Wadau waitaka Serikali iwajibike kuwalinda wenye ualbino

Baadhi ya vijana wenye ualbino wakifrahia kwenye Summer camp jijini Mwanza. Picha Saada Amir

Muktasari:

  • Serikali na viongozi wa ngazi za juu wametakiwa kuyachukulia kwa uzito mkubwa matukio yanayowakabili watu wenye ualbino kwa kuwawekea ulinzi na usalama katika maeneo yao.

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku sita tangu kunyakuliwa kwa mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novatus (2) na watu wasiojulikana kijijini kwao Bulamula mkoani Kagera, baadhi ya wadau wameshauri kuwe na mikakati endelevu ya kuwalinda watu wenye ulemavu huo.

Asimwe alinyakuliwa kwenye mikono ya mama yake Mei 30, 2024 katika Kijiji cha Bulamula, Kata ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera na watu wasiojulikana na kutokomea naye pasipojulikana.

Kutokana na tukio hilo, wadau mbalimbali wakimo wabunge wa viti maalumu, watetezi wa haki za binadamu na Chama cha Wenye Ualbino Tanzania (TAS), wameitaka Serikali na viongozi wengine kulipa kipaumbele jambo hilo na kuwachukulia hatua kali wahusika.

Kutokana na hito huo, Serikali imesema itaendelea kulinda na kusimamia haki za watu.

Deogratius Ndejembi, waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, ametoa ahadi hiyo alipozungumza katika kikao na wabunge wa viti maalumu kundi la watu wenye Ulemavu, viongozi wa TAS pamoja na Taasisi ya Matumaini kwa wenye Ulemavu (FDH) jijini Dodoma, leo Juni 4, 2024.

Ndejembi amebainisha kuwa utaratibu wa kulinda watu wenye Ulemavu katika ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata na Wilaya utaendelea kutekelezwa kwa lengo la kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wote.

"Vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kudhibiti vitendo hivyo na kuwachukulia hatua kali za kisheria watakaobainika kufanya matukio hayo," amesema Ndejembi.

Pia, amepongeza jitihada zinazofanywa na uongozi wa Mkoa wa Kagera, Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na wananchi katika harakati za kumtafuta mtoto huyo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Stella Ikupa amesema Serikali inatakiwa kuwa na mipango mikakati amabayo ni endelevu itakayoweza kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu.

 “Haki ya kuishi ni ya kikatiba kwa kila Mtanzania na sisi watu wenye ulemavu pia ni Watanzania kama walivyo wengine, hivyo tuniomba Serikali isisite kuchukua hatua kali kwa wale wote ambao wamekuwa wakihusika na vitendo vya vya kikatili kwa watu wenye ulemavu,” amesema Ikupa.

Mkurugenzi wa FDH, Michael Hosea pia ameitaka Serikali kuchukua hatua za kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya wenye ulemavu.

 “Watu wenye ualbino tuna matumaini makubwa sana na Serikali kwamba itachukua hatua za kukabiliana na jambo hili,” amesema Hosea.

Kwa upande wake wakili na mtetezi wa haki za binadamu, Maduhu William amesema matukio yanayowakabilia watu wenye ualbino yanatakiwa kuingiliwa kati na viongozi wa juu wakiwepo mawaziri, wabunge na Jeshi la Polisi ili kuyakomesha.

"Tuna wawakilishi katika Bunge ambao wanatetea walemavu lakini wamekaa kimya baada ya tukio hili kutokea, tunawahitaji wapaze sauti na ikiwezekana uwe ni mjadala wa dharura," amesema Maduhu alipozungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Ofisa habari TAS, Godson Mollel amesema ili kukomesha matukio hayo washukiwa wa matukio wasiwe wanaachiwa hadi pale watakapotaja mtandao wanaoshirikiana nao.

"Ili kukomesha matukio haya Rais Samia akiingilia kati na kukubali adhabu ya kunyongwa kwa washtakiwa wa mauaji ya albino, hiyo itakuwa fundisho kwa wengine maana wataogopa kuwafanyia ukatili watu hao," amesema Mollel.

Katika hatua nyingine, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa wito kwa Serikali kupitia vyombo vyake vyote vya ulinzi na usalama kuhakikisha mtoto Asimwe anapatikana na wahusika wote wanafikishwa mbele ya sheria.

Wito huo umetoleo na Mkurugenzi wa kituo hicho Anna Henga kuwa Serikali inatakiwa kufanya upelelezi wa matukio yote na kuhakikisha unakamilika na wahusika wote wanafikishwa mahakamani.

"Kuwepo na mfumo madhubuti wa usalama wa watu wenye ualbino utasaidia kuibua matukio mengi yasiyoripotiwa na vyombo vya habari.

“Hii inatokana na ukweli kwamba baadhi ya familia za waathirika hukosa mfumo wa kutoa taarifa na kufuatilia ufanyiwaji wa matukio hayo," amesema Henga.