Ugomvi wa kuku, wampeleka jela miaka minne

Muktasari:
- Hamisi Jumanne (21) alikuwa anakabiliwa na shitaka moja la kuua bila kukusudia, ambapo alimchoma kisu Alfred Raymond kutoka na mgogoro wa kuku.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemuhukumu Hamisi Jumanne (21) kutumikia kifungo cha miaka minne gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila kukusudia.
Jumanne ambaye ni mchunga mifugo na mkulima wa mbogamboga, alimuua Alfred Raymond, maarufu Mandela kwa kumchoma visu sehemu mbalimbali za mwili wake kutokana na kutokea ugomvi wa kuku baina ya wawili hao.
Ilielezwa kuwa ugomvi huo unatokana na mshtakiwa kuiba kuku watatu wa bosi wake ambao alikuwa anataka kwenda kuwauza, na alipohojiwa na Raymond anawapeleka wapi kuku hao ndipo alipoingia ndani ya nyumba na kutoka na kisu ambacho alianza kumchoma Raymond sehemu ya shingo, tumbo na kwenye mapafu.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Februari 28, 2025 na Jaji Hamidu Mwanga, baada ya mshtakiwa kukiri mwenyewe shitaka la kuua bila kukusudiwa.
Awali, mshtakiwa huyu alikuwa anakabiliwa na shitaka la kuua kwa kukusudia, lakini leo kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ndipo mshtakiwa alipokiri shitaka la kuua bila kukusudiwa na upande wa mashitaka kumbadilisha hati ya mashitaka kwa kuondoa ile ya kuua kwa kukusudia na kuwa mauaji ya bila kukusudia.
Mshtakiwa huyo alishtakiwa chini ya kifungu 196 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Mshtakiwa huyo alisema kuwa amepitia hati yake ya mashitaka na maelezo yake anaomba kukiri shitaka la kuua bila kukusudia na kama hakuna pingamizi lolote kutoka upande wa mashitaka, anaomba kuwasilisha.
Hata hivyo, upande wa mashitaka ukiongozwa na Said Seif, ulieleza kuwa hauna pingamizi juu ya ombi hilo na hivyo kumbadilishia hati ya mashitaka na kisha kumsomea.
Akimsomea shitaka hilo, wakili Seif alidai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na shitaka la kuua bila kukusudia chini ya kifungo cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Alisema kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 4, 2022 eneo la Makurunge, Wilaya ya Kisarawe.
Ilielezwa kuwa siku hiyohiyo, mshtakiwa alisababisha kifo cha Alfred Raymond kwa kumchoma visu mwili wake baada ya kutokea kwa ugomvi baina yake na Raymond.
Maelezo yake
Akisomewa maelezo ya mshtakiwa, wakili Seif alisema kuwa Hamisi na Raymond walikuwa wanafahamiana na wote waliajiriwa na Fredrick kufanya kazi ya kuchunga mifugo shambani kwake, eneo la Makurunge, Wilaya ya Kisarawe.
Ilielezwa Agosti 4, 2023 jioni, mshtakiwa alikuwa shambani akichunga na akiwa eneo hilo aliiba kuku watatu waliokuwepo eneo hilo kwa lengo la kwenda kuuza.
" Wakati akiwa katika harakati ya kwenda kuuza kuku hao, alikutana na Raymond aliyemuuliza kuku hao anawapeleka wapi? Na wakati huo alikuwa ameshika simu mkononi hivyo alimpigia bosi wao na kumueleza kuwa Hamis ameiba kuku" alisema wakili Seif
Alisema kutokana na hali hiyo, kulitokea ugomvi ambapo mshtakiwa alikimbia ndani na kutoka na kisu ambacho alianza kumchoma Raymond sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha aanguke chini huku akipiga kelele za kuomba msaada.
"Watu walifika eneo la tukio na kumchukua Raymond na kumpeleka hospitali ya Kisarawe, huku mshtakiwa akipelekwa Hospitali ya Mloganzila kwa ajili ya matibabu kutokana naye kujeruhiwa" alisema wakili Seif.
Agosti 7, 2023 uchunguzi wa mwili wa Raymond ulifanyika ulionyesha kuwa kifo chake kimetokana na kuvuja kwa damu nyingi kutoka na majeraha yaliyosababishwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kwenye moyo, mapafu utumbo na shingoni.
Agosti 9, 2023 mshtakiwa alikamatwa akiwa hospitali akiendelea na matibabu na kuhojiwa polisi.
Akitoa hukumu, Jaji Mwanga alisema Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyo chini ya kifungu 195 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Hata hivyo, kabla ya kutoa uamuzi, Jaji Mwanga alimpa nafasi mshtakiwa ya kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali.
Mshtakiwa aliomba apunguziwe adhabu kutokana na umri wake kuwa mdogo na pia amekaa gerezani mwaka mmoja na miezi sita.
Pia mshtakiwa huyo alisema kuwa hata yeye alijeruhiwa na Raymond sehemu ya mgongoni na shingoni.
Kwa upande wa mashitaka ulieleza kuwa hauna kumbukumbu za nyuma za makosa ya jinai, na kwa mujibu wa kifungu alichoshtakiwa nacho mshtakiwa adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano, hivyo wanaomba Mahakama ilitoa adhabu kwa mujibu wa sheria.
Akitoa adhabu hiyo, Jaji Mwanga alisema "Baada ya kupitia shufaa zilizotolewa na mshtakiwa pamoja na upande wa mashitaka na nimezingatia muda aliokaa gerezani mshtakiwa, hivyo Mahakama hii inakuhukumu kutumikia kifungo cha miaka minne gerezani ili iwe fundisho."