Wafanyabiashara hatarini kupata magonjwa ya mlipuko

Uchafu ukiwa umerundikana katika soko la walaji Bomang'ombe wilayani Hai mkoani Kilimanjaro
Hai. Wafanyabiashara wa Soko la Walaji Bomang'ombe, Wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, wapo hatarini kupata magonjwa ya mlipuko ikiwamo kipindupindu kutokana na mrundikano wa taka katika eneo hilo.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wamesema takataka hizo zimeanza kutoa harufu na kuwa kero kwa wafanyabiashara na watu wanaoenda kufanya Manunuzi sokoni hapo na hivyo wameomba ziondolewe.
Anna Munisi ambaye ni mmoja wa mfanyabiashara sokoni hapo, amesema taka hizo zimekuwepo sokoni hapo kwa muda wa mwezi mmoja na kwamba zinaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.
"Tunaomba watu wa mazingira wafike, watusaidie kuondoa takataka hizi kwani zinasababisha harufu mbaya na wakati mwingine tunaweza kupata magonjwa ya mlipuko ikiwamo kipindipindu," amesema Anna
Kwa upande wake Mariamu Kasimu, amesema kutokana na takataka hizo kurundika karibu na eneo anapofanyia biashara, wateja wake wamekuwa wakishindwa kifika na hivyo kujikuta akipata hasara.
"Mimi na baadhi ya wenzangu, wateja wanakwepa kuja huku kutokana mrundikano huo, nah ii inatusababishia hasara,tunaomba waondoe takataka hizi na hivyo kufanya mazingira ya biashara kuwa mazuri kwani tunalipa ushuru," amesema Mariamu
Kwa upande wake Ofisa Mazingira wa wilaya hiyo, Alfred Njekite, amekiri kuwapo kwa tatizo hilo, ambapo amesema mtu aliyekuwa amechukuwa zabuni ya kukusanya uchafu muda wake umekwisha.
Na kwamba kuna utaratibu wa kumpatia mzabuni mwingine, hata hivyo katika kunusuru hali hiyo isilete kero yeyote, ofisa huyo amesema: “Halmshauri itaingilia kati kwa ajili kunusuru hali hiyo, kwa leo au kesho uchafu utaondoka.”