TCU yatangaza nafasi 170,000 shahada ya kwanza, wadau wataka njia mbadala
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Profesa Charles Kihampa akizungumzia kufunguliwa kwa dirisha la udahili kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Muktasari:
- Wadau hao wamesisitiza kuwa badala ya kupima mafanikio kwa idadi ya wanaojiunga na vyuo vikuu pekee, Tanzania inapaswa kujenga mfumo unaozalisha wataalamu wa ngazi zote kulingana na mahitaji ya uchumi wa viwanda, teknolojia na huduma.
Dar es Salaam. Wakati Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ikifungua dirisha la maombi ya udahili wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2026/2027, taasisi za elimu ya juu nchini zimeweka nafasi zaidi ya 170,000 kwa waombaji wenye sifa.
Hata hivyo, wadau wa elimu wanasema ongezeko la wahitimu wanaostahili kujiunga na vyuo vikuu linapaswa kwenda sambamba na sera zitakazopanua fursa za elimu baada ya sekondari.
Wanasema mafanikio ya sekta ya elimu hayapaswi kupimwa kwa idadi ya wanaojiunga na vyuo vikuu pekee, bali kwa uwezo wa mfumo wa elimu kuzalisha wataalamu wa ngazi mbalimbali.
Kwa mujibu wa wadau hao, Tanzania inahitaji kuimarisha kwa wakati mmoja vyuo vikuu, vyuo vya kati na vya ufundi, ili kukidhi mahitaji ya uchumi wa viwanda, teknolojia na sekta ya huduma.
Dirisha hilo limefunguliwa ikiwa ni siku chache baada ya kutoka kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2026 ambapo asilimia 99.92 ya wanafunzi 133,647 watahiniwa sawa wanafunzi 133, 540 wamefaulu.
Akitoa taarifa ya kufunguliwa kwa dirisha hilo leo Julai 10 hadi Agosti 10, 2026, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amewataka waombaji kufuata taratibu zote zilizowekwa, ili kuepuka usumbufu wakati wa kutuma maombi.
"Tunawasihi waombaji kusoma kwa makini mwongozo wa udahili pamoja na maelekezo maalumu yanayotolewa na kila chuo kabla ya kuanza kutuma maombi. Mwaka huu nafasi zaidi ya 170,000 zimeendelea kuongezeka ikilinganishwa na mwaka jana zilipokuwa nafasi 150,000.
Profesa Kihampa amesema waombaji wa Kitanzania wenye vyeti vya sekondari vilivyotolewa na mabaraza ya mitihani ya nje ya nchi wanapaswa kwanza kuthibitisha ulinganifu wa vyeti hivyo, kupitia Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta).
Kwa vyeti vya stashahada amesema vihakikiwe Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet).
Wasemavyo wadau
Wakati idadi ya wanafunzi wanaojiunga vyuo vikuu inaongezeka, wadau wa elimu wana mtazamo tofauti kuhusu hali hiyo.
Mhadhiri wa masuala ya elimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk John Mkwizu amesema mafanikio hayo yanatakiwa kwenda sambamba na maandalizi ya situ kuongeza nafasi, bali pia kuboresha miundombinu ya kufundishia.
"Kadiri wanafunzi wanaofaulu wanavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya vyuo, wahadhiri, mabweni, maabara na mikopo yanavyoongezeka. Bila maandalizi hayo tunaweza kujikuta tumepanua ufaulu lakini tukashindwa kutoa fursa za kuendelea na elimu ya juu," amesema Dk Mkwizu.
Kwa upande wake, mchambuzi wa sera za elimu, Benson Mwaikinda, amesema hoja kubwa si kama vyuo vinaweza kuwachukua wote wanaodahiliwa, bali kama uchumi wa Tanzania unahitaji kila mhitimu wote wa kidato cha sita kuwa na shahada.
Amesema mataifa yenye mifumo imara ya elimu huweka uzito sawa kati ya elimu ya vyuo vikuu, vyuo vya kati na mafunzo ya ufundi kulingana na mahitaji ya uchumi.
"Taifa linahitaji pia mafundi, wabunifu wa teknolojia, wataalamu wa viwanda, kilimo, ujenzi na huduma nyingine zinazotolewa kupitia elimu ya ufundi na vyuo vya kati," amesema Mwaikinda.
Naye mtaalamu wa uchumi wa elimu, Dk William Mosha, amesema ongezeko la wahitimu linapaswa kuonekana kama fursa ya kuongeza mtaji watu, lakini mafanikio hayo yatategemea namna Serikali itakavyopanua uwezo wa taasisi za elimu ya juu.
"Hata kama mwanafunzi ana sifa za kujiunga na chuo kikuu, lazima kuwe na nafasi, uwezo wa familia kugharamia elimu au kupata mkopo, pamoja na mazingira bora ya kujifunzia. Haya yote yanaathiri idadi ya wanaoweza kujiunga kila mwaka.
Changamoto nyingine ni uwezo wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwahudumia waombaji wengi zaidi kila mwaka. Ongezeko la wahitimu linaweza kuongeza ushindani wa mikopo, jambo litakalowalazimu baadhi ya wanafunzi kuahirisha masomo au kutafuta njia nyingine za kujisomesha” amesema Dk Mosha.
Kwa upande wake mtaalamu wa maendeleo ya jamii, Dk Asha Omari, amesema ni wakati wa kubadili mtazamo wa jamii kuhusu mafanikio ya elimu.
"Mzazi asione mtoto aliyekwenda chuo cha ufundi ameshindwa maisha. Tunahitaji mfumo unaotambua vipaji na uwezo tofauti wa vijana. Wengine watafanikiwa zaidi kupitia elimu ya vitendo kuliko elimu ya nadharia ya vyuoni," amesema.
Amesema Serikali inapaswa kuendelea kuwekeza katika vyuo vya ufundi na teknolojia ili kuvifanya viwe chaguo la kwanza kwa baadhi ya wanafunzi badala ya kuwa sehemu ya mwisho kwa waliokosa nafasi vyuoni.