Tabia nchi: Tulipotoka, tulipo na tunakoelekea

Wakazi wa vijiji vya Kisisi, Mafwene na Inyalanyala wakiwa kwenye foleni ya kuchota maji baada ya kuchimba katika Mto Kinyasungwi uliokauka katika Kata ya Godegode mkoani Dodoma. Picha na Habel Chidawali

Muktasari:

Hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980 Wilaya ya Mpwapwa iliongoza kwa utunzaji wa mazingira uliowafanya wananchi wapate maji baridi yaliyotiririka kutoka milima ya Chibodyani, tofauti na ya sasa iliyojaa mawe huku mmomonyoko wa ardhi ukishuhudiwa katika vijiji vingi.

Hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980 Wilaya ya Mpwapwa iliongoza kwa utunzaji wa mazingira uliowafanya wananchi wapate maji baridi yaliyotiririka kutoka milima ya Chibodyani, tofauti na ya sasa iliyojaa mawe huku mmomonyoko wa ardhi ukishuhudiwa katika vijiji vingi.

Kati ya kata 33 zinazounda wilaya hiyo, mazingira ya kata 12 yameharibiwa, hasa Chitemo, Berege, Kingiti, Rudi, Godegode, Mang’aliza, Mazae, Mima, Chunyu, Nghambi, Mpwapwa Mjini na Mlembule.

“Mwaka 1983 usingeweza kutoka kijiji kimoja kwenda kingine, kulikuwa na wanyama wengi, kilimo kilikuwa kinalipa, maji yalikuwapo ya kutosha na hatukuwa na vumbi kama hivi sasa ambapo maisha yamekuwa tabu,” anasema Simoni Ndagwa.

Ndagwa (70) alihamia Kijiji cha Kisisi mwaka 1984 kulikosifika kwa kutoa mazao mengi, maji yakitiririka kutoka milimani.

Sasa hivi anasema hali imekuwa tofauti, kwani upatikanaji wa maji umekuwa wa shida na yanayopatikana ni ya chumvi na hata wakilima hawavuni kama zamani. Mzee huyo anasema misitu imeisha na hawawezi kupata dawa za kienyeji kama awali.

Mkazi wa Kijiji cha Kisisi, Joyce Mogolo anasema baada ya miti yote kufyekwa mateso wanayopata ni kukosekana kwa maji na ardhi kutokuwa na rutuba, hivyo kulima kwa gharama kubwa na kuambulia kidogo.

Mbali ya hayo, Joyce anasema kukosekana kwa misitu kunawafanya washindwe kupata kuni. Shida nyingine anasema ni ukosefu wa maji, kwani wanayafuata umbali mrefu na kuyabeba kwa kuwatumia punda.

“Ili upate maji inabidi uamke saa tisa usiku kwenda mtoni na utarudi saa tano nyumbani ukikuta foleni au saa mbili kama hakuna watu wengi,” anasema Joyce.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisisi, Samweli Chihongwe anasema ukame umesababisha watu wengi wayakimbie makazi yao na kuhamia maeneo mengine.

“Tulikuwa tukipata maji baridi, tena mengi hapo mlimani, hivi sasa maisha ni magumu. Wakati mwingine watu wanashindwa kula kwa kukosa maji. Hivi unawezaje kumudu kununua ndoo moja kwa Sh500 ukiwa na familia?” anahoji Chihongwe.


Mambo yanayosababisha ukame

Mpwapwa ni tone tu katika bahari yanapotajwa maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa na shughuli za binadamu nchini na kote Afrika.

Nchini Angola, Ethiopia, Msumbiji na Somalia vita vilivuruga kilimo na kuwalazimu wakulima kuyatelekeza mashamba ili kuokoa maisha yao.

Uchafuzi wa mazingira na ongezeko la joto duniani pamoja na ongezeko la watu ni mambo mengine yanayoongeza changamoto hiyo. Wastani wa ongezeko la watu Afrika ni asilimia tatu kwa mwaka, mkubwa zaidi duniani. Ili kukidhi mahitaji ya chakula wakulima wanalazimika kulima bila kuyapumzisha mashamba yao.

Misitu inaharibiwa, watu wanaifyeka ili kupata ardhi kwa ajili ya kilimo. Jarida la African Insight linasema miaka 40 iliyopita asilimia 20 ya ardhi ya Ethiopia ilikuwa msitu, lakini hivi sasa ni chini ya asilimia mbili.

Kati ya matatizo yote ya mazingira yanayoitishia dunia, kufyeka misitu ndilo kubwa zaidi, kwani huathiri hali ya hewa na kuchangia mmomonyoko wa udongo na kuenea kwa jangwa.


