Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vigogo CWT waendelea kusota rumande, DPP akisubiriwa

Muktasari:

  • Vigogo wanane wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wameendelea kusota rumande kwa takribani miezi miwili baada ya upande wa Jamhuri kueleza kuwa upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi na rushwa haujakamilika, huku kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kikisubiriwa.

Dodoma. Vigogo wanane wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wameendelea kushikiliwa rumande baada ya upande wa Jamhuri kueleza kuwa upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi na rushwa inayowakabili bado haujakamilika.

Upande umeieleza mahakama kuwa unasubiri kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kuendelea na hatua zinazofuata za shauri hilo.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Mei 25, 2026 na kusomewa mashtaka 14 ya uhujumu uchumi na rushwa. Hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Washtakiwa ni aliyekuwa Rais wa CWT, Leah Ulaya, Rais wa sasa wa CWT, Suleiman Ikomba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maganga Japhet, Katibu Mkuu wa sasa, Joseph Misalaba, Nashon Kidudu, Baraka Mbonalibha, Wambura Kihengu, Angelina Wambura pamoja na kampuni ya Pyrite and Industries Company Limited.

Shauri hilo lilipotajwa jana Julai 9, 2026, Wakili wa Serikali, Gothard Mwingira aliiambia mahakama kuwa upelelezi umefikia hatua za mwisho, lakini haujakamilika, hivyo akaiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.

Hata hivyo, mawakili wa utetezi walipinga maelezo hayo wakidai upande wa Jamhuri umekuwa ukitoa sababu hiyo kwa muda mrefu bila kueleza ni lini hasa upelelezi utakamilika na lini kibali cha DPP kitapatikana.

Wakili Sedrick Mbunda amedai kuwa hati ya mashtaka ina maelezo ya kina, ikiwemo namba za miamala, kiasi cha fedha, tarehe na muda wa miamala hiyo, hivyo akahoji sababu ya kuendelea kwa upelelezi.

"Kwa nini mnawaleta watu mahakamani wakati upelelezi haujakamilika? Kamilisheni kwanza upelelezi ndipo mje kuwafungulia mashtaka," amesema Mbunda.

Kwa upande wake, Wakili Meshack Ngamando amesema mahakama imekuwa kama sehemu ya kuwahifadhi washtakiwa huku upelelezi ukiendelea bila kikomo, jambo alilodai linawanyima haki wateja wake.

Amesema washtakiwa hao ni watumishi wa umma wenye makazi yanayofahamika, hivyo wasingeweza kutoroka iwapo wangeachiwa wakati upelelezi ukiendelea.

Akitoa uamuzi, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Denis Mpelembwa, ameutaka upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi na kupata kibali cha DPP kitakachoelekeza mahakama yenye mamlaka ya kuendelea kusikiliza shauri hilo.

Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Julai 23, 2026. Washtakiwa wataendelea kusalia rumande kwa kuwa makosa yanayowakabili hayana dhamana.