Utapeli wa ajira watinga Iringa, wawili watiwa mbaroni, vijana 75 waokolewa
Vijana 75 kutoka mikoa tofautitofauti waliotapeliwa na kampuni ya Q-NET wakiwa katika kituo cha Polisi mkoani Iringa baada ya Watuhumiwa kukamatwa. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Operesheni hiyo, Jeshi la Polisi mkoani Iringa wamesema wamewaokoa watu 75 waliokuwa wameathirika na mtandao huo, wakiwemo wanawake 36 na wanaume 39 na wengine ambao ni vijana wa umri wa kati ya miaka 20 hadi 30, waliotoka katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Mwanza, Lindi, Njombe, Mtwara na Mafia.
Iringa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limewakamata watu wawili wanaotuhumiwa kuongoza mtandao wa utapeli unaowalenga vijana kwa kisingizio cha kuwapatia ajira.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi wakati akizungumza na waandishi wa habari Aprili 2, 2026 amesema operesheni hiyo maalumu ililenga kudhibiti vitendo vya uhalifu na imezaa matunda baada ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao wawili.
Watuhumiwa waliotajwa ni Jackson Kalu (26), mkazi wa Bahi mkoani Dodoma, na Michael Mfuse (32), mkazi wa Wanging’ombe mkoani Njombe ambapo inadaiwa kuwa Mfuse alikamatwa akiwa na gari aina ya BMW X1, ambalo linahusishwa na shughuli hizo, pamoja na nyaraka mbalimbali zinazodaiwa kuwa za kampuni ya Q-NET.
Katika operesheni hiyo, polisi pia wamesema waliwaokoa watu 75 waliokuwa wameathirika na mtandao huo, wakiwemo wanawake 36 na wanaume 39 na wengine waathirika hao ni vijana wa umri wa kati ya miaka 20 hadi 30, waliotoka katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Mwanza, Lindi, Njombe, Mtwara na Mafia.
Imeelezwa kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakiwarubuni vijana kwa ahadi za ajira ndani na nje ya nchi na baada ya kuwashawishi, waliwataka kufika Iringa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni hatua za kuanza kazi au safari ya kwenda nje ya nchi.
Kamanda Bukumbi amesema walipofika Iringa, vijana hao waliingizwa katika mfumo wa mafunzo na kupewa masharti ya kutoa fedha kuanzia shilingi 600,000 hadi milioni 4, wakielezwa kuwa ni gharama za usajili na kuanza biashara.
Aidha imeelezwa kuwa vijana hao waliaminishwa kuwa wakifanikiwa kuingiza watu wengine wawili, wangeweza kurejeshewa fedha zao pamoja na kupata faida.
Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa waathirika hao waliishi katika mazingira magumu, ambapo baadhi yao walilazimika kulala zaidi ya watu 10 katika chumba kimoja wakisubiri kuanza kwa shughuli hizo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa, SCAP Allan Bukumbi akizungumza na waandishi wa habari kituoni hapo juu ya sakata la kuwakamata Watumumiwa wa utapeli wa kuahidi ajira hewa kwa vijana 75. Picha na Mtandao
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi limewataka wazazi na walezi wenye watoto waliopotea baada ya kuahidiwa ajira kufika Kituo Kikuu cha Polisi Iringa kwa ajili ya utambuzi wa waliokolewa huku likisisitiza wazazi kuwa makini na kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao ili kuepuka matukio ya aina hiyo.