Tatizo la afya ya akili linavyovaliwa njuga

Muktasari:
- Benki ya Exim Tanzania imezindua Exim Bima Festival 2024 lenye kaulimbiu "Amsha Matumaini" ili kuongeza uelewa wa afya ya akili na kuchangisha fedha kwa huduma bora.
Dar es Salaam. Tatizo la afya ya akili limekuwa likiongezeka kwa kasi, huku sababu mbalimbali zikitajwa kuchangia changamoto hiyo. Kwa kutambua uzito wa suala hili, Benki ya Exim Tanzania imeanzisha tamasha maalum litakalosaidia kutatua changamoto hii.
Tamasha hilo, linalojulikana kama Exim Bima Festival 2024, lenye kaulimbiu “Amsha Matumaini”, litafanyika tarehe 28 Septemba 2024 katika viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam, likiwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 27 ya benki hiyo tangu kuanzishwa kwake. Tamasha hili linatoa fursa kwa watu binafsi, wadau, na taasisi mbalimbali kuungana kukusanya fedha kwa lengo la kusaidia kuleta mabadiliko chanya kwa wale wanaokabiliwa na matatizo ya afya ya akili.
Tamasha hili ni sehemu ya mpango wa kijamii wa Exim Cares, ambao mwaka huu unalenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa bima katika jamii na kusaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ya akili kote nchini. Benki ya Exim inalenga kukusanya Sh300 milioni katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kuboresha miundombinu na huduma katika vituo vya afya ya akili.
Stanley Kafu, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, anasema, “Tatizo la afya ya akili sio tu ugonjwa wa kimwili, bali ni suala la kijamii. Wanaoathirika ni familia zetu, marafiki zetu, na wafanyakazi wenzetu. Kupitia Exim Bima Festival 2024, tunalenga kuongeza uelewa, kuvunja unyanyapaa, na kubadilisha maisha ya Watanzania.” Kafu alisisitiza kwamba tamasha hilo litasaidia kujenga jamii yenye mwamko wa juu kuhusu afya ya akili na kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wahitaji.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Aprili 2024, ilibaini ongezeko kubwa la wagonjwa wa afya ya akili na changamoto katika utoaji wa huduma, ikiwa ni pamoja na upungufu wa vituo vya huduma nchini. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya mikoa 28, ni mikoa mitano pekee iliyo na vituo vya huduma za afya ya akili, hali inayozidisha changamoto ya utengamo kwa wagonjwa.
Ripoti hiyo pia ilibaini ongezeko la vifo na idadi ya wagonjwa wa akili nchini. Katika mwaka 2022, Hospitali ya Taifa ya Mirembe ilirekodi ongezeko la wagonjwa kutoka 3,472 mwaka 2019 hadi 5,060 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 31. Aidha, mzigo wa maradhi ya akili umesababisha ongezeko la vifo vya kujinyonga kwa kiwango cha asilimia 8.15 kwa kila watu 100,000.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk John Jingu, alieleza kuwa serikali inalifanyia kazi suala la afya ya akili kwa kuhakikisha mifumo inaimarishwa ili wagonjwa wapate huduma stahiki kwa wakati. Hata hivyo, ripoti zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2012 hadi 2021, idadi ya wagonjwa wa akili imeongezeka kutoka 386,358 hadi 2,102,726, ongezeko la asilimia 82.
Exim Bima Festival 2024 inalenga kuamsha matumaini na kuchochea hatua stahiki katika kupambana na tatizo la afya ya akili kwa Watanzania.