Simulizi bibi wa miaka 70 alivyofariki dunia kwa kunyweshwa dawa ya ‘Kamchape’

Mwili wa bibi Busula Magimbi ukiwa kwenye jeneza. Picha na Idd Hassan
Muktasari:
- Mwanamke mwenye miaka (70), Busula Andrew Magimbi Mkazi wa Kijiji cha Kaparamsenga, Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi amefariki dunia baada ya kulazimishwa na mganga maarufu 'Kamchape' anywe dawa ya kienyeji kwa lengo la kuondoa uchawi nyumbani kwake.
Katavi. Mwanamke mwenye miaka (70), Busula Andrew Magimbi Mkazi wa Kijiji cha Kaparamsenga, Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi amefariki dunia baada ya kulazimishwa na mganga maarufu 'Kamchape' anywe dawa ya kienyeji kwa lengo la kuondoa uchawi nyumbani kwake.
Tukio hilo limetokea jana Jumatano saa mbili usiku, ambapo inadaiwa watu watatu walifika nyumbani kwa bibi huyo, wawili wakiwa wanafahamika na mmoja akiwa hajulikani.
Inaelezwa kuwa baada ya kufika walisema wamepata kibali cha kuondoa uchawi ndani ya nyumba ya bibi huyo (marehemu). Hivyo alitakiwa kunywa dawa ili uchawi uliopo uweze kuondoka.
Akizungumza na Mwananchi Digital, mtoto wa marehemu, Emmanuel Kalambwi amesema alipata taarifa saa 12:30 jioni kutoka kwa dada yake kuwa kuna watu wanataka kuondoa uchawi waliodai umeingia ndani mwao kutoka nyumba ya jirani.
“Hivi karibuni kwa jirani yetu kulitokea msiba kutokana na ajali ya moto. Jirani huyo alipata taarifa ya moto unawaka shambani kwake ikabidi atoke nyumbani kwenda kuzima huo moto na alipofika huko ulimzidi uwezo na akafariki kwa kuungua. Sasa baada ya hapo familia pamoja na ndugu huyo wa marehemu wakatafuta mganga ili aje kuangalia kama kifo cha ndugu yao kimetokana na uchawi, au la,” amesimulia.
Amesema kwamba mganga huyo alipofika nyumbani kwa huyo marehemu, akawaambia vitu vilivyosababisha ndugu yao kufariki dunia kwa moto vimekimbilia nyumbani kwao ndipo akawashauri waende kwa jirani kusafisha huo uchawi.
“Sasa ilipofika saa mbili usiku nilikuwa tayari nimerejea nyumbani na chakula cha usiku kilikuwa kimeandaliwa, walikuja watu watatu wakivuta sigara wawili wakiwa ni majira zetu ambao tunawajua wakatueleza lengo lao lakini wakasema mama yetu (enzi za uhai wake) anatakiwa kunywa dawa itakayosaidia kuondoa uchawi,” amesimulia.
Ameongeza kuwa, “Japo nilihoji kama wanakibali cha kufanya lambalamba nyumbani kwetu, wao wakatueleza kuwa wanavibali vyote. Hivyo wakampa mama vikombe viwili vya dawa akanywa lakini baada ya muda kidogo alianza kukohoa na kuishiwa nguvu, nikawauliza mmempa dawa gani, wakanijibu atakuwa sawa ni dawa inafanya kazi basi tukasubiri.”
“Hali ya mama ikazidi kuwa mbaya akaanguka chini na kuanza kutoa povu puani na mdomoni ikabidi wale watu tuwakamate na tukawapeleka Kituo cha Polisi, Karema. Baada hapo tulichukua pikipiki ili kumuwahisha mama hospitali na wakati tunampeleka, aliniambia mwangu nakufa nahisi dawa imeingia hadi kwenye moyo na tulivyofika hospitalini daktari alituambia amefariki dunia,” amesimulia.

Mwili wa bibi Busula Magimbi ukiwa kwenye jeneza. Picha na Idd Hassan
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amefika katika tukio hilo na kukemea watu wanaojishughulisha na vitendo hivyo viovu na ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa tukio hilo.
"Mwaka jana tukio kama hili lilijitokeza Kijiji cha Ikora na Karema watu walipoteza maisha na Serikali ilichukua hatua stahiki kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria na baadhi yao walihukumiwa jela,” amesema.
“Nataka niwaambie watu wa hapa Kaparamsenga tutachunguza kwa kina, tutapita kwenye kila uvungu, kila kona na chochoro zote kuwakamata wote wanaohusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria,” amesisitiza Buswelu.
Mkuu huyo wa wilaya amesema hatakubali wananchi wanapoteza maisha baada ya kufikia umri wa uzee kwa kisingizio cha kudhaniwa ni wachawi.
“Hilo halikubaliki na halivumiliki tutachukua hatua kali na ninachoomba wananchi toeni taarifa za uhalifu ili tushirikiane kudhibiti watu wenye tabia hizi,"amesema Buswelu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kaparamsenga, Paul Mpaga ameeleza kuwa amejitahidi kukemea matukio ya ramli chonganishi katika eneo hilo ambazo zinazosababisha vifo kwa wananchi na kuomba Serikali kuchukua hatua kali kwa wahusika.
Anastasia Nkohozi ambaye ni jirani wa marehemu, amesema tukio hilo limewaumiza kwa kuwa mama huyo enzi za uhai wake walikuwa wakiishi naye vizuri.
“Tunaomba Serikali ichukue hatua za kisheria kudhibiti matukio kama haya maana wananchi tumeanza kuishi kwa wasiwasi,” amesema