Waandishi wajitosa kukabili mabadiliko ya tabiachi
Muktasari:
- Serikali imeipa kongole Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa kilimanjaro (Mecki) kwa kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira.
Moshi. Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Kilimanjaro (Mecki) imeadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kupanda miti maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye chemi chemi ya Miweleni.
Upandaji miti hiyo ni jitihada za kuunga mkono Serikali katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira.
Pamoja na hayo imetaka jamii, wenyeviti wa vijiji pamoja na watendaji wa maeneo hayo kuitunza miti hiyo ili iweze kukua vizuri na kufanikisha lengo.
Kufuatia shughuli hiyo, Serikali imeipongeza Mecki kwa kuona umuhimu wa kupanda miti katika maeneo hayo korofi.
Akizungumza leo Jumapili, Juni 2, 2024 kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Ofisa Tarafa Moshi Magharibi, Senzia Msafiri ameipongeza klabu hiyo.
"Kweli niwape kongole kwa kuona umuhimu wa kupambana na uharibifu wa mazingira kwa kupanda miti maeneo mbali mbali huu ni uzalendo, mmeenda sambamba na kauli mbiu yenu inayosema waandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Senzia.
Amewaeleza wanahabari kuwa wao ni mashahidi wa mkoa huo kiwango cha joto kipo juu tofauti na kipindi cha nyuma, hali inayosababishwa na ukataji miti hovyo na uchomaji wa mkaa.
“Serikali tukiona watu wenye taaluma mnajitolea kufanya shughuli kama hizi kwetu ni faraja sana, tunawapongeza na wengine waige jambo kama hili, tunza mazingira yakutunze mmefanya jukumu zuri,” amesema.
Senzia amewataka wasiishie hapo, bali liwe hatua endelevu, “sisi jukumu letu ni kuitunza, tutawasiliana na wenyeviti wa vijiji na watendaji kuhakikisha hii miti inakuwa.”
Ramadhani Bingwa kutoka bodi ya maji Bonde la Pangani kitengo cha mazingira, amesema chanzo hicho cha chemi chemi ya Miwaleni kimepakana na vijiji vitatu, hivyo kuwaomba viongozi wa maeneo hayo kulinda miti hiyo ili tija iweze kuonekana.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisakisangeni, Alen Mshana amesema watatekeleza na kuhakikisha miti hiyo inakuwa kwa kuizungushia uzio kwani maji ya chanzo hicho wananufaisha watu wengi.
Akiwasilisha taarifa ya klabu hiyo, Sia Lyimo, amesema wamepanda miti zaidi ya 500 katika maeneo ya Kijiji cha Miwaleni, Wilaya ya Moshi mkoani hapa kama ishara ya maadhimisho hayo.
Amesema klabu katika kuendana na kauli mbiu ya mwaka huu inayosema waandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, imetoa miche ya miti 1,000 katika Shule ya Polisi Moshi (CCP).