Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tari Kihinga na mikakati ya Taifa kujitosheleza kwa mafuta ya kula

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti Tanzania (Tari) kituo cha Kihinga Dk Filson Kagimbo (aliyechuchumaa chini) akikagua shamba la michikichi.

Muktasari:

Tanzania inahitaji tani 650, 000 ya mafuta ya kula, lakini uwezo wa ualishaji kwa mwaka ni tani 290, 000 pekee, sawa na asilimia 44.6 ya mahitaji.

Kigoma. Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) Kituo cha Kihinga mkoani Kigoma kinatekeleza mikakati maalum ya kuongeza tija kwenye kilimo cha zao la mchikichi inayotumika kuzalisha mafuta ya kula aina ya mawese ili hatimaye kuwezesha Taifa kujitsheleza kwa mahitaji.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalum, Mkurugenzi wa Tari Kituo cha Kihinga, Dk Filson Kagimbo amesema mpango hup wa miaka saba unalenga kuokoa zaidi ya Sh470 bilioni zinazotumika sasa kuagiza zaidi ya tani 360, 000 za mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

‘’Malengo yetu ni kuona Taifa haliagizi tena mafuta ya kula kutoka nje ya nchi ndani ya kipindi cha miaka saba ijayo; ili kufikia malengo hayo, kila mwaka tunatakiwa kuzalisha miche anagalau million 2 ya michikichi itakayopandwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 14 itakayowezesha kuzalisha tani 56,000 za mafuta kwa mwaka,’’ amesema Dk Kagimbo

Amesema katika kipindi hicho cha miaka miaka saba, kituo hicho kimejiwekea lengo la kuzalisha na kupanda miche ya michikichi katika eneo lenye ukubwa wa hekta 100, 000 na hivyo kuwa na uwezo wa kuzalisha tani 400, 000 za mafuta ya mawese.

“Kwa sasa, Tanzania inahitaji tani 650, 000 ya mafuta ya kula, lakini uwezo wetu ni kuzalisha tani 290, 000 pekee kwa mwaka, sawa na asilimia 44.6 ya mahitaji ya nchi,”amesema Kagimbo

Amesema kiwango hicho cha mahitaji na uzalishaji kinasababisha Taifa kuwa na upungufu wa tani 360, 000 za mafuta ya kula, sawa na asilimia 55.4 ya mahitaji yote ya tani 650, 000 ya nchi; na hivyo kulazimika kutumia zaidi ya Sh470 bilioni kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi.

Mtafiti wa Kituo cha Tari Kihinga, Basil Kavishe ametaja miongoni mwa mikakati inayotekelezwa kuwa ni kuwahimiza wakulima kungóa miche ya zamani na kupanda mipya yenye uwezo wa kuzalisha mafuta mengi zaidi.

Amesema hata wakulima wenye shamba madogo wanaweza kulima zao la mchikichi kupitia kilimo mseto kwa kuichanganya na mazao mengine jamii ya mikunde kama maharage, kunde na mimea inayotambaa jamii ya maboga .

‘’Mimea isiyotakiwa katika shamba la mchikichi ni ile yenye mizizi kama mihogo na nyanya kwa sababu inatumia kiwango kikubwa cha virutubisho,’’ amesema Kavishe

Ofisa Kilimo Kituo cha Tari Kihinga, Diana Obadia ametaja panya kuwa miongoni mwa visumbufu vya zao la mchikichi na kuwataka wakulima kutoa taarifa mapema wanapoona dalili za uwepo wa panya shambani.

‘’Mkulima akiona dalili za kuwepo kwa panya shambani kwake anaweza kuzungushia mche wake wavu kwa kuuchimbia sentimita 60 chini ya ardhi,’’ amesema Diana

Timotheo Rusulie, mkulima wa mchikichi Kata ya Kagera Manispaa ya Kigoma Ujiji ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi wa kuongeza tija kwenye kilimo cha zao hilo na uzalishaji wa mafuta ya mawese akisema kimemwezesha kupata miche 230 ya mbegu mpya aina ya Tenera ambayo siyo tu hustawi, bali pia kukomaa kwa haraka na kuzalisha mafuta kwa wingi kulinganisha na mbegu ya zamani.

“Nimeongoa miche ya michikichi ya zamani iliyokuwa inatoa mafuta kidogo na kupanda miche mipya 230; lengo ni kufikia miche 550 itakayoniwezesha kulima hekari 10,’’ amesema Rusulie