Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shule mpya Kwa Sadala kuokoa maisha ya wanafunzi, yaleta matumaini

Mwonekano wa Shule ya Msingi Kwa Sadala iliyopo Kata ya Masama Mashariki, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, moja ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika eneo hilo.

Muktasari:

  • Ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Kwa Sadala katika Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, umeondoa hatari ya vifo na ajali za barabarani zilizokuwa zikiwakabili wanafunzi waliolazimika kutembea umbali wa kilomita 12 kwenda shule huku ukiboresha mahudhurio na ufaulu wao darasani

Hai. Wanafunzi wa eneo la Kwa Sadala, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wameondokana na adha ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 12 kufuata elimu, baada ya kujengewa shule mpya iliyopo jirani na makazi yao.

Kukosekana kwa shule hiyo iliyogharimu zaidi ya Sh351.5 milioni, kulikuwa kukihatarisha maisha ya wanafunzi hao wakati wa kuvuka barabara kuu ya Moshi - Arusha kwenda shule ambapo baadhi yao walikabiliwa na ajali za mara kwa mara zilizoua wenzao 10.

Hayo yamebainishwa leo Jumapili Mei 31, 2026 wakati wa ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi aliyetembelea na kukagua shule hiyo iliyopo Kata ya Masama Mashariki, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Emmanuel Ngailo amesema shule hiyo yenye wanafunzi 223, kabla haijajengwa, wanafunzi hao walikuwa wakitumia muda mwingi njiani wakitembea kilomita 12 kufika shuleni kupata masomo.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, akizungumza leo Mei 31, 2026 katika Shule ya Msingi Kwa Sadala, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, akiwa katika ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM, uhai wa chama na miradi ya maendeleo.

Amesema jambo hilo liliathiri mahudhurio yao shuleni, kiwango cha umakini darasani pamoja na maendeleo ya kitaaluma.

“Kabla ya mradi huu, wanafunzi walilazimika kutembea umbali mrefu wa kilomita 12 kwenda na kurudi kilomta 12, lakini kwa sasa watoto wanapata elimu karibu na makazi yao. Mahudhurio yameongezeka na mazingira ya kujifunzia yameimarika kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na hali iliyokuwapo awali,” amesema Ngailo.

Ameongeza kuwa: “Imesaidia kuimarika kwa usalama wa watoto, kuboreka kwa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za elimu karibu na wananchi na kuwawezesha wazazi na walezi kutumia muda mwingi katika shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya familia zao.”

Amesema shule hiyo ilianza kujengwa mwaka 2024 na kukamilika mwaka 2025 kwa gharama ya zaidi ya Sh351.5 milioni, mradi uliohusisha ujenzi wa madarasa saba ya shule ya msingi, madarasa mawili ya elimu ya awali, jengo la utawala pamoja na matundu 19 ya vyoo.

Ngailo amesema wananchi wa eneo hilo, pia, walichangia nguvu kazi yenye thamani ya zaidi ya Sh4.7 milioni kwa kushiriki kuchimba misingi ya baadhi ya majengo, mitaro na mashimo ya majitaka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema shule hiyo imejengwa baada ya jamii kuathirika kwa muda mrefu na kuamua kutoa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa shule ambapo hadi sasa wanafunzi 10 wamepoteza maisha kutokana na ajali.

“Watoto walikuwa wanavuka barabara kutafuta elimu, umbali ulikuwa mkubwa na ajali zilikuwa nyingi ambapo wanafunzi 10 walipoteza maisha kutokana na mazingira hayo. Leo hii watoto wanasoma karibu na makazi yao na hatari hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa,” amesema Babu.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, akizungumza kuhusu ujenzi wa Shule ya Msingi Kwa Sadala leo Mei 31, 2026, wakati wa ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Kihongosi, amesema shule hiyo ni miongoni mwa miradi iliyobadili maisha ya wananchi kwa kuondoa changamoto iliyokuwa ikiwakabili watoto kwa miaka mingi.

“Faida kubwa ya mradi huu siyo majengo pekee. Faida kubwa ni kuokoa maisha ya watoto. Zamani walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda shule na kukabiliwa na hatari mbalimbali njiani ikiwemo ajali lakini sasa elimu imewasogelea,” amesema Kihongosi.

Ameongeza kuwa kuondolewa kwa safari ndefu za kila siku kutasaidia kuongeza muda wa wanafunzi kujifunza, kuboresha mahudhurio na kuongeza ufanisi wao katika masomo.

Kihongosi amewataka wananchi kuhakikisha miundombinu ya shule hiyo inalindwa kwa kuwa ni mali ya umma iliyojengwa kwa gharama kubwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Miundombinu hii lazima ilindwe. Serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya watoto wetu. Ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha shule hii inatunzwa ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu,” amesema.

Amesema ushirikiano ulioonyeshwa na wananchi katika utekelezaji wa mradi huo ni mfano wa namna jamii inaweza kushiriki kuharakisha maendeleo kwa kushirikiana na Serikali.

Mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao, Ramadhan Jamal, ameshukuru Serikali kwa kusikilia kilio chao cha muda mrefu na kuwa kujengwa kwa shule hiyo kutaongeza usalama kwa watoto wao.

“Tunashukuru Serikali kwa ujenzi wa shule hii kwani itasaidia kuongeza usalama wa watoto wetu na kuboresha matokeo yao kwani shule imesogezwa karibu kwa sasa,” amesema.