Simulizi tukio la mauaji Kigogo Fresh kwa mganga wa jadi

Mwonekano wa nyumba ya mganga wa jadi baada ya kuharibiwa an wananchi wenye hasira.

Muktasari:

  • Kaka wa marehemu aeleza siku za mwisho za ndugu yake aliyekuwa mlinzi kwa mganga wa jadi.

Dar es Salaam. Wakati Mganga wa jadi Tazani Nonyo, akishikiliwa polisi  kwa tuhuma za mauaji ya mlinzi wake Japhari Mwinyimvua (40), kaka wa marehemu ameeleza kilichotokea kabla ya kifo chake.

Mauaji yalitokea Aprili 21, 2024 eneo la Kigogo Fresh, Pugu wilayani Ilala polisi likisema chanzo kinadaiwa kuwa ni baada ya Tazani kumshutumu Mwinyimvua kumwibia mali alizokuwa akilinda.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Muliro akizungumzia tukio hilo  Aprili 22, alisema mbali ya hilo, Richard Nonyo (65), baba mzazi wa Tazani aliuawa kwa kushambuliwa na kundi la wananchi wakimtuhumu mtoto wake kuhusika na kifo cha mlinzi wake.

Kundi hilo la wananchi pia liliharibu mali za Tazani.

Kamanda Muliro alisema mganga huyo ambaye uchunguzi dhidi yake unaendelea, alikamatwa maeneo ya Chanika jana mchana akiwa katika harakati za kukimbia.


Kaka wa marehemu


Akizungumzia tukio lilivyokuwa, Hamza Jaji, ambaye ni kaka wa Mwinyimvua amesema siku chache zilizopita ndugu yake alikuwa na ugomvi na bosi wake akimdai mshahara wake wa miezi miwili.

Amedai bosi huyo pia alikuwa akimtuhumu ndugu yake kuiba mashine ya kuchezea kamari iliyoibwa eneo la biashara ya vinywaji.

Tuhuma hizo anadai zilitokana na bosi huyo kumtuma Mwinyimvua awapeleke wageni anaowatibu kwenye nyumba ya kulala kwa kuwa huwa analaza wagonjwa hapo.

"Marehemu (Mwinyimvua) alipomweleza tukio la kuibwa mashine hakumwelewa, alimwambia yeye ndiye mwenye dhamana ya kulinda mali zake,” amedai.

Hamza amedai bosi huyo alimfungia Mwinyimvua kwenye chumba siku nzima mpaka pale alipopata msaada kutoka kwa askari mmoja wa polisi kutoka kituo cha Chanika.

Hamza amedai siku mbili kabla ya kifo cha Mwinyimvua aliwaambia kapigiwa simu ya kurudi kazini, lakini askari aliyemsaidia alionyesha shaka na kumtaka asiende lakini yeye alienda na kulipokucha kukawa na taarifa kwamba ameuawa.


Ilivyokuwa

Mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo, Mashaka Yasin, amesema saa moja asubuhi akiwa nyumba jirani na kwa Tazani alisikia kina mama wakipiga kelele na kulia wakisema: “Amemuua, amemuua.”

Anasema alisogea eneo hilo na kukuta mwili wa mlinzi huyo ukiwa kwenye kochi na shingoni ikionekana alichinjwa na kitu chenye ncha kali.

Wakati watu wanazidi kuongezeka na kupiga kelele, amesema baba wa Tazani alitoka kuangalia mwili huo na baadaye alisema anaelekea kwa mjumbe kutoa taarifa ya tukio hilo.

"Hata hivyo, wakati baba huyo anarudi alikutana na kundi la watu waliomhoji kila mtu kwa wakati wake na wengine kutaka kumpiga,” amesema.

"Mwisho wa siku waligundua alikuwa amebeba panga ambalo lilianguka katika hali ya kumsongasonga, ndipo walipomshambulia hadi  akapoteza maisha," amesema Yasin.

Viongozi Serikali ya mtaa

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kigogo A, ambako mauaji yalitokea, Edwin Kamugisha, amesema alipata taarifa ya tukio hilo saa tatu asubuhi kupitia mitandao ya kijamii.

Kamugisha amesema alipoenda eneo la tukio alikuta askari polisi wamefika wakiwatuliza wananchi waliokuwa wameghadhibika.

Amedai Tazani hana ushirikiano mzuri na wanajamii wengine lakini akieleza hiyo ni hulka ya mtu.

"Kwenye maisha kila mtu ana namna alivyoamua kuishi, hivyo mwenzetu naye ndiyo maisha alioamua kuishi kwani hata itokee msiba kwa jirani au shughuli za kijamii huwezi kumuona. Ndugu aliyekuwa anajulikana kwake ni baba yake ambaye ndiye alikuwa msimamizi wa biashara zake, ikiwamo duka la vyakula, duka la vinywaji na eneo la kuuza chakula," amesema Kamugisha.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigogo Fresh B, Emmanuel Tarimo amesema katika eneo lake Tazani ana maduka, hivyo wakati uharibifu wa mali unatokea nyumbani kwake Kigogo Fresh A, wananchi wengine walivamia maduka hayo.

Amesema ameshapokea mashauri kadhaa ofisini kwake dhidi ya Tazani kutoka kwa vijana wakimtuhumu kuwadhulumu katika kazi za ujenzi.

Tarimo amesema hivi karibuni alikuwa na shauri kuhusu Tazani la kuwahamisha waliokuwa wapangaji bila kufuata taratibu kwenye fremu za maduka alizonunua.

"Pamoja na yote yaliyotokea, naomba nitoe wito kwa wananchi kunapotokea matukio kama hayo wasipende kuchukua sheria mkononi, badala yake watoe ripoti kwenye vyombo husika likiwemo Jeshi la Polisi,” amesema.

Kauli za majirani

Katika makazi ya Tazani eneo la Kilimani kuna nyumba zaidi ya nne ya mbele ambayo ni eneo la biashara ya kuuza chakula, mwananchi Digital imeshuhudia vioo vya madirisha vikiwa vimevunjwa, baadhi ya mali kama vile runinga, vinywaji na samani za ndani zikidaiwa kuibiwa.

Khalifa Musa, amedai Tazani amekuwa haelewani na vijana anaowapa kazi zikiwamo za ujenzi ikidaiwa huwadhulumu.