Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shule 10 za Tanga zaingizwa kwenye mpango maalumu wa kuinua ufaulu

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Centre for Education, Yusuph Ugutu, akitoa mafunzo na mbinu za kujibu mitihani ya taifa kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mikanjuni jijini Tanga. Picha na Mbonea Herman.


Muktasari:

  • Shule kumi za sekondari katika Jiji la Tanga ambazo zimekuwa zikifanya vibaya katika mitihani ya taifa kwa miaka mitatu mfululizo zimeingizwa kwenye mpango maalum unaolenga kuboresha ufaulu kupitia mafunzo kwa wanafunzi, walimu na wadau wa elimu.

Tanga. Shule kumi za sekondari katika Jiji la Tanga ambazo zimekuwa zikifanya vibaya katika mitihani ya taifa kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo zimeingizwa kwenye mpango maalumu unaolenga kuboresha ufaulu na kuondoa changamoto ya matokeo duni ambayo imekuwa ikiathiri wahitimu.

Shule zilizonufaika na mpango huo ni Nguvumali, Mikanjuni, Hoteni, Kihera, Mwapachu, Tongoni, Kirare na Marungu pamoja na shule nyingine mbili za jiji hilo.

Mpango huo umeandaliwa na mradi wa TangaYetu chini ya udhamini wa Botnar Foundation ya Uswisi kwa kushirikiana na taasisi ya Innovex.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Centre for Education, Yusuph Ugutu amesema shule hizo zilichaguliwa baada ya tathmini kubaini kuwa zimekuwa zikifanya vibaya katika mitihani ya taifa kwa miaka mitatu mfululizo.

Ugutu amesema mpango huo unahusisha mafunzo kwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne, yatakayofuatiwa na mafunzo kwa walimu, wakufunzi wa walimu, viongozi wa elimu wa kata pamoja na kamati za wazazi ili kuhakikisha wadau wote wanashiriki katika kuboresha kiwango cha elimu.

"Katika programu hii tutawajumuisha pia maafisa watendaji wa kata ili waweze kutambua changamoto zilizopo katika maeneo yao, hususan tatizo la utoro wa wanafunzi na kushiriki katika kutafuta suluhisho litakalosaidia kufikia malengo ya programu," amesema Ugutu.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mikanjuni, jijini Tanga, wakijiandaa kwa mitihani ya taifa wakati wa utekelezaji wa mpango maalumu wa kuboresha ufaulu katika shule 10 zilizofanya vibaya kwenye mitihani ya kidato cha pili na cha nne kwa miaka mitatu mfululizo. Picha na Mbonea Herman.


Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanahusisha uchambuzi wa muhtasari wa masomo kwa kuainisha mada na malengo mahususi, sambamba na ufafanuzi wa muundo wa mitihani ya kidato cha pili na cha nne kwa kuonesha mada zinazotahiniwa, idadi ya maswali kwa kila mada na uzito wake katika mtihani.

Ugutu amesema hatua hiyo itawasaidia wanafunzi kupanga vizuri maandalizi yao ya mitihani. Pia watafundishwa namna ya kutafsiri misamiati inayotumika katika maswali ya mitihani, kama vile Describe, ili waweze kuelewa kinachotakiwa kabla ya kujibu swali. Aidha, