Tanzania inaagiza nje tani 360,000 za mafuta ya kula

Muktasari:
Mahitaji ya mafuta nchini ni zaidi ya tani 570,000
Morogoro. Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba amesema Tanzania inaagiza tani 360,000 za mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
Mgumba ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Agosti 25, 2018 wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa zao la michikichi unaofanyika mkoani hapa.
Amesema kilimo cha michikichi kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa miche na mbegu bora.
Amebainisha kuwa mahitaji ya mafuta nchini ni zaidi ya tani 570,000 huku uzalishaji ukikadiriwa kuwa ni tani 210,000.
Amesisitiza kuwa kiwango hicho ni cha mafuta yanayotokana na zao na mchikichi, ufuta, alizeti na mazao mengine.
“Tuna ardhi ya kutosha ya kuzalisha mafuta ndani ya nchi. Kukutana kwetu hapa ni kuleta tija, kuziainisha na kuzipatia ufumbuzi ili kuondokana na changamoto katika uzalishaji,” amesema.
Mkurugenzi wa taasisi ya Trade Mark East Africa (TMEA), John Ulanga amesema wadau katika mkutano huo wanapaswa kupanga mikakati wa namna ya kuleta mapinduzi katika zao la michikichi kwa maelezo kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa katika zao hilo kuna fursa nyingi.
Amesema majadiliano hayo pia yanaweza kuleta tija kwa wananchi kwa kuongeza kipato chao kwa kulima zao hilo.
“Soko la kwanza la mafuta yatokanayo na mchikichi liko ndani ya Tanzania. Ikiwa tutakuza zao hili tutaweza kukuza mazao mengine ya mafuta kutokana na unafuu wa bei utakaokuwepo,” amesema.
“Hata wafanyabiashara ambao wanaagiza mafuta nje ikiwezekana kuzalisha nchini na kuuza kwa bei nafuu nina amini wataanza kununua kwa wingi pamoja na kwamba tunajua kutakuwa na vikwazo lakini hatuna budi kukabiliana navyo.”
Kaimu mtendaji mkuu wa wakala wa mbegu za kilimo (ASA), Dk Sofia Kashenge amesema kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa kazi iliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mkoani Kigoma alipokwenda kuhamasisha kilimo cha michikichi.
Amesema zao la mchikichi katika programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP ll), liliongezewa uzito baada ya kuona matumizi ya mafuta ya mawese nchini na malighafi zinazotokana na zao michikichi kuongezeka kwa kasi.