Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau washauri mwarobaini kukabili baa la njaa Afrika

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa nafaka na Mazao Mchanganyiko, Irene Mlola akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wadau wa bidhaa za mazao ya nafaka, pembeni ni Mkurugenzi wa Baraza la Nafaka Ukanda wa Afrika Mashariki (EAGC), Gerald Masila

Dar es Salaam. Wito umetolewa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi ili kuweka urahisi wa kuuza mazao ya nafaka kwa nchi zisizo na chakula au zilizotangaza kuwa na baa la njaa.

Wito huo umetolewa wakati ambao tayari Tanzania imeiuzia Zambia tani 650,000 za mahindi ikiwa ni hatua za kukabiliana na baa la njaa lililopo katika nchi hiyo.

Hayo yamesemwa leo Julai 16,2024  katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wa mazao ya nafaka, kampuni na wizara kutoka nchi za EA na baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo Malawi, Zimbabwe.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Baraza la Nafaka Ukanda wa Afrika Mashariki (EAGC), Gerald Masila amesema kuna  baadhi ya nchi zina akiba ya chakula na zenye  upungufu hivyo ni vyema kuangalia namna ya kuzisaidia.

“Nchi kama Uganda na Tanzania zina chakula cha kutosha na kuna nchi kama Zambia ambayo ina uhaba wa chakula inaweza kuangaliwa namna ya kuzisaidia nchi nyingine ambazo zina uhaba wa chakula ndani ya Afrika,” amesema Masila.

Amesema katika kushughulikia suala hilo ni vyema kuangalia baadhi ya sera zinazoweza kuoanishwa kwa sababu nchi zote zina lengo moja la kuhakikisha kunakuwa na uhakika na usalama wa chakula.

Makadirio yanaonyesha kuwa nchi zote za ukanda wa kusini mwa Afrika zina uzalishaji  na usambazaji wa bidhaa kuu za nafaka ikiwemo mahindi chini ya wastani, pia zinatarajiwa kutotosha kukidhi mahitaji ya kikanda kwa Mwaka wa Masoko 2024/25.

Malawi inatarajiwa kuwa chini ya wastani wa asilimia 45, Msumbiji asilimia 41, Afrika Kusini asilimia 10, Zimbabwe asilimia 55 na Zambia asilimia 34.

Amesema wananchi wa Afrika Mashariki pia wamekuwa na mahitaji ya bidhaa kama vile maharage ya soya ambayo yanapatikana nchini Malawi na Zambia, lakini marufuku iliyowekwa ya mauzo ya bidhaa za nafaka nje ya nchi zao imekuwa kizuizi.

“Kuna vikwazo bado katika biashara zinazovuka mipaka, wanachama wa EAGC walinunua soya tani 500 kutoka Zambia lakini walipotaka kusafirisha kulikuwa na zuio la kuuza mazao nje ya nchi, waliokuwa wamenunua hawakurudishiwa fedha na thamani yake ilikuwa zaidi ya Dola 60,000.”

Amesema kusingekuwa na vikwazo kama hivyo wakulima ndiyo wangenufaika sana na wafanyabiashara wangepata soko la uhakika la kuuza mazao yao.

Mkurugenzi wa Trade Mark Afrika Tanzania, Elibariki Shammy amesema wamekuwa wakihakikisha kuwa chakula kinachouzwa ni bora kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

“Vikwazo visivyo vya ushuru vinahusisha sana maeneo ya mipakani, urahisi wa bidhaa kupita bila kukaguliwa na mamlaka mbalimbali, muda unaotumika. Tunatakiwa kuangalia tunayofanya ukaguzi ili uwe katika namna ambayo unasaidia biashara kufanyika,” amesema Shammy.


Amesema ni vyema pia kuangalia namna teknolojia inavyoweza kutumika kuomba vibali mbalimbali ili kuwarahisisha wafanyabiashara kuviomba katika sehemu walizopo bila kulazimika kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Wakati hayo yakisemwa, Ofisa Kilimo kutoka Idara ya Masoko Wizara ya Kilimo, Dk Abel Mtembeji amesema kama nchi imeendelea kusimamia azma yake ya kuongeza uzalishaji na tija ili kuhakikisha chakula cha kutosha nchini na cha kuziuzia nchi jirani kinakuwepo.

“Juhudi mbalimbali zimefanyika katika kuhakikisha kuwa tunaongeza uzalishaji na tija ili kuhakikisha nchi inakuwa na chakula cha kutosha  na ziada ya kuuzia nchi jirani.”

“Juhudi mbalimbali zimefanyika katika kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ili kuhakikisha kuwa mabadiliko ya tabianchi hayaathiri uzalishaji,” amesema Dk Mtembeji.

Amesema jitihada hizo zimeenda sambamba na utafiti kwa ajili ya kupata mbegu bora zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi, kuhakikisha zinawafikia wakulima hususani wadogo na kuwapatia mbolea za ruzuku ili wazalishe kwa tija.