Wabunge watoa ushauri malipo ya wenza wa vigogo
Muktasari:
- Baada ya Serikali kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba Nne ili pamoja na mambo mengine kutoa kiinua mgongo kwa wenza wa vigogo wastaafu, Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeshauri kuondolewa kwa baadhi ya maneno.
Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeshauri Serikali kuondoa maneno kiinua mgongo na kuandika malipo ya fadhila kwenye mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mafao ya Kustaafu katika Utumishi wa Kisiasa, inayolenga kuweka malipo kwa wenza wa vigogo wastaafu.
Mapendekekezo hayo ambayo yapo katika muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba nne wa mwaka 2023, yanalenga katika kuongeza kwa vifungu vipya vya 9A, 12A, na 14A kuwawezesha wenza wa Rais Mstaafu, Makamu wa Rais Mstaafu, na Waziri Mkuu Mstaafu kulipwa kiinua mgongo wakati wa kipindi cha uongozi wa wenza wao.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Florent Kyombo amesema hayo leo Jumanne Oktoba 31, 2023 wakati akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba nne wa mwaka 2023.
Kyombo amesema kamati ilipendekeza kutotumia maneno kiinua mgongo (Gratuity) kwa kuwa maneno hayo kwa muktadha wa sheria hiyo yanatumika kuwalipa watumishi wa umma.
Watumishi hao wa umma wametajwa kuwa ni Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Naibu wa Spika, Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya.
“Kamati iliishauri Serikali kutumia maneno malipo ya fadhila (ex-gratia) kuakisi lengo linalokusudiwa,”amesema.
Aidha, Kyombo amesema Ibara ya 51 inarekebishwa ili kuwaimarishia ulinzi Makamu wa Rais Mstaafu na Waziri Mkuu Mstaafu pamoja na familia zao za karibu.
Amesema hata hivyo maneno ‘familia ya Karibu’ hayakupewa tafsiri rasmi kwenye sheria hiyo na ili kutoleta tafsiri ambazo hazikukusudiwa.
Amesema kutokana na ufafanuzi wa Serikali kuwa wanakusudia kuimarisha ulinzi kwenye makazi ya viongozi hao wastaafu, Kamati iliishauri Serikali kutumia neno ‘makazi’ kama mbadala wa maneno ‘familia ya Karibu’.
Kyombo amesema Serikali ilikubaliana na ushauri wa kamati na wamefanya mabadiliko kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na Kamati. “Kamati inaipongeza Serikali kwa kufanya mabadiliko ya kufuata maneno ‘kiinua mgongo’ na kuandika maneno ‘malipo ya fadhila’ na kufuta maneno ‘familia ya karibu’ na kuandika neno ‘makazi’.
Awali akiwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba tatu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk Eliezer Feleshi amesema sehemu ya sita ya muswada huo, inapendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Mafao ya Kustaafu katika Utumishi wa Kisiasa.
Amesema katika mabadiliko hayo wanapendekeza kufanya marekebisho ya kifungu namba 14, ili kuwezesha mawaziri wakuu wastaafu, waliostafu kabla ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Mafao ya Kustaafu katika Utumishi wa Kisiasa kwa mwaka 1999 kuwa na wasaidizi kwa ajili ya kuwasaidia kwenye kazi zao.
“Kifungu cha 18 kinapendekeza kurekebishwa ili kuweka utaratibu wa mwenza wa spika mstaafu aliyefariki kupekea mafao ya pensheni ya kila mwezi,”amesema.
Amesema katika sehemu ya saba ya muswada huo inapendekeza kufanyiwa kwa marekebisho kwa Sheria ya Utumishi wa Umma.
Amesema lengo ni kutamka kuwa Rais anayeingia madarakani, makamu wa Rais anayeingia madarakani au Waziri Mkuu aliyeteuliwa ambaye ni mtumishi wa umma kustaafu katika utumishi wa umma kwasababu za kiusalama pale mwenza wake anaposhika wadhifa husika.
Amesema pia wanapendekeza kurekebishwa ili kumwezesha mjane au mgane wa Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu aliyefariki kulipwa mafao ya pensheni ya kila mwezi.