salama,” ameongeza.