Ujumbe wa Rais Samia, Mpango kwa Kardinali mteule Rugambwa

Askofu Mkuu Mwandamizi Jimbo Kuu la Tabora, Protase Rugambwa
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Makamu wake, Dk Philip Mpango wamempongeza Askofu Mkuu Mwandamizi Jimbo Kuu la Tabora, Protase Rugambwa kwa kuteuliwa kuwa kardinali.
Rugambwa ameteuliwa katika wadhifa huo leo Jumapili Julai 9, 2023 na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francisco.
Viongozi hao wakuu, wametumia akaunti zao za kijamii za Twitter na Instagram kumpongeza Rugambwa kwa kuweka picha yake na ujumbe wao.
Rais Samia ameandika, “nakupongeza Askofu Mkuu Protase Rugambwa kwa kuteuliwa na Baba Mtakatifu Fransisko kuwa Kardinali. Naungana na Watanzania wote kukutakia kheri na kukusindikiza katika sala, unapoendelea na kazi yako ya utume katika hatua hii mpya.
“Mwenyezi Mungu ambaye amekuinua kwa baraka na jukumu hili kwenye wito wako, aendelee kukuongoza katika kulitumikia Kanisa na jamii yetu kwa ujumla,” amemalizia.
Kwa upande wake, Dk Mpango ameandika, “Mhashamu Baba Askofu Mkuu Mwandamizi Protase Rugambwa: Nimepokea kwa furaha kubwa kuteuliwa kwako na Baba Mtakatifu Fransisco, kuwa Kardinali wa tatu katika nchi yetu ya Tanzania.”
“Uteuzi huu unathibitishwa na maneno kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (8:28) kwamba: Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.” HONGERA SANA.”
Rugambwa mwenye miaka 63, anakuwa kardinali wa tatu nchini akitanguliwa na Laurean Rugambwa aliyefariki dunia Desemba 8, 1997 na Polycarp Pengo aliyestaafu mwaka 2019.
Papa amemteua Rugambwa kuwa kardinali ikiwa ni takribani miezi mitatu tangu alipomteua Aprili 13, 2023 kuwa askofu mkuu mwandamizi mrithi wa Jimbo Kuu la Tabora akichukua nafasi ya Askofu Mkuu Paulo Ruzoka aliyestaafu.
Rugambwa ameteuliwa miongoni mwa makardinali 21 walioteuliwa leo Jumapili na Papa na watasimikwa Septemba 30, 2023, Vatican nchini Italia.