Siku za kufukua makaburi Vingunguti zaongezwa, mengine 150 yagundulika

Muktasari:
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeongeza siku tatu kuendelea kuhamisha baadhi ya makaburi ya Vingunguti baada ya kubainika kuwepo kwa mengine 150 kichakani.
Dar es Salaam. Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeongeza siku tatu kuendelea kuhamisha baadhi ya makaburi ya Vingunguti baada ya kubainika kuwepo kwa mengine 150 kichakani.
Shughuli hiyo iliyoanza juzi ilikuwa ifikie tamati leo ambapo makaburi 200 yalipangwa kuhamishwa eneo hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Desemba 29, 2021 Meya wa Jiji hilo, Omar Kumbilamoto amesema hatua hiyo inakuja baada ya kugundulika kuwepo kwa makaburi zaidi yaliyokuwa yamezibwa na kichaka kilichoota eneo la mita kumi kutoka usawa wa mto ambapo shughuli hiyo inapaswa kufanyika.
"Wathamini walipopita hawakuyaona makaburi hayo, hivyo wakati shughuli ya kuyachimbua mengine ikiendelea ndio yakabainika, hivyo tunaenda kutengengeza majeneza mengine 150 kwa ajili ya kuhifadhi mabaki hayo.
"Jambo hili ndilo limetufanya pia tuongeze siku tatu zaidi ili kukamilisha kazi hii," amesema Kumbilamoto.
Kwa upande wake Ofisa Afya wa Jiji hilo, Reginald Mlay amesema shughuli hiyo inaendelea vizuri na kabainisha kuwa idadi ya watu wanaotaka kwenda kuzika kwao imeongezeka kutoka watu watano waliojiandikisha awali na kufika 15 hadi kufika leo.