Sungusungu waliohukumiwa kwa mauaji walivyoepa kitanzi
Muktasari:
- Ilidaiwa siku ya tukio, Agosti 6, 2017 sungusungu hao wakiwa katika doria yao ya kawaida walimsimamisha David Albert ambaye kesho yake mwili wake ulikutwa katika mashamba ya mpunga.
Arusha. Mahakama ya Rufaa imebatilisha hukumu ya kunyongwa hadi kufa iliyokuwa imetolewa dhidi ya sungusungu watatu baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya mfanyakazi wa Chemi and Cortex Industries Limited, David Albert.
Katika rufaa ya jinai namba 503/2024, Juma Said, Emmanuel John na Aman Saniel wameachiwa huru. Awali, Mei 4, 2023, Mahakama Kuu ilikuwa imewahukumu adhabu ya kifo.
Uamuzi huo umetolewa Machi 2, 2026 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Dk Mary Levira, Gerson Mdemu na Issa Maige, baada ya kubaini kuwa ushahidi wa mashtaka haukuthibitisha hatia bila shaka.
Ilivyokuwa
Upande wa mashtaka ulidai kuwa Agosti 6, 2017 katika eneo la Isamilo, Misungwi, warufani walikuwa kwenye doria kama sungusungu eneo la Bukumbi walipomsimamisha David aliyekuwa akielekea Usagara. Asubuhi iliyofuata, mwili wake ulikutwa kwenye shamba la mpunga.
Shahidi mmoja alidai kuwa aliwaona warufani wakiwa na marehemu chini ya mwanga wa umeme. Polisi waliwakamata na kudai walikiri katika maelezo ya onyo na ziada, wakieleza pia kuwa walimwibia fedha na kugawana Sh1 milioni kila mmoja. Kwa msingi huo, Mahakama Kuu ilihitimisha kuwa walikuwa watu wa mwisho kuonekana na marehemu akiwa hai na ikawahukumu kifo.
Rufaa na uamuzi
Katika rufaa, warufani walipinga kutegemewa kwa ushahidi wa “mtu wa mwisho kuonekana”, wakidai haukuungwa mkono na ushahidi wa kutosha. Pia walipinga uhalali wa maungamo wakieleza yalirekodiwa kinyume cha taratibu na mengine kuwa na dosari za kimaandishi. Walilalamikia pia kutokuitwa kwa mashahidi muhimu.
Jaji Mdemu, akisoma hukumu, alisema kanuni ya “mtu wa mwisho kuonekana” ni ushahidi wa mazingira unaohitaji mlolongo usiovunjika wa matukio. Hata hivyo, Mahakama ilibaini kuwa shahidi aliyedai kuwaona hakutoa maelezo ya kina ya utambuzi, na mashahidi muhimu hawakuitwa, jambo lililoacha shaka.
Mahakama pia iliondoa maelezo ya onyo ya warufani wote watatu baada ya kubaini yalirekodiwa nje ya muda wa kisheria na kuwa na mkanganyiko na dosari ambazo hazikujibiwa ipasavyo na Mahakama Kuu.
Baada ya kuondoa ushahidi wa maungamo na kubaini kuwa kanuni ya “mtu wa mwisho kuonekana” haikuthibitishwa, Mahakama ilihitimisha kuwa hapakuwa na ushahidi mwingine wa kuunga mkono hatia. Hivyo, ikaruhusu rufaa, ikafuta hukumu ya Mahakama Kuu na adhabu ya kifo, na kuamuru warufani waachiwe huru.