Misimu saba ya ukame mkubwa

Tanzania imepitia vipindi mbalimbali vya ukame, lakini saba ni vikubwa zaidi kutokana na ukali wake na madhara ambayo Taifa liliingia. Vipindi hivi vilitokea katika miaka tofauti, kabla hata baada ya uhuru. Kwanza ni mwaka 1918, 1927, 1939, 1949 na 1955. Na baada ya uhuru ilikuwa mwaka 1969 na 1972.

Mwaka 1984 hadi 1985 kulikuwa na baa kubwa la njaa, hasa kusini mwa Jangwa la Sahara, hususan nchini Ethiopia ambako takriban watu milioni moja walikufa. Kwa Tanzania ukame huo ulijitokeza, lakini haukuwa na madhara makubwa kama ilivyokuwa katika nchi hiyo na Somalia.


Ukame mbaya katika Afrika

Mwaka 1992, mataifa ya kusini mwa Afrika yalikumbwa na ukame mbaya zaidi katika kumbukumbu zilizopo, kwani mabwawa, visima na baadhi ya mito ya kudumu ilikauka.

Inaelezwa kuwa huenda ndio ukame mbaya zaidi katika karne hii, kwani uliacha misiba mingi.

“Ni mbaya, tena sana kuliko tulivyotazamia. Ilikuwa huwezi kuotesha chochote. Ardhi imekufa,” alisema katika hali ya kutamauka mkulima mmoja wa Zimbabwe aliyenukuliwa na gazeti la The Guardian Weekly la nchini Uingereza.

Kuna mahali wanakijiji wenye njaa nchini Zimbabwe waliripotiwa kula matope au mizizi ya mimea ya mwituni. Mashirika ya misaada yalielemewa na uhitaji uliokuwapo. Kwa mujibu The Guardian Weekly, “kusini mwa Afrika imepoteza kiasi kikubwa cha mazao yake kuliko zilivyopoteza Ethiopia na Sudan katika ukame wa 1985.”

Watu milioni 18 walikaribia kufa njaa nchini Angola, hatari ambayo ndiyo mbaya zaidi iliyopata kutokea katika historia ya nchi hiyo. Inakadiriwa kwamba mifugo milioni moja ilikufa katika mwaka mmoja na karibu asilimia 60 ya mazao yaliharibika nchini humo kutokana na ukame huo.

Hadi Agosti 1992, theluthi mbili ya mazao nchini Zambia yaliharibika, ikalazimu kuingiza tani milioni moja za mahindi kutoka nje kwa karibu watu milioni 1.7 waliokuwa katika hatari ya kufa njaa.

Zimbabwe iliyokuwa ikiitwa bohari la chakula kusini mwa Afrika, ilikuwa na watu milioni nne waliokuwa wakihitaji msaada wa chakula, ambao ni sawa na nusu ya idadi ya watu waliokuwapo kipindi hicho nchinihumo. Katika eneo moja mwalimu wa shule alikaririwa na vyombo vya habari akisema: “Maji ni haba na vyakula ni nadra. Hata jani moja halikubakia ardhini.”

Katika baadhi ya vijiji watu walichuma majani ya miti wakayapika. Serikali ililazimika kupunguza msaada wa chakula kutoka kilo 15 hadi tano kwa kila mtu kwa mwezi. Maji ya Ziwa la Kariba yalipungua kuliko wakati mwingine wowote na matumizi yake yaliwekewa vizuizi huko jijini Bulawayo kuhakikisha hayaishi na yanawanufaisha wengi.

Maelfu ya wanyama katika mbuga za Zimbabwe walikufa. Gazeti moja liliripoti: “Ndege wafu wameanguka kutoka miti iliyonyauka, kobe, nyoka, wanyama-wagugunaji na wadudu wametoweka.”

Msumbiji pia ilikuwa miongoni mwa nchi zilizoathiriwa zaidi na ukame. Ilipata asilimia 80 tu ya chakula chake kwa msaada wa kimataifa. Ilikadiriwa kwamba watu milioni 3.2 walikuwa hatarini kufa njaa. Wananchi wake walikimbia hivyo wakimbizi walimiminika Malawi, Afrika Kusini, Swaziland na Zimbabwe.

Mara nyingi wanaoishi mjini hawajui uzito wa ukame ukilinganisha na walio vijijini. Ofisa aliyehusika na misaada ya chakula Msumbiji alisema “hasara zilizosababishwa na ukame huonekana kama matukio ya mbali kwa watu wengi, hasa wa maeneo ya mjini ambao wamepona katika janga hili la upungufu mkali wa chakula na maji.”

Ingawa mvua zilisaidia kidogo kurudisha uoto wa asili, lakini maeneo mengi ya Msumbiji, Swaziland na Afrika Kusini yalihitaji mvua zaidi, lakini bado matokeo ya ukame huo yaliendelea kudumu kwa miaka mingi iliyofuata hapo baadaye.