Wadau wagonga nyundo mabadiliko ya jina la tume ya uchaguzi

Muktasari:

  • Kampuni ya Mwananchi Communications Limited imeendesha mjadala wa X-Space uliokuwa na mada isemayo ‘Mbadiliko ya jina la Tume ni chachu kufanyika kwa uchaguzi huru?’ na kushirikisha wadau mbalimbali.

Dar es Salaam. Wanasiasa na wadau wa siasa nchini Tanzania wamesema, mabadiliko ya jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ni kuwahadaa imewadanganya wananchi.

Wamesema uchaguzi huru chini ya tume huru yenye mamlaka kisheria utaongeza ushindani na kuondoa ‘chawa na kunguni’ wanaojipendekeza nchini.

Mabadiliko ya jina la tume, yanakosolewa na wadau hao wanaosema jina pekee halikuwa hitaji la wananchi bali ni mfumo wa tume otakaoonyesha uhuru wa kweli na si jina.

Uwepo wa jina bila kubadilishwa mfumo, ndicho wanachosimamia wadau hao kupinga mabadiliko hayo wakisema kilichofanyika ni kinyume na matakwa ya Katiba ambayo inasema mabadiliko yeyote ya sheria lazima yaendane na Katiba, jambo ambalo halijafanyika.

Hoja hiyo ni kufuatia mjadala ulioendeshwa na Mwananchi leo Jumatano, Aprili 17, 2024 kupitia Jukwaa la Mwananchi X space (zamani Twitter) ikijadili mada isemayo ‘Mbadiliko ya jina la Tume ni chachu kufanyika kwa uchaguzi huru?’

Mjadala huo unachochewa na tangazo la Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi la kuanza kutumika kwa jina jipya la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuanzia Aprili 12, 2024.

Tangazo hilo ni baada ya kukamilika kwa mabadiliko ya sheria ya tume ya taifa ya uchaguzi iliyopitishwa na Bunge kisha kusainiwa na Rais kuwa sheria ambapo wadau walitaka mabadiliko ya jina yaambatane na muundo kwa mujibu wa Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na 2 ya mwaka 2024.


Anachosema Lema

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Gobless Lema akichangia mjadala huo amesema Serikali imefanya makusudi kuja na kitu ambacho ni kinyume na Katiba ili kizue mjadala.

Lema amesema kimsingi hakuna jina la tume linaloweza kutoa Tume bora ya uchaguzi kama tume ya uchaguzi haipo chini ya atiba huru na katiba bora katika taifa.

“Ili upate tume huru lazima uwe na katiba bora, katiba bora ambayo itatengeneza ‘balance’ ya nguvu kuanzia Bunge, Mahakama na Serikali yenyewe,” amesema.

Mbunge huyo wa zamani wa Arusha Mjini amesema katiba bora inayoweza kuwawajibisha na kutoa adhabu kwa kuzingatia vigezo na masharti ambazo zitajali haki, usawa na utu, chochote kitakachotengezwa chini ya katiba hiyo kitakuwa bora kwa sababu msingi wake umeshakuwa imara.

Lema amesema hakuna kitu kinacholeta amani kwenye nchi ni uchaguzi huru.

“Chama tawala kinapokuwepo kwenye mamlaka kikashindwa kuonyesha uongozi mzuri, kama nchi ina mifumo ya utawala bora, umma hauwazi kwenda porini, umma unawaza kulipa kisasi kwenye boksi la kura.

Hawa wamenunua magari ya Sh190 bilioni wakati mashine za kusafisha figo 300 zingepatikana, hawa tutakutana kwenye uchaguzi,” ameeleza Lema.

Lema amesema ili wananchi wafikie ujasiri huo uchaguzi lazima kuwa huru na haki.

“Umma ukikata tamaa hatuwezi kufanya mabadiliko ya masuala ya sera na mambo mengine ya msingi kwa njia ya uchaguzi, kinachotokea nini, kwa kufahamu au kutofahmu yanaweza kuzaliwa makundi mbalimbali ya uasi kwa sababu hakuna njia nyingine ya kupata utawala katika nchi kwa njia ya uchaguzi.

Kama njia ya uchaguzi haiwezi kutoa utawala wa watu kupiga kura, maana yake njia mbadala ni fujo,” amesema.

Lema amesisitiza kuwa kubadili Taifa na kujengwa Taifa la watu washindani akisema jambo hilo “haliwezi kufanikiwa kama mfumo wa uchaguzi haupo huru kuleta ushindani wenye kuondoa machawa, viroboto na kunguni.”

Hoja hizo zinaungwa mkono na Mwanahabari mkongwe, Dk Ananilea Nnkya akisema uchaguzi huru hauji kwa jina bali kilichopo ndani ya sheria ndio hufanya sheria kuwa huru au sio huru.

“Kwa jinsi sheria hiyo iliyopitisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2023 na kusainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan 2024, sioni ikitoa chachu ya uchaguzi huru,” amesema.

Dk Nnkya amesema tume yeyote ya uchaguzi haiwezi kuwa huru kama haina mfuko wake wa fedha.

Amesema tume inaomba fedha kwenye wizara au kwa mtu yeyote mtu inaweza kukwamishwa kwa sababu za kisiasa, uhuru wa tume ni masuala ya kisaiasa na hivyo inahitajika tume kuwa huru hasa ili kusiwepo mtu wa kuichezea.


Alichokisema Msuya

Mwandishi Mwandamizi wa Mwananchi, Elias Msuya akichokoza mjadala huo amesema sheria ya Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi imeundwa chini ya katiba inayolalamikiwa,

Msuya amesema Katiba ibara 74(1) inasema kutakuwa na Tume ya Uchaguzi, haijaeleza kama ni huru lakini Sheria inasema kutakuwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi sasa kumekuwa na malumbano ya hilo jina, watu wakisema hicho kifungu kinaeleza hali ya tume na sio jina.

Amesisitiza sheria hiyo iliyoanza kutumika Aprili 12, 2024 ibara ya tano inasema kutakuwa na uongozi ikitaja mwenyekiti na wajumbe lakini Tume imeanza kufanya kazi bila hao wanaotajwa.

Msuya amesema uhuru wa tume hauundwi na jina bali muundo.

“Tume kwenye katiba inayolalamikiwa hatuwezi kuwa na tume huru,” amesema.

Naye Macheyeki Filbert amesema kinachofanya uchaguzi kuwa huru sio jina la tume, kilichofanywa na Serikali ni kubadili chupa wakati pombe ni ileile.

“Wadau walitoa mapendekezo wakitarajia mabadiliko makubwa yatakayoondoa malalamiko ya muda mrefu ya udanganyifu kwenye uchaguzi na wizi wa kura lakini hayajatokea,” amesema.