TFNC, WFP waanzisha mradi wa majaribio kupambana na udumavu mashuleni
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk Esther Nkuba akitoa elimu ya lishe kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule ya msingi Kibasila manispaa ya Temeke ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Afya na Lishe unaotekelezwa katika shule za msingi 15 za Manispaa ya Temeke.
Muktasari:
- Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani. (WFP) wanatoa elimu ya lishe katika shule za Temeke kuboresha afya ya wanafunzi, kuzuia udumavu, kuhamasisha michango ya lishe, bustani za shule na maandalizi ya mlo kamili bora.
Dar es Salaam. Katika kukabiliana na changamoto za lishe kwa wanafunzi wa shule za msingi nchini, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani (WFP) wameanza kutoa elimu ya lishe kwa wanafunzi, wazazi na walimu katika shule za msingi namna ya kuandaa mlo kamili.
Elimu hiyo inatolewa kupitia mradi wa majaribio wa Afya na Lishe unaotekelezwa katika shule 15 za Manispaa ya Temeke kwa ushirikiano kati ya TFNC na WFP.
Mradi huo wa mwaka mmoja unalenga kuhamasisha utekelezaji wa mpango wa lishe mashuleni, kubadili tabia, kupika vyakula visafi na salama, pamoja na kuhamasisha uanzishwaji wa bustani za shule unategemewa kuwanufaisha wanafunzi takribani 29,000 wakati wa utekeelzaji wake.
Akizungumza leo Novemba 18,2025 jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara ya kutoa elimu katika shule tatu za msingi za Temeke, yaani Kibasila, Ububini na Lioness Miburani Ofisa Lishe Mtafiti kutoka TFNC, Eliasaph Kurwijila, ameeleza namna tatizo la lishe linavyowaathiri watoto kutokana na kutopata mlo kamili.
Amesema. kwa mujibu wa utafiti uliofanyika nchini mwaka 2019, kati ya watoto watatu wa shule ya msingi, mmoja huondoka nyumbani asubuhi bila kula chakua chochote.
“Mtoto ili ubongo ufanye kazi vizuri ni lazima apate chakula chenye virutubisho, hivyo ni muhimu mzazi kumpatia mtoto kifungua kinywa kabla hajaondoka nyumbani kuelekea shuleni,” amesema.
Amebainisha kuwa, shule nyingi hutoa chakula kwa wanafunzi wa madarasa ya mitihani pekee au wakati wa shughuli maalumu.
“Mtoto katika ukuaji wake anapaswa kupata vyakula kutoka katika makundi sita ambayo ni nafaka, mizizi yenye wanga na ndizi mbichi (zinazoliwa baada ya kupikwa), mbogamboga, matunda, vyakula jamii ya mikunde, karanga na mbegu zenye mafuta, vyakula vya asili ya wanyama na mafuta. Hivyo wazazi ni muhimu kuchangia lishe mashuleni,” amesema Kurwijila.
Amesema Tanzania inakabiliwa na tatizo la lishe kwa watoto, ambapo ni asilimia 56 pekee ya watoto wote nchini wanaopata chakula shuleni.
Mtaalamu huyo ametaja matatizo yatokanayo na lishe yanayowakumba wanafunzi kuwa ni udumavu, uzito kupita kiasi, uzito mdogo, upungufu wa damu na upungufu wa madini chuma.
“Karibu asilimia 25 ya wanafunzi wa shule za msingi wamedumaa, asilimia 11 wana ukondefu, asilimia 33 wana upungufu wa damu na asilimia nne wana uzito kupita kiasi,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe wa TFNC, Dk Esther Nkuba, amewahimiza wazazi kuhakikisha wanawapa watoto wao elimu kuhusu aina ya chakula wanachopaswa kula na kuwaepusha na vyakula vyenye sukari nyingi.
Amesema tabia hiyo inaweza kudhibitiwa na wazazi kwa kuwaelekeza watoto aina ya vyakula vinavyofaa, pamoja na kushirikiana na walimu katika kutoa michango ya lishe.
Dk Nkuba amesema mradi huo wa lishe unatekelezwa kwa mwaka mmoja na baadaye utaongezwa muda hadi miaka mitatu baada ya majaribio kukamilika.
Shule zinazofaidika na mradi huu unaolenga kuboresha mazingira ya usafi kwenye maeneo ya chakula mashuleni na kuhamasisha lishe ni: Ububini, Lioness Miburani ya Temeke, Likwati ya Miburani, Madenge ya Temeke, Charambe, Chemchem, Nzasa zote za Kilungule,
Pia ipo Kilamba ya Charambe, Marten Lumbanga ya Kilungule, Amani ya Buza, Bokorani ya Mtoni, Ally Hassan Mwinyi ya Tandika, Mabatini ya Tandika, Umoja ya Temeke na Kibasila ya Miburani.
Hilary Hassan, mzazi wa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kibasila, amesema ni vyema wazazi kuchangia fedha za lishe kwa wanafunzi ili kuwawezesha kusoma bila maradhi.
“Mtoto akila na kushiba kabla ya kutoka nyumbani na akapata chakula shuleni, humwezesha kusoma kwa utulivu,” amesema.