VIDEO: Moto wateketeza nyumba ya vyumba 12 Moshi

Mwonekano wa nyumba iliyoungua alfajiri ya leo Mei 17,2024 mjini Moshi.

Muktasari:

  • Moto huo ambao unadaiwa kuanza kuwaka saa 10:44 alfajiri Mei 17,2024, eneo la  katikati ya mji wa Moshi, umeteketeza vyumba 12 vya biashara, jiko na baa.

Moshi. Moto  ambao chanzo chake bado hakijajulikana, umeteketeza nyumba ya biashara yenye vyumba zaidi ya 12, baa na jiko.

Nyumba hiyo ambayo ipo katikati ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ilianza kuwaka moto saa 10 alfajiri ya kuamkia leo Ijumaa Mei 17, 2024.

Hata hivyo, baadhi ya mashuhuda wameiambia Mwananchi Digital kuwa moto huo ungeweza kudhibitiwa haraka kama magari ya zimamoto yangekuwepo ya kutosha.

Akizungumza akiwa eneo la tukio, Mkaguzi Hassan Wakuchegura kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, amesema walipokea taarifa ya moto huo saa 10:44 alfajiri, wakati huo gari la zimamoto lilikuwa wilayani Mwanga kwenye tukio lingine.

Hata hivyo, Wakuchengura amesema gari hilo lilifika licha ya kwamba lilichelewa, lakini walijitahidi kuudhibiti moto huo.

“Saa 10:44 tulipata taarifa kuna jengo linalohusika na baa na maduka ya vifaa vya ujenzi linawaka moto, wakati huo gari ya zimamoto lilikuwa linatokea kwenye tukio lingine Mwanga ambako gari ya gesi ilikuwa ikiwaka moto, tulifika eneo la tukio na kuanza kupambana na moto huo,” amesema.

Moto wateketeza nyumba ya vyumba 12 Moshi

Naye shuhuda wa moto huo, Noreen Charles amesema alianza kusikia vitu vikipasuka na alipotoka nje ndipo akaona moto mkubwa ukiwaka upande wa jikoni.

“Niliita watu, lakini hawakuweza kuuzima,  nilikimbilia polisi wakasema gari ya zimamoto inakuja na mpaka wanafika moto ulikuwa umeshakuwa mkubwa na tayari paa lilikuwa limeanguka,” amesimulia Noreen.

Mmiliki wa eneo hilo, Benjamini Abdi amelalamika licha ya kutoa taarifa mapema lakini gari la zimamoto lilichelewa kufika hali iliyosababisha aingie hasara kubwa.

"Tulipiga simu zimamoto tukaambiwa gari limeenda kuzima moto Mwanga lakini liko njiani linakuja,  limefika tayari moto umeshateketeza vyumba 12 vya biashara, jiko na baa vyote vimeteketea,” amesema Abdi.

Hata hivyo, ameishauri Serikali iuongezee mkoa huo  magari ya zimamoto badala ya kuendelea kutegemea gari moja.

“Kwa mfano hapa kwangu, kwa muda tuliotoa taarifa kama gari lingine lingekuwepo, huenda haya madhara makubwa yasingekuwepo,” amesema Abdi.

Aidha amesema kwa sasa hawezi kusema nia hasara kiasi gani amepata kwa sababu ni mapema mno.