Sintofahamu usajili chama kipya cha siasa
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
Muktasari:
- Sintofahamu yaibuka baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwa na kigugumizi katika kujibu madai ya chama tarajiwa cha siasa cha Independent People's Party (IPP), kinachotaka kufuatwa kwa sheria ya vyama vya siasa kipengele 4(a) ambacho wanadai hakijatekelezwa katika maombi yao ya usajili wa muda.
Dar es Salaam. Sintofahamu yaibuka baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwa na kigugumizi katika kujibu madai ya chama tarajiwa cha siasa cha Independent People's Party (IPP), kinachotaka kufuatwa kwa sheria ya vyama vya siasa kipengele 4(a) ambacho wanadai hakijatekelezwa katika maombi yao ya usajili wa muda.
Kwa tafsiri isiyo rasmi, kifungu hicho kinasema: “Mara baada ya kupokea maombi chini ya kanuni ya (3), Msajili atachapisha notisi katika angalau magazeti mawili yanayosambazwa nchi nzima, moja likiwa la Kiswahili na lingine la Kiingereza, kukaribisha pingamizi au jambo lingine lolote linalohusiana na usajili wa chama husika.”
Katika tamko lao ambalo Mwananchi Digital ina nakala yake, IPP inahoji ni kwanini baada ya wao kukamilisha taratibu zote za maombi ya usajili wa muda bado ofisi hiyo yenye jukumu la kusajili na kulea vyama vya siasa nchini haijatimiza takwa hilo la kisheria?
“Kifungu hicho kinaitaka ofisi hiyo kutoa tangazo kupitia magazeti si chini ya mawili yenye usomaji wa nchi nzima na kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza, ikikaribisha pingamizi kutoka kwa mtu yeyote au chama chochote cha siasa kuhusiana na jina, nembo au rangi ya chama kinachotafuta usajili wa muda au jambo lolote maalum linalohusiana na usajili wa chama husika,” inasomeka sehemu ya tamko hilo.
Akizungumza na Mwananchi Digital, mmoja wa wanzilishi wa chama hicho, Andrew Bomani amesema waliwasilisha nyaraka za kuomba usajili tangu Mei 4 mwaka huu lakini ofisi hiyo imekuwa kimya hadi Julai 15,2023 walipopokea barua kutoka ofisi hiyo kuhusiana na nyaraka walizowasilisha japo haionyeshi tarehe ya kupokelewa kwa nyaraka hizo.
“Kwa faida ya Watanzania, tarehe 15 Juni, 2023 tuliyopokea barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusiana na nyaraka zetu. Tuliwasilisha ombi letu tarehe 4 Mei, 2023. Cha ajabu ni kwamba hiyo barua haionyeshi ni lini ofisi hiyo ilipokea ombi la kuisajili IPP. Nini kinafichwa hapa?” amehoji na kuongeza;
“Tumehangaika kwa muda mrefu na kila tulipokuwa tukiwatafuta walikuwa hawapokei simu na tukiwatumia ujumbe walikuwa hawajibu, tumekuwa kwenye wakati mgumu na wasiwasi kuhusiana na mwenendo wa ofisi hiyo ikizingatiwa tangu mwaka 2014 hakuna chama kipya kilichosajiliwa,” alisema.
Hata hivyo Mwananchi Digital, ilimtafuta Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa Sisty Nyahoza ambaye ametajwa na Bomani kwamba aliwaahidi kuwapa mrejesho baada ya wiki moja tangu kuwasilisha nyaraka zao lakini amejibu kwamba “Niko kwenye majukumu ya kazi siwezi kuzungumza labda mtafute Jaji Francis Mutungi atakupa majibu,” amesema Nyahoza.
Baada ya kumtafuta Jaji Mutungi ameliambia Mwananchi Digital kuwa: “Kwa sasa afya yangu haiko sawa niko Hospitali naumwa nikipata nafuu basi nikuwa tayari kujibu madai yao.”
Awali Jaji Mutungi Mei 14 mwaka huu alifanya mahojiano na gazeti la Mwananchi na kudai ofisi yake imepokea maombi ya vyama vipya 18 mbayo yamewasilishwa na wanasiasa mbalimbali nchini wanaohitaji kupata usajili wa muda.
“Tulikuwa na maombi 17, lakini juzi tumepata ombi jingine la chama kimoja, lakini hadi sasa ni vyama sita tu katika maombi hayo ndivyo vimekidhi masharti ya kupata usajili wa muda, sio kila ombi litakidhi,” alisema Jaji Mutungi,
Katika mahojiano hayo Jaji Mutungi alidai baada ya kukidhi sifa kwa baadhi ya vyama hivyo, vitaingizwa katika mpango wa bajeti kwa ajili ya uhakiki wa wanachama.
Hata hivyo, Bomani amesisitiza kwamba kulingana na muda waliowasilisha nyaraka zao wanaona ofisi hiyo inashindwa kusimamia sheria na wanaona hawawezi kuwa na kesho nzuri.
“Barua yao ilichelewa mno kutufikia pamoja na kuikumbusha ofisi hiyo mara kwa mara. Kwenye sheria wanasema haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa.“