Wadau waweka maazimio adhabu ya viboko shuleni
Mwalimu akiwa anamwadhibu mwanafunzi wake. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Aprili 30 ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Adhabu ya Viboko. Mwaka huu Tanzania imeiadhimisha kwa kufanya mdahalo uliokuwa na kauli mbiu ya No Collabo, uliohusisha wadau mbalimbali, ikiwamo Save the Children Tanzania, WiLDAF, UNICEF, WHO, HakiElimu, Msichana Initiative na LHRC.
Dar es Salaam. Wakati wadau wa elimu wakiweka maazimio sita katika mkakati wa kuondolewa kwa adhabu ya viboko shuleni, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na wazazi wameibuka na mtazamo tofauti juu ya jambo hilo.
Adhabu hiyo imekuwa ikipingwa vikali na baadhi ya wadau wa elimu wakitaka waraka wake wa 2002 uondolewe, kwani unadhoofisha ustawi wa wanafunzi na kuzuia maendeleo ya taifa.
Waraka huo unaeleza mzazi au mwanafunzi atakayepinga adhabu ya viboko atafukuzwa shule, na mwalimu ambaye hatatoa adhabu hiyo atachukuliwa hatua.
Katika mdahalo uliokwenda sanjari na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Adhabu ya Viboko, uliofanyika jana Aprili 30, 2026 jijini Dar es Salaam, mjadala mkubwa uliibuka kati ya walimu, wazazi na wadau wengine wa elimu.
Baadhi ya walimu walieleza changamoto wanazopitia katika kuwalea na kuwafundisha watoto hao shuleni, wakitaka wazazi pia kutimiza wajibu wao katika malezi.
Wazazi pia walieleza namna ambavyo baadhi ya walimu wamekuwa wakiwaadhibu wanafunzi hovyo, wengine kuwasababishia majeraha makubwa hadi vifo.
"Wapo walimu ambao hadi leo wana kesi, wengi wao ukizungumza nao huwa wanajuta," amesema mmoja wa wazazi katika mdahalo huo.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2023 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), matukio 11 ya matumizi ya nguvu kupita kiasi yaliripotiwa, ambapo matukio nane yalisababisha vifo na matatu yalisababisha ulemavu wa kudumu kwa wanafunzi.
Akizungumzia hilo, Mkuu wa Idara ya Sera, Utafiti na Ushirikiano wa Kimataifa wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Prosper Lubuva, amesema wao ndiyo wahusika katika utekelezaji wa adhabu za viboko na kueleza mara kadhaa zinawatia hatiani.
"Mwongozo unasema kabla ya kumpa adhabu mwanafunzi, uangalie afya; mwalimu si daktari, hiyo afya atahisi tu. Nashauri tungeachana nazo," amesema.
Amesema kuna namna nzuri ya kuondokana na adhabu ya viboko kwa mwalimu na mwajiri wake ambaye ni serikali.
"Kuwe na uwiano mzuri kati ya mwalimu na wanafunzi; hii itasaidia hata kufuta waraka wa adhabu ya viboko. Mwalimu atawafahamu wanafunzi mmoja mmoja na changamoto zao; hii itasaidia katika kujifunza. Akiwa nao wengi wamesongamana ni ngumu," amesema.
Mkurugenzi wa Shirika la WILDAF, Anna Kulaya, amesema wao kama wadau wana vitu vingi vya kufanya katika hilo, akitaja maazimio sita ambayo watayafanyia kazi kwa haraka ili kuona namna mwongozo wa viboko utabadilishwa, ikiwamo kuwa na midahalo ya mara kwa mara na kupata maoni ya wadau.
Mengine ni kufanya kazi kwa karibu na Kamati ya Bunge ili kuona ni namna gani wataboresha kanuni, kumuandikia Waziri wa Elimu maoni yao, kushirikiana moja kwa moja na CWT, kuwashirikisha wakaguzi na kufanya tafiti za athari za viboko shuleni.
Mwakilishi wa Wizara ya Elimu, James Mnyati, alikiri waraka wa viboko mashuleni umepitwa na wakati, hivyo akashauri kuwe na mjadala wa kuboresha mazingira ya kujifunza na ufundishaji. "Katika hili tukubaliane kuna wajibu wa mzazi, mtoto na wasimamizi wa elimu."
Mtaalamu wa ufundi wa ulinzi wa mtoto na utawala wa haki za mtoto kutoka Save the Children, Barnabas Kaniki amesema matumizi endelevu ya adhabu ya viboko shuleni bado ni changamoto, yakisababisha majeraha, ulemavu na hata vifo.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Tandika, Hauleti Abdallah amesema adhabu ya viboko si njia sahihi ya nidhamu kwani, mbali na kusababisha majeraha ya mwili, yanavuruga ujifunzaji.
Amegusia tukio la mdogo wake aliyepigwa na mwalimu kwa kuchelewa kufika shuleni na kumsababishia majeraha ya mkono na mgongo; kwa siku kadhaa hakuweza kukaa vizuri wala kuhudhuria masomo.