Tabora waomba mkoa ugawanywe, Rais Samia awajibu

Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na wananchi wa Kigwa, Igalula mkoani Tabora alipokuwa njiani kutoka Kijiji cha Tura Wilaya ya Uyui kwa ajili ya shughuli ya uzinduzi wa barabara ya Nyahua-ChayaLeo Jumanne Mei 17, 2022. Picha na Ikulu
Muktasari:
Rais Samia Suluhu Hassan ameutaka Mkoa wa Tabora kuendelea na mchakato wa kuugawa mkoa huo kwa kukamilisha mambo muhimu yanayotakiwa.
Tabora. Rais Samia Suluhu Hassan ameutaka Mkoa wa Tabora kuendelea na mchakato wa kuugawa mkoa huo kwa kukamilisha mambo muhimu yanayotakiwa.
Hata hivyo amewekwa angalizo kuwa wasitegemee kuwa mkoa utagawanywa sasa hivi kwani bado kuna mambo mengi ya kushughulikiwa ikiwemo kuinua uchumi wa Nchi.
Akizungumza leo Jumanne Mei 17, 2022 wakati wa uzinduzi wa barabara inayounganisha Mkoa wa Tabora na Singida, Rais Samia amesema mchakato uendelee na wakikamilisha vigezo wampeleke.
"Naomba muendelee na mchakato wa kuugawa na mkitimiza vigezo nikute mezani kwangu" amesema
Amesema kwa Sasa hawawezi kuanzisha maeneo mapya ya utawala kwani kazi inayofanywa sasa ni kuinua uchumi ambao ukikua mambo mengi yatafanywa ikiwamo kuanzishwa maeneo mapya ya utawala.
Mkuu huyo wa nchi ambaye yuko katika ziara ya siku tatu mkoa Tabora alikuwa akijibu maombi ya baadhi ya viongozi wa mko huo walioomba mkoa huo ugawanywe kutokana na mkoa huo kuwa mkubwa.
Miongoni mwa viongozi walioomba mkoa huo ugawanywe ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian huku wabunge wa majimbo ya Igalula na Tabora Kaskazini, Venant Daud na Almas Maige wakiomba Wilaya ya Uyui igawanywe na pia kupatikana halmashauri nyingine.
Awali, Dk Batilda alisema mkoa huo una eneo kubwa ambapo hata katika mbio za Mwenge wa Uhuru unakimbizwa kilometa nyingi.
Ameeleza kuwa ukiwa mkoani Tabora, Mwenge wa Uhuru unakimbizwa kilometa nyingi ambazo ni sawa na mikoa mitatu.
Mkoa wa Tabora una ukubwa eneo la kilomita za mraba 75,000 ukiwa unaongoza kwa ukubwa wa eneo nchini kwa sasa.
"Wakati wa mbio za Mwenge tunakimbiza kwa kilomita za mikoa mitatu, tunaomba uangalie namna ya Kufanya" amesema Dk Batilda
Kwa upande wake Mbunge wa Igalula, Venant Protas ambaye aliungwa mkono na Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige wameomba Wilaya ya Uyui na majimbo yake yagawanywe kwa kuwa ni makubwa.