Wabunge wataka hatua zaidi athari za mafuriko

Wananchi wa mtaa wa sokoni Kata ya Mji Mpya, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wakiendekea kutoa kwenye maeneo yao maji na tope yaliyotokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia leo Aprili 25 ,2024. Picha na Florah Temba

Muktasari:

  • Serikali yasema mpango umeandaliwa kuchimba mabwawa kukusanya maji kwa ajili ya umwagiliaji, uvivu na kunyweshea mifugo.

Dodoma. Wabunge wameitaka Serikali kuchukua hatua zaidi kutatua athari zinazotokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.

Wamesema hayo bungeni Dodoma leo Alhamisi Aprili 25, 2024 katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu baada ya kuwasilishwa taarifa ya Serikali kuhusu athari za mafuriko.

Mbunge wa Viti Maalumu, Tunza Malapo katika swali lake amesema badala ya kuacha utashi wa mzazi pekee ama kumpeleka shule au kutompeleka kutokana na hali mbaya ya hewa, kwa nini mamlaka za chini zisiwe zinatoa taarifa za uwepo wa mvua kubwa katika maeneo yao, hivyo watoto wote wasiende shuleni ili kuepusha madhara.

Akijibu swali hilo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ni jukumu la kamati za maafa za ngazi za chini kutoa taarifa ya hali ya hewa ili kuepusha madhara hayo.

“Wakuu wa wilaya na mikoa wajenge utamaduni wa kuwa na mawasiliano na kutoa taarifa wakati wote wanapokuwa na taarifa za hali ya hewa kuwa mbaya katika eneo hilo,” amesema.

Amewataka viongozi hao wafuatilie taarifa za hali ya hewa katika maeneo yao katika kipindi chote hadi Mei, 2024.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumatano Aprili 24, 2024 kuhusu hatua zinazochukuliwa, alisema Serikali imezisihi shule kuchukua hatua za tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, ikiwemo kutowalazimisha watoto kwenda shule kama hali imeonekana kuwa mbaya kwa siku husika.

Alisema wazazi wana haki ya kutoruhusu watoto kwenda shule endapo watakuwa na wasiwasi na hali ya hewa ya siku husika.

Profesa Mkenda alisema tangu mvua zianze kunyesha kumekuwa na changamoto ya wanafunzi kufika shule, hali iliyozilazimu baadhi ya shule kuwapumzisha watoto kwa muda.

Mbunge wa Morogoro Kusini, Innocent Kalogeresi amehoji nini mpango wa Serikali wa kukabiliana na mafuriko yanayojitokeza kila mwaka mkoani Morogoro.

Amehoji Serikali ina mpango gani wa kuchimba mabwawa ili kupunguza kasi ya mito mingi iliyopo Mkoa wa Morogoro inayoleta maafa kwa watu na Serikali kutumia fedha kukabiliana na majanga.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zimeshaandaa mpango wa kuchimba mabwawa kukusanya maji kwa ajili ya umwagiliaji, uvivu na kunyweshea mifugo.

“Tayari wataalamu wako huko kuona maeneo sahihi ya kuchimba ili kuchepusha maji kutoka kwenye mfereji mkubwa wa Rufiji kupeleka kwenye mabwawa. Mkakati huo unaendelea mpaka uelekeo wa Mto Wami kupitia mfereji huo wanachimba bwawa la Kidunda kwa ajili ya matumizi ya maji ambayo yataingia Dar es Salaam,” amesema.

Amesema maeneo ya Rufiji wametenga fedha za kuchimba mabwawa.

Waziri Mkuu amesema wataendelea kuchimba mengine katika bonde la Ruvuma na Nyasa. Amesema wizara zitaendelea kuongezewa bajeti kadri fedha zitakavyopatikana.