VIDEO: 'Boni Yai’ apandishwa kizimbani Kisutu

Boniface Jacob maarufu 'Boni Yai' akiwa kizimbani. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Aliyekuwa meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob maarufu kama ‘Boni Yai’ tayari amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Ni jioni ya leo Alhamisi, Septemba 19, 2024 na anasubiri hakimu aingie mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashtaka yanayomkabili.
Jopo la waendesha mashtaka mawakili wa Serikali wakiongozwa na Job Mrema pamoja na jopo la mawakili wa Jacob linaloongozwa na Peter Kibatala wapo ndani ya ukumbi wa mahakama sambamba na wanachama wa Chadema.
Boni Yai alikamatwa jana Jumatano, maeneo ya Sinza na Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam na kumpeleka Kituo cha Polisi cha Osterbay. Kisha usiku wa jana alipelekwa nyumbani kwake Mbezi Msakuzi kwa upekuzi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime katika taarifa aliyoitoa jana Septemba 18, 2024 alisema jeshi hilo limemkamata na linamshikilia Jacob, mkazi wa Mbezi Msakuzi, jijini Dar es Salaam kutokana na makosa ya kijinai anayotuhumiwa nayo.
Endelea kufuatilia mitandao na tovuti ya Mwananchi.