Ushahidi waeleza Padri Rwegoshora alimuahidi ‘shangingi’ baba wa Asimwe

Washtakiwa 9 wa kesi ya mauaji ya mtoto mwenye Ualbino Asimwe Novath wakiwa wanasomewa mwenendokabidhi katika Mahakama ya wilaya Bukoba mkoani Kagera.
Kagera. Upande wa Jamhuri katika kesi ya mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2) umewasilisha maelezo ya ushahidi katika hatua ya awali, ukieleza utakuwa na mashahidi 52 na vielelezo 37.
Katika maelezo hayo ya ushahidi, mmoja wa mashahidi ameeleza mbinu iliyotumiwa na washtakiwa kumpora mtoto huyo na kutokomea, pia ikitajwa ahadi ya gari aina ya Toyota V8, maarufu kama shangingi, kwa baba wa mtoto.
Asimwe aliporwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwao Kijiji cha Bulamula, Kata ya Kamachumu wilayani Muleba mkoani Kagera, Mei 30, 2024 saa 2:00 usiku na kutokomea naye kusikojulikana.
Siku 17 baadaye mabaki ya mwili wake yalipatikana yakiwa yamefungwa kwenye mfuko wa sandarusi (kiroba) na kutelekezwa chini ya kalavati lililoko Barabara ya Makongora, Kitongoji Kabyonda, Kata ya Ruhanga wilayani humo.
Siku kadhaa baadaye, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa ya kuwashikilia watu tisa akiwemo baba wa marehemu, Novath Venanth na Padri Elpidius Rwegoshora na kuwafungulia kesi ya mauaji namba 17740/2024, katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba mkoani humo.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Nurdini Masudi, Ramadhani Selestine, Rweyangira Alphonce, Dastan Bruchard, Faswiu Athuman, Gozbert Alikad na Desdery Everigist wote wakazi wa mkoani Kagera.
Shauri hilo linatarajiwa kufikia hatima yake ya usikilizwaji katika Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.
Wakili Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Bukoba kuwa shahidi aliyepewa jina ‘P24’ ambaye ni askari wa Jeshi la Polisi, katika maelezo yake ya ushahidi amesema wakati akimchukua maelezo mshtakiwa wa nne katika shauri hilo (Ramadhani Selestine) alikiri kuhusika katika mauaji ya mtoto huyo.
Katuga amedai shahidi huyo kwenye maelezo aliyomchukua Ramadhani alikiri kuwa akiwa na mshtakiwa mwenzake Nurdini Masudi walienda hadi Kijiji cha Bulamula ilipokuwa inaishi familia hiyo na kuzima kibatari kilichokuwa kikwaka na kumkaba mama wa marehemu (Asimwe) akiwa gizani kisha kumpora mwanaye na kutokomea naye.
“Shahidi P24 ameeleza kuwa mshtakiwa namba tano alieleza walivyopanga, kuwa wakifika nyumbani kwa mama wa mtoto mmoja amuite kwa sauti kuwa ameng'atwa na nyoka huku akilia kuhitaji msaada na mama huyo akitoka basi mwenzake aingie ndani na kuchukua mtoto,” amedai.
Kwa mujibu wa wakili Katuga, shahidi alielezwa na washtakiwa kuwa baada ya kumpora mtoto huyo walikimbia, huku wakiwa wamemfunga mdomo asipige kelele, jambo lililosababisha afariki dunia kwa kukosa hewa.
Amedai baada ya kufanikiwa kwenye mauaji ya mtoto huyo na kumkata baadhi ya viungo vyake vya mikono ikiwemo viganja viwili ,taratibu za kutafuta mteja wa kuvinunua zilizokuwa zikiratibiwa na Padri Rwegoshora zilizaa matunda baada ya padre huyo kudai mteja ameshapatikana.
Katuga anadai shahidi ‘P28’ kwenye maelezo yake alidai mshtakiwa namba tano alisema kuwa Padri Rwegoshora alimwambia apeleke viungo hivyo Bukoba ambako alikuwepo mteja na endapo akikamatwa akiwa njiani, basi anywe sumu kwa lengo la kujitoa uhai ili kupoteza ushahidi.
Shahidi anadai mshtakiwa namba tano baada ya kukamatwa pamoja na wenzake, alikunywa sumu hiyo inayosadikiwa kuwa ni ya kuua panya, hata hivyo hakufariki baada ya askari wa Jeshi la Polisi kumuwahi na kumpatia huduma ya kwanza.
Wakili mwingine wa Serikali, Erick Mabagala akisoma maelezo ya awali ya mshtakiwa namba mbili ambaye ni baba mzazi wa marehemu, Novath Venant amedai mshtakiwa kwenye maelezo yake alikiri kushiriki kupanga njama za kumuiba mtoto wake na Padri Rwegoshora.
Amedai mshtakiwa huyo alisema ili kufanikisha lengo hilo Padri Rwegoshora alimpatia ahadi ya kumpatia Sh30 milioni, gari aina ya V8 (Toyota Land Cruiser) nyeusi na ahadi ya kuhamishwa kutoka katika kijiji hicho kwenda kuishi Dar es Salaam endapo angefanikisha utekwaji wa mtoto huyo.
Amedai ushahidi wa mashahidi hao 52 na maelezo waliyoandika washtakiwa wote yameonyesha wazi jinsi walivyoshiriki katika mauaji ya mtoto mwenye ualbino Asimwe.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi, Eliapokea Wilson amesema mchakato wa mwenendo wa usikilizwaji wa ushahidi huo umekamilika na shauri hilo litahamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.
“Taratibu za mwenendo kabidhi zimekamilika na washtakiwa wote tayari mmejulishwa ushahidi utakaowasilishwa na Jamhuri kwenye kesi hii. Hivyo washtakiwa wote mnarudishwa rumande mpaka mtakapotaarifiwa kwenda Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikiliza kesi yenu,” amesema hakimu.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba Agosti 21, 2024, mbele ya Jaji Gabriel Malata ilikubali ombi la Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) la kuzuia kutumika kwa majina na taarifa za mashahidi katika kesi hiyo.
Uamuzi wa Mahakama ulitokana na maombi ya DPP kupitia maombi ya jinai namba 23143 ya 2024 ambayo yalisikilizwa chemba ili kulinda usalama wa mashahidi na ndugu zao, kwani kumekuwa na tishio la kiusalama dhidi yao.
DPP katika maombi hayo alieleza kumekuwapo majaribio mbalimbali kutoka kwa washirika wa washtakiwa kupata majina na utambulisho wa watu ambao wanaweza kuwa mashahidi, kwa lengo la kuwadhuru ili wasitoe ushahidi wao.
Jaji Malata amezuia matumizi ya nyaraka ambazo zinaweza kutoa utambulisho wa mashahidi na nyaraka hizo zitafanywa siri katika hatua zote za usikilizwaji wa shauri hilo.
Jaji Malata katika uamuzi wake alisema usambazaji na uchapishaji wa taarifa yoyote ya ushahidi wa nyaraka na ushahidi mwingine wowote ambao utahusu utambulisho wa mashahidi wa Jamhuri hautaruhusiwa kabisa.
Si hivyo tu, pia uchapishaji na usambazaji wa taarifa yoyote ambayo inaweza kubainisha eneo, makazi na mahali walipo mashahidi wa upande wa mashitaka au ndugu yeyote wa karibu wa mashahidi hao umepigwa marufuku.
Katika uamuzi huo, Jaji Malata alisema usikilizwaji wa kesi hiyo utafanyika faragha, pia kupitia video conference, matumizi ya sauti au upotovu wa uso na kutoa utambulisho wa mashahidi hautaruhusiwa.
Kiapo cha RCO Kagera
Katika maombi hayo, DPP aliambatanisha kiapo cha Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Kagera, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Boniface Kibuga ambaye katika kiapo hicho alijenga hoja za kuishawishi Mahakama kukubali ombi hilo.