Teknolojia ya kidijitali inavyobadili samani za ndani
Muktasari:
- Wataalamu wa usalama na mafundi wa samani wanasema mvuto wa samani za kisasa unaambatana na changamoto zinazohitaji kuangaliwa kwa umakini.
Dar es Salaam. Mabadiliko ya mitazamo na mitindo ya matumizi ya samani nchini Tanzania yamesababisha kuongezeka kwa bidhaa zenye nakshi na mapambo ya kisasa.
Miongoni mwa vipengele vinavyoongeza mvuto huu ni matumizi ya taa za LED ambazo hutumia nishati ndogo kuliko balbu za kawaida, pamoja na mifumo ya kusokota au kuzunguka (rotating systems) na vifaa vingine vinavyotumia umeme.
Ingawa samani hizi huongeza mwonekano wa kuvutia na kuipa nyumba taswira ya kisasa, wataalamu wa usalama pamoja na mafundi wa samani wanatahadharisha kuwa mvuto huo wa kisanii, unakuja sambamba na changamoto kadhaa zinazohitaji kuzingatiwa kwa umakini.
Ilivyo sasa, samani zenye mwanga wa LED, viti vinavyojikunja kwa umeme, meza zenye sehemu za kuchaji simu na vitanda vinavyohamishika zimekuwa kivutio kwa watumiaji wa mijini. Kwa wateja, samani hizo zenye nakshi na teknolojia zinaonyesha hadhi na zinaendana na maisha ya kisasa.
Pamoja na mvuto huo, wataalamu wanaonya juu ya athari zinazoandamana na matumizi ya vifaa vya umeme kwenye samani, zikiwamo za hatari za kiusalama.
Hilo linatokana na mchanganyiko wa utengenezaji samani hizo unaojumuisha mbao, sponji na mifumo ya umeme.
Wadau wanapendekeza wazalishaji wa ndani kuwekeza katika ubunifu salama unaozingatia viwango vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na watumiaji kuangalia ubora wa miunganisho ya umeme kabla ya kununua.
Umakini muhimu
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi amesema ukuaji wa teknolojia ni mzuri, lakini unahitaji umakini wa hali ya juu kwa watumiaji na wazalishaji wa samani hizo.
“Jambo la msingi ninaloliona ni namna ya kuwa makini kwenye matumizi ya soketi zinazowekwa kwenye samani. Mtu anaweza kuweka sehemu ya kuchajia simu na kuondoka akiacha soketi inafanya kazi,” amesema.
Amesema changamoto inayoonekana kwenye maeneo mengi ya uzalishaji samani na majumbani ni ufahamu mdogo wa hatari za umeme.
Kwa mujibu wa Mabusi, kwenye samani hizo vipo vifaa vinavyoshika moto kwa haraka kama vile mbao na magodoro.
Amesema hitilafu inapojitokeza, kama vile waya kugusana, kifaa kuungua ndani, panya kutafuna nyaya au watoto kumwaga maji mtumiaji hawezi kugundua chochote kwa kuwa kila kitu kimefichika.
Mabusi amesema moto unaweza kuanza taratibu kwa kuongeza joto ndani ya sofa au kitanda bila kutambuliwa na hatimaye ukasambaa.
Amesema aina hii ya hitilafu ni hatari zaidi kuliko moto wa soketi ya ukutani kwa sababu chanzo chake hakionekani na mara nyingi hugundulika baada ya madhara kuwa makubwa.
Hatari nyingine, amesema inatokana na mafundi kutumia vifaa vya umeme visivyo na viwango, huku wanaotengeneza baadhi hawana utaalamu wa masuala ya umeme.
Kwa upande wake, Fredrick Mwakaluko, mkaguzi wa umeme anabainisha kuwa matukio ya samani kuungua pasipo watu kujua chanzo, yanaongezeka kutokana na watu kushindwa kutambua uwepo wa umeme ndani ya sofa au vitanda hivyo.
“Tumeshapokea kesi za waya kuyeyuka ndani ya sofa kwa sababu watu hawaoni kama vina umeme. Tatizo si sofa lenyewe, bali ubora wa mfumo wa umeme ulio ndani. Hivyo ni muhimu samani hizi ziwe na vyeti vya uthibitisho wa ubora, vinginevyo ni mabomu yanayosubiri kulipuka,” amesema.
Amesema soketi hutengenezwa bila kuwapo kifaa kinacholinda nyaya, vifaa na mifumo ya umeme dhidi ya mzigo mkubwa kupita uwezo wake wa kubeba.
Vilevile, nyingine huwa na ubora wa kiwango cha chini, hivyo kusababisha kuwaka moto haraka zinapopata joto.
Pia anaeleza nyingine huwa na plastiki laini ambayo huyeyuka kirahisi inapopokea mzigo mkubwa wa umeme.
Amesema tatizo la kuchaji vifaa bila kuzima kwa saa nyingi, limekuwa chanzo kingine cha moto, akieleza watu hutumia samani hizo wakiwa wamelala, wakitazama televisheni au wakiwa nje ya chumba.
“Simu inapojazwa chaji lakini ikaendelea kubaki imechomekwa, chaja huendelea kupasha moto, hasa zile za bei zisizo na kiwango. Moto huo unapokutana na mbao au vitambaa visivyoweza kutawanya joto vizuri, hatari ya kuungua huongezeka maradufu,” amesema.
Kilio cha gharama
Athuman Juma, fundi anayetengeneza sofa na vitanda vya umeme eneo la Mabibo, mkoani Dar es Salaam, amesema mara nyingi hawatumii mafundi maalumu wa umeme wanapotengeneza samani hizo, badala yake wao wenyewe huunganisha nyaya.
“Mara nyingi hatutafuti mafundi wa umeme kwa sababu ya gharama, hivyo tunakwenda dukani kununua vifaa zikiwamo nyaya, swichi moja au mbili kisha tunaunganisha,” amesema.
Amesema changamoto kubwa ni wateja kutaka bei ya chini kuliko viwango halisi, jambo linalowalazimu wao kutumia vifaa vya umeme vya viwango vya chini.
“Mtu anakwambia nipunguzie bei, kutoka Sh900,000 hadi Sh500,000 kwa hali hii, lazima utanunua waya na vifaa vingine vya uwezo mdogo. Lakini baadaye anakuja kuchomeka kifaa cha kusaga au chaja yenye uwezo mkubwa. Hapo ndipo shoti inatokea,” amesema.
Fundi huyo amesema baadhi ya wateja hutaka kutengenezewa sehemu za kupitishia umeme wakieleza kuwa wana mafundi wao wa kufanya kazi hiyo.
Mtaalamu wa umeme, Ismail Mohamed amesema tatizo kubwa watu wengi wanafanya kazi za umeme bila kupita kwenye mafunzo yoyote rasmi.
“Wengi wao wanafanya wenyewe kwa kuhofia gharama, hivyo wakati mwingine wanachukua mtu mwenye uelewa kidogo wa masuala ya umeme na kumpa kazi ya kuunganisha nyaya bila kufikiria madhara ya baadaye,” amesema.
Amesema ameshakutana na kesi kadhaa za kuitwa kwenye nyumba za watu kurekebisha sofa na vitanda baada ya kuungua.
Katika marekebisho anayofanya, alisema amebaini baadhi ya nyaya zinazotumika ni za milimita 0.5 ambazo hutumika kwenye spika, wakati zinazohitajika za milimita mbili.
Mtaalamu huyo amesema ni ngumu kutambua inapotokea tatizo kwa sababu kunakuwa kumefunikwa, hivyo ni rahisi sofa na vitanda kuungua.
Debora Shelukindo, mkazi wa Kawe amesema awali alikuwa akizima swichi kwenye sofa au kitanda pekee na kuacha ikiwaka ukutani.
Amesema kwa sasa anachukua tahadhari kwa kuhakikisha anazima kila mahali baada ya matumizi baada ya shoti ya umeme kutokea.
“Watoto wangu walipofika hapa walijisahau wakalala bila kuzima ukutani, kitanda kilinusurika kuwaka kwa sababu waliwahi kuzima kwenye njia kuu ya umeme (main switch), sasa tumejifunza kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vitu vyote,” amesema.