Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vijana 500 wa Mwanza wamepewa mchongo kujikwamua

Muktasari:

  • Vijana hao wanatarajia kunufaika na ujuzi wa kuchakata taka, kukuza masoko ya biashara zao kidijitali na stadi za maisha jijini Mwanza.

Mwanza. Vijana zaidi ya 500 wa Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya uchakataji taka, stadi za maisha, ujuzi wa kidijitali, mitaji na vifaa, katika mpango wa kuwawezesha kujiajiri na kukuza biashara kwa njia ya teknolojia.

Mafanikio hayo yanakuja kupitia Programu ya Green and Smart Cities SASA yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 75, inayotekelezwa kwa miaka mitano katika majiji mawili ya Mwanza, Tanga pamoja na Pemba kwa ufadhili wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU).

Akizungumza jana Aprili 10, 2025, wakati wa uzinduzi wa ofisi za programu hiyo jijini Mwanza, Mratibu wa Programu ya SASA Manispaa ya Ilemela, Ahmed Sakibu amesema vijana hao watafaidika kwa awamu mbalimbali. Wengi wao watafundishwa uchakataji wa taka, wengine ujuzi wa kidijitali na kundi jingine litapatiwa nafasi katika vyuo vya mafunzo ya ufundi.

“Kati ya vijana 500, zaidi ya 150 watajifunza ujuzi wa kidijitali, 200 watafundwa kuchakata taka za chakula na kuzigeuza mali. Wengine 150 watapelekwa vyuo vya Veta na Feta kwa miezi sita ili wapate ujuzi wa kujiajiri,” amesema Sakibu.

Ameongeza kuwa, kupitia programu hiyo, miradi mikubwa minne ya kimkakati itatekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa gharama ya takribani Sh43 bilioni. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa soko la kisasa la Buswelu, uboreshaji wa soko la samaki Mwaloni na miundombinu ya mwalo katika maeneo ya New Igombe na Old Igombe.

Meneja wa Miradi kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Ubelgiji (Enabel), Kikolo Mwakasungula amesema mradi huo utasaidia vijana na akina mama wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi, uchakataji taka na biashara ndogo ndogo ili kuanzisha biashara, kuzirasimisha na kupata mitaji.

Katibu Tawala msaidizi upande wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Mwanza, Patrick Karangwa (kushoto) na Mkuu wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Marc Stalmans (kulia) wakipeana mkono baada ya kuzindua ofisi ya Mwanza ya mradi wa Green and Smart Cities SASA Program unaotekelezwa na jumuiya hiyo. Picha na Damian Masyenene

“Taka ni fursa. Wapo wajasiriamali wanaookota taka za plastiki, tunaweza kuwapatia mashine ndogo kwa ajili ya kuchakata na kuongeza thamani. Mwanza kuna uchafu mwingi unaotokana na uvuvi, ambao unaweza kutumika kama fursa kutengeneza mbolea,” amesema Mwakasungula.

Meneja wa Utekelezaji kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Dk Fred Lerise, amesema zaidi ya asilimia 80 ya taka zinazozalishwa mijini zinaweza kuchakatwa na kutumika kama rasilimali za kibiashara. Alihimiza kaya kuanza kutenganisha taka ili zisiharibike mapema na zipate soko kwa urahisi.

“Taka tuzione kama mali. Tukizitenganisha tangu nyumbani zitakuwa salama kwa ajili ya kuchakatwa. Wakusanyaji wa taka wanapaswa kuwa na vifaa vya kuchambua taka kama ozeshi, vyuma chakavu, na vifaa vya kielektroniki. Hii itawasaidia kuzipata zikiwa safi na kuokoa muda wa kuzisafisha,” amesema Dk Lerise.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza anayesimamia Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Patrick Karangwa, mradi huo unatekelezwa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kama Veta, Feta na Sido ili kutoa mafunzo ya fani mbalimbali ikiwemo ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na uzalishaji wa bidhaa kwa kutumia taka.

“Mpango huu utachangia maendeleo endelevu. Mbali na kuongeza ajira, pia utaongeza mapato ya Serikali kwa kutumia teknolojia za kidijitali kuboresha utendaji kazi katika halmashauri na miongoni mwa wananchi,” amesema Karangwa.

Mmoja wa wanufaika wa programu hiyo, Praxeda Mgyabuso, ambaye ni mzalishaji wa sabuni wilayani Ilemela, amesema kupitia programu hiyo ameongeza ufanisi kwenye biashara yake kwa kutumia stadi za kidijitali kutangaza bidhaa zake kupitia vipeperushi na stika alizojifunza kutengeneza.

“Sasa naweza kuandaa vipeperushi, stika na kutumia mitandao ya kijamii kuwafikia wateja zaidi. Hii imenisaidia kukuza mtandao wa biashara na kuongeza mauzo,” amesema Mgyabuso.

Mbali na kuwawezesha vijana, programu hiyo inalenga pia kuboresha miundombinu ya masoko ikiwemo Soko la Kirumba, machinjio na Mwalo wa Igombe, huku ikiendeleza matumizi ya teknolojia ya kisasa katika shughuli za biashara na ujasiriamali.