Prime
Ukurasa mpya Z’bar wafunguliwa rasmi
Muktasari:
- Pande mbili zimekubaliana mazingira ya Zanzibar yanahitaji ushirikiano utajaojenga umoja, mshikamano na maridhiano ya dhati yenye amani na utulivu endelevu wa kuunda kamati ya pamoja ya majadiliano kwa mujibu wa ratiba iliyokubaliwa
Zanzibar. Ukurasa mpya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) umefunguliwa baada ya viongozi wa ACT-Wazalendo na Chama cha Mapinduzi (CCM) kusaini tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa Zanzibar.
Tamko hilo lenye vipengele saba limesomwa na kutiwa saini leo, Alhamisi, Julai 9, 2026, katika Ikulu ya Zanzibar na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mansura Mosi Kassim.
Hatua hiyo inaashiria mwanzo wa ukurasa mpya katika siasa za Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano, maelewano na maridhiano ya kisiasa kati ya pande hizo.
Utiaji saini umeshuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi na viongozi waandamizi wa CCM na ACT- Wazalendo, mabalozi na pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.
Miongoni mwa mambo hayo ni kujenga imani na kuaminiana, kupitia upya Katiba ya Zanzibar, mfumo wa uendeshaji wa uchaguzi, utumishi wa umma, mfumo wa utoaji haki na Serikali za mitaa.
Kabla ya kusoma tamko hilo, Mansura amesema jumla ya vikao tisa vya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa Zanzibar vilifanyika kuanzia Novemba 9, 2025, vikuhusisha marais wastaafu wa Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein.
Lakini kwa upande wa ACT-Wazalendo mazungumzo yaliongozwa na Juma Duni Haji (mwenyekiti mstaafu wa ACT- Wazalendo) na Othman Masoud Othman ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa chama hicho.
“Tukio hili la pamoja linaainisha dhima ya pande hizi kufanya kazi pamoja ili kupata ufumbuzi wa kuduma na endelevu wa changamoto zinazoikabili Zanzibar, kisiasa, kijamii na uendeshaji wa shughuli za umma,” amesema.
Akisoma tamko hilo, Mansura amesema pande mbili hizo zimekubaliana mazingira ya Zanzibar yanahitaji ushirikiano utajaojenga umoja, mshikamano na maridhiano ya dhati yenye amani na utulivu endelevu wa kuunda kamati ya pamoja ya majadiliano kwa mujibu wa ratiba iliyokubaliwa.
“Pande zote mbili zinakubaliana kuchukua hatua stahiki za kuendelea imani kwa wananchi na wadau wa uchumi, biashara na uwekezaji Zanzibar,” amesema.
“Pia, kutambua viongozi wa kisiasa wana dhamira ya dhati ya kujenga mfumo na taasisi zitakazoimarisha demokrasia, utawala bora, uwajibikaji na utawala wa sheria, ambapo uendeshaji wa chaguzi huru na haki, na utoaji wa haki kwa ufanisi utakuwa kielelezo cha kufanikisha dhamira hiyo,” amesema.
Mansura amesema pande hizo mbili zimekubaliana mchakato huo kuwa shirikishi kwa kadri itakavyohitajika na wananchi, asasi za kiraia na makundi mbalimbali yatashirikishwa.
“Mchakato huu utaongozwa kanuni ya ukweli, dhamira ya dhati, uadilifu na masilahi ya Zanzibar ndio yatakayotangulizwa si vyama, kikundi au binafsi,” amesema.
Amesema tamko hilo la pamoja limeambatana na ajenda zilizokubaliwa kwa kuwekwa saini za pamoja na zitajadiliwa katika kamati itakayoshauri kuhusu mfumo, taratibu na utekelezaji wa makubaliano yatayofikiwa hatua kwa hatua.
“Katika kufanikisha hili chombo maalumu kitaundwa ili kuratibu utekelezaji wa mambo hayo. Utekelezaji utaanza mara baada ya kutolewa kwa tamko hili la pamoja,” amesema Mansura.
Othman
Akizungumzia hatua hiyo, Othman amemshukuru Dk Mwinyi kwa kutamka kwa cheo chake, huku akieleza uwepo wa Rais Samia ni kauli nzito ya kiuongozi na alama muhimu wa hekima na kielelezo cha namna alivyobariki mchakato huo.
Othman amesema baadhi ya maeneo yatakayokwenda kufanyiwa kazi ni mfumo wa uendeshaji wa uchaguzi, utumishi wa umma, mfumo wa utoaji haki na Serikali za mitaa, akieleza hatua zilizochukuliwa zinaweza kutafsiriwa ni kupata ufumbuzi wa kisiasa tu kwa faida ya vyama hasa katika chaguzi.
“Huo ni mtizamo mfupi, mtazamo sahihi ni kuwa Zanzibar inahitaji zaidi hatua zilizoainishwa kwa manufaa mapana na ya muda mrefu ya kijamii na kiuchumi,” amesema Othman.
Amesema nchi zote zilizopiga hatua za maendeleo hasa za visiwa zimetanguliza hazina kuu tano ambazo ni utengamano wa kijamii,
Serikali yenye uadilifu, uwazi na inayoongozwa na utawala wa sheria, uwajibikaji, utulivu wa kisiasa, amani na utulivu.
“Zanzibar ni nchi ya uchumi wa huduma na biashara, ina ndoto ya kuwa kituo kikuu cha biashara, huduma na usafirishaji. Hatua zinazokusudiwa kuchukuliwa sio tu za manufaa ya kisiasa bali masilahi mapana ya kijamii, kiuchumi na kiutawala.
“Ni juhudi za kuijenga na kuipeleka mbele Zanzibar ili kutimiza ndoto zake,” amesema Othman ambaye amewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Othman amesema hatua ya kutoa tamko ni jitihada nzuri katika kutafuta ufumbuzi lakini kuna mgawanyiko wa makundi matatu, wapo viongozi na wananchi wengi waliofurahi na kuomba dua jambo hilo lifanikiwe.
Lakini amesema wapo na wale waliokata tamaa wakiwa hawana imani na mchakato huku wakisema ni yale yale hakuna litakalofanikiwa.
“Kundi la tatu ni wale wasiokubali mchakato huu na wapo tayari kupambana nao ili lolote lisifanikiwe. Hawa hawapingi tu mchakato huu bali wanapinga hata Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Hawa wanaamini haya ni makaratasi, hii ni njia tu ya funika kombe lakini mambo yataendelea kama kawaida. Hawa ni wachache sana wenye masilahi binafsi na sio ya nchi wala wananchi, lakini baadhi wana nyadhifa, wana mamlaka na wana ushawishi mkubwa,” amesema.
Hata hivyo, Othman amewataka Wazanzibari kuungana kuipa fursa Zanzibar kufikia pale inapostahiki akisema yote yanakusudiwa kufikiwa katika mchakato huo, sio kwa masilahi ya vyama wala watu binafsi bali kwa nchi na vizazi vijavyo.
Ahadi za ACT- Wazalendo
Katika hotuba yake, Othman amesema chama hicho kinatoa ahadi tatu ikiwamo ACT- Wazalendo kuingia katika mchakato ikiwa na dhamira njema kwa nia ya kutekeleza yatakayoafikiwa.
“Tunafahamu bado safari iliyopo mbele yetu bado ni kubwa sana na ngumu, lakini tumejidhatiti kwenda ili kutafuta ndoto ya watu wa nchi hii ya amani na utulivu,” amesema.
“Chama chetu kinawaahidi Wazanzibari, kutanguliza mbele masilahi yao, kamwe hatutatanguliza masilahi ya chama chetu wala masilahi binafsi.”
Mbali na hilo, Othman ameahidi chama hicho kuyasimamia yote sambamba na kuwafikia wananchi wote wa Zanzibar bila kujali itikadi zao kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa mchakato huo.
Dk Mwinyi
Katika hotuba yake, Dk Mwinyi amesema hatua hiyo inadhihirisha nia ya pamoja ya kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kupata ufumbuzi wa kudumu na endelevu wa changamoto zinaziokabili Zanzibar kisiasa.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa Wazanzibari na Watanzania kwa pamoja ili kuleta umoja, mshikamano, maridhiano ya kitaifa yenye lengo la kuleta kufanikisha jitihada za maendeleo na uchumi.
“Ni dhahiri hatua hii tuliyofikia leo ni muhimu ya kufungua njia katika kufikia utekelezaji wa matakwa ya Kikatiba ya kuwezesha uundwaji wa SUK kwa mujibu wa vifungu vya tisa kifungu kidogo cha tatu na 39 vya katiba ya Zanzibar ya mwka 1984,” amesema.
Dk Mwinyi amesema hatua hiyo ni muhimu kwake akiwa kiongozi wa nchi katika utekelezaji wa azma yake ya kuimarisha umoja, mshikamano na wananchi wa Zanzibar ili kwa pamoja kushirikiana kuleta maendeleo ya Taifa.
Amewahakikishia Wazanzibari kuwa yupo tayari kushirikiana na viongozi wenzake kusimamia hatua ya pili ya mchakato, akiamini itaongozwa na dhamira ya dhati ya kupata mwafaka na masilahi ya Zanzibar yawekwe mbele.
Amesema hatua ya mwafaka baada ya utiaji saini, itazidi kuimarisha imani za wananchi na wadau mbalimbali wakiwamo wawekezaji, wafanyabiashara na washirika wa maendeleo katika kuendelea kushirikiana na Zanzibar.
“Natoa wito, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kuunga mkono dhamira hiyo njema ya kuleta maelewano kwa ajili ya maendeleo,” amesema Dk Mwinyi.
Maoni kuhusu tamko
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Masoud Hamad amesema wamefurahishwa na hatua hiyo kwa Zanzibar, akisema kumekuwapo na sintofahamu zinazosababisha misuguano yenye madhara.
“Haya ni makubaliano au maridhiano ya tano, tangu shughuli za vyama vya siasa kuanzishwa nchini tumechukua hatua kubwa na tumefikia pakubwa, huu utakuwa ni mwendelezo,”amesema Hamad
Katibu Mkuu wa Chama cha The United People's Democratic Party ((UPDP), Hamad Mohmed Ibrahim amesema viongozi hao wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa Serikali na vyama hivyo kuhakikisha jambo hilo linapata mafanikio.
“Jambo kubwa ambalo Wazanzibari wanalihitaji ni maendeleo na sio migogoro na wanataka kuona jitihada zinazofanywa zinafikia hatua ya kufanikiwa,” amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Africa Farmers Party (AAFP), Soud Said Soud amesema jambo hilo linatakiwa kuungwa mkono na kila mmoja kutekeleza yale ambayo wanakubaliana ili kuondosha sintofahamu za mara kwa mara.
Askofu wa makanisa ya AGT, Dickson Kaganga amesema kwa nyakati tofauti wamekuwa wakishauri jambo hilo ili kuondoa mkwamo wa kisiasa visiwani humo, hivyo anashukuru kuona limetekelezeka.
Imeandikwa na Bakari Kiango, Jesse Mikofu na Aurea Simtowe, Zanzibar.