Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uchumi shirikishi unavyoweza kujenga au kubomoa familia

Muktasari:

Wiki iliyopita Mahakama ya Mwanzo jijini Mbeya ilipata kesi ya aina yake baada ya wanandoa, wote wakiwa watumishi wa Serikali kufungua madai ya talaka huku kila mmoja akiamini hilo ndilo suluhisho katika tatizo linalowakabili.

Wiki iliyopita Mahakama ya Mwanzo jijini Mbeya ilipata kesi ya aina yake baada ya wanandoa, wote wakiwa watumishi wa Serikali kufungua madai ya talaka huku kila mmoja akiamini hilo ndilo suluhisho katika tatizo linalowakabili.

Katika shauri hilo la madai ya talaka, mke ambaye ni mwalimu anamlalamikia mumewe, askari magereza kwa kile anachodai anataka kumnyanyasa kiuchumi kwa kumnyang’anya kipato anachopata kutokana na kazi yake na kukiingiza kwenye matumizi ya familia.

Mwanamke anadai mumewe anataka kadi yake ya benki ili mshahara utakapoingia fedha azichukue yeye na kuzipangia matumizi, jambo ambalo hakubaliani nalo na analichukulia kama ukatili wa kiuchumi.

Kwa upande wa mume, analalamika licha ya mkewe kuwa na ajira ya kudumu inayomuingizia kipato, hana mchango wowote kwenye familia, pesa zake zote anapeleka kanisani, hali inayomfanya majukumu yote kuyabeba yeye, ikiwamo kuhudumia familia, ada za watoto na mambo mengine mengi.

Kuna mengi yameelezwa kwenye sakata hilo, lakini kwa kuwa shauri lipo mahakamani tutaliacha kama lilivyo ili sheria iamue hatima ya wanandoa hao ambao wote wako tayari kuvunja ndoa ili kila mmoja aendelee na maisha yake.

Kilichotokea kwenye familia hii kinaweza kuwa mfano wa matatizo ya familia nyingi hapa nchini, hasa zinazohusisha wanandoa ambao wote wana shughuli za kujiingizia kipato na mama analazimika kuwa sehemu ya kubeba majukumu ya familia.


Wanachosema wanafamilia?

Akizungumzia hilo ushirikiano wa kiuchumi katika familia, Faraja Lubava ambaye ni mke na mfanyabiashara ndogondogo anasema pamoja na mume wake kubeba majukumu makubwa ya familia na yeye anashiriki katika kufanikisha hakuna kinachokwama kwa sababu ya fedha.

“Sio kwamba nina fedha nyingi hapana, tunachofanya mume wangu anafanya majukumu yote makubwa mfano ada za watoto, matumizi ya nyumbani sasa inapotokea kuna kitu kimepungua au ndio mimi nanyoosha mkono wangu kuhakikisha tunakwenda sawa.

“Inaweza ikatokea amelipa ada lakini hapo katikati mtoto akahitaji kitu cha shuleni na baba yake hayupo vizuri kifedha ninachokua jukumu hilo kama mama kwa kifupi tunashirikiana,” anasema Faraja.

Kwa upande wake Noel Massawe anasema yeye hashughuliki na fedha ya mkewe anachofanya ni kutekeleza wajibu.

“Mimi ni kichwa kwenye familia lazima niwe baba hivyo basi nafanya vitu vyote vinavyohusu familia kulingana na kipato changu. Mahitaji yote ya muhimu lazima niyatimize. Ni kweli anafanya kazi lakini hela yake ni yake akiamua kuitumia kwa ajili ya familia ni sawa ila simlazimishi kufanya hivyo.”


Washauri wanasemaje?

Mshauri wa uhusiano, Deogratius Sukambi anasema kumekuwa na mjadala mgumu sana kuhusu suala la kipato ndani ya familia kutokana na wanawake wengi wa kileo kubeba majukumu ambayo si yao.

Pia, anasema wapo wanaume wanaoacha kwa makusudi majukumu yao wakiamini wake zao watafanya.

Sukambi anasema kwa sasa kumekuwa na wimbi la wanawake kubeba majukumu ya familia na watoto wao wanakua wakiona hivyo ndiyo inapaswa kuwa.

Pia, anasema kuna wanaume wanaoa wakiamini wake zao watawasaidia kubeba majukumu.

Hali hiyo anasema imewafanya wanaume wengi kukumbatia dhana ya ushiriki wa mke katika kufanya majukumu ya kifedha ndani ya familia na kutumia mwanya huo kuacha kubeba majukumu yao.

“Tunapozungumzia uchumi shirikishi kwa sasa wanawake wamevuka mpaka, kwa sababu hiyo wameachiwa majukumu ya kutunza na kuhudumia familia. Unapotengeneza usawa kwenye kutekeleza majukumu ya familia na mwanamke akafanya, basi mwanamume anaona anaweza kumuachia, hasa ikitokea amefanya bila ridhaa ya mume,” anasema Sukambi.

“Ifahamike kuwa, taasisi ya ndoa kiongozi wake ni mwanamume na kutokana na uongozi huo, basi anatakiwa kubeba majukumu yote ya familia kuanzia mwanzo hadi mwisho, mwanamke ataingia kama msaidizi, hivyo atafanya pale atakapoelekezwa kufanya,” anasema Sukambi.

Pamoja na uhalisia kuwa hivyo, kinachotokea kwa wanawake wengi ni kuzifuata hisia zao na kuamua kubeba majukumu ya mume kwa kile wanachoamini wananusuru mambo yasiharibike, matokeo yake wanaachiwa mzigo.

“Kutokana na kutawaliwa na hisia, utakuta mwanamke anaona mtoto hajalipiwa ada anakimbia kulipa, chakula hakipo nyumbani ananunua chakula tena bila kupata ridhaa ya mwenza wake, hapa ndipo tatizo linapoanzia, kwani mwanamume anaona ooh kumbe anaweza.

“Tunapozungumzia dhana ya uchumi shirikishi, mwanamume ndiye kiongozi, anatakiwa afanye majukumu yake, mwanamke kazi yake ni kumsaidia. Kama mwanamume hafanyi anavyotakiwa kufanya jukumu la mwanamke sio yeye kuyafanya, bali kumsaidia jinsi ya kufanya majukumu hayo,” anasema Sukambi.

Pia, anasema mwanamke anatakiwa kumuhamasisha mwanamume jinsi ya kufanya hayo majukumu na ikitokea ameshindwa atatoa maelekezo ya kumsaidia, lakini siyo kufanya bila kupata ridhaa yake.

Sukambi anasema yapo pia makosa yanayofanywa na wanaume, hasa wa kisasa wanaoingia kwenye ndoa na wanawake wenye shughuli za kujiingizia kipato, wakiamini watakuwa na msaada kwenye maisha yao.

“Kuna hili tatizo limeanza kuota mizizi, yaani mwanamume anaoa mwanamke mwenye uwezo akiamini atakuwa msaada kwake, ni kosa kubwa, majukumu yote ndani ya nyumba yanapaswa kubebwa na mwanamume, mke anabaki kuwa msaidizi.

“Ili akusaidie unapaswa kumshawishi kwa nini akusaidie, umpe sababu za kukusaidia na hutakiwi kumpa masharti kwa pesa anazotafuta mwenyewe, pesa hizo ni zake sio za kwako,” anasema Sukambi.

Mwanasaikolojia Lilian Malya anasema kwa asili wanaume huwa hawafanyi majukumu kwa kushirikiana, wanaamini katika kila mtu kufanya jukumu lake, hii iko tofauti na wanawake, wao wanafurahia kushirikiana kufanya majukumu.

“Kwa wanaume dhana ya ushirikiano sio halisi, ni aidha jukumu afanye yeye au afanye mkewe basi. Hivyo mnapoleta pesa pamoja kwa ajili ya matumizi ya familia uwezekano wa mwanamume kuziweka zake pembeni akazifanyie majukumu mengine ni mkubwa. Ingawa wapo ambao wanaweza kushiriki kikamilifu.”


Nini kifanyike

Sukambi anasema kitu cha muhimu kwa sasa ni wanawake kutambua nafasi yao na kurudi nyuma kuwapisha wanaume kuchukua nafasi zao kwenye nyumba na familia kwa jumla.

“Wanawake wanapaswa kurudi nyuma na kutambua wazi mzigo waliobeba sio wao, kisha wakae kuzungumza na kukubaliana atafanya nini katika nafasi yake ya usaidizi, lakini sio mume amelala, hela yake yote anaipeleka sehemu nyingine halafu majukumu yabebwe na mama,” anasema Sukambi.

“Kinachowaponza wanawake wengi ni hizi hisia kwamba mtoto wangu lazima avae vizuri au asome shule nzuri wakati anatambua fika mwenza wake hana uwezo wa kumudu, kwa namna yoyote ukilazimisha lazima atakuachia. Kubali kuishi kulingana na uwezo alionao mwenza wako.”