Tafiti 75 kujadili ustawi, uwezeshaji wa wananchi
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima
Muktasari:
- Mkutano huo umewaleta pamoja watafiti, wasomi, watunga sera na wadau wa maendeleo kutoka nchi 11 kujadili njia bora za kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii zao.
Dar es Salaam. Serikali imesema matokeo ya tafiti mbalimbali zinazowasilishwa katika mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Uwezeshaji wa Watu na Ustawi wa Jamii (ICPEW 2026) yataisaidia Tanzania kuimarisha utekelezaji wa sera, mikakati na sheria zinazolenga maendeleo na ustawi wa wananchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo leo Juni 5, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema mkutano huo umewaleta pamoja watafiti, wasomi, watunga sera na wadau wa maendeleo kutoka nchi 11 kujadili njia bora za kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii zao.
Dk Gwajima amesema tafiti zinazowasilishwa zinagusa maeneo mbalimbali muhimu kama kilimo, afya, uwezeshaji wa kiuchumi, ulinzi wa jamii na namna taasisi za umma na binafsi, zinavyoweza kusaidia kuboresha maisha ya wananchi.
“Mkutano huu unatusaidia kupata ushahidi wa kisayansi unaoweza kutumika katika kuboresha utekelezaji wa sera zetu. Lengo ni kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika maendeleo yao na ustawi wa nchi kwa ujumla,” amesema Dk Gwajima.
Amesema Tanzania imejielekeza katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza uwekezaji kwa watu, maendeleo jumuishi na ustawi wa jamii, hivyo matokeo ya mkutano huo yatakuwa nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), Dk Joyce Nyoni amesema mkutano huo wa kwanza wa kimataifa umewakutanisha washiriki 250 kutoka Tanzania, Uganda, Kenya, Nigeria, Namibia, Lesotho, Zimbabwe, Afrika Kusini, Norway, Austria na Hungary.
“Mkutano huu si tukio la kawaida la kitaaluma. Unawakutanisha watafiti, watendaji na watunga sera ili kujadili changamoto na fursa zinazohusu ustawi wa wananchi katika nyanja mbalimbali,” amesema Dk Nyoni.
Amebainisha kuwa mkutano huo unajadili mada sita kuu ambazo ni jinsia, mamlaka na ushirikishwaji wa kijamii; ulinzi wa watoto, haki za watoto na ustawi wa vijana; afya ya akili na ustawi wa kisaikolojia; mageuzi ya kidijitali, akili bandia na teknolojia kwa maendeleo; maisha na uwezeshaji wa kiuchumi pamoja na ulinzi wa jamii; na utawala bora pamoja na maendeleo ya taasisi.
Kwa mujibu wa Dk Nyoni, zaidi ya tafiti 75 zinawasilishwa katika mkutano huo, zikiwa zimejikita katika kutoa ushahidi wa kisayansi unaoweza kusaidia kuboresha maamuzi ya sera na programu za maendeleo.
Amesema mkutano huo pia umeandaliwa kama mchango wa Chuo cha Ustawi wa Jamii katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga Tanzania yenye uchumi ulioimarika, taasisi imara, wananchi wenye ujuzi na maendeleo jumuishi yasiyomwacha mtu nyuma.
Dk Nyoni amesema miongoni mwa matokeo yanayotarajiwa kutokana na mkutano huo ni kuimarika kwa msingi wa ushahidi unaotumika katika utungaji wa sera na utekelezaji wa programu mbalimbali za maendeleo.
Aidha, amesema machapisho bora yatakayowasilishwa yatafanyiwa mapitio ya kitaalamu na kuchapishwa katika jarida la Chuo cha Ustawi wa Jamii, hatua itakayosaidia kuongeza ushawishi wa tafiti hizo na kutoa nafasi kwa watafiti chipukizi kujitangaza kimataifa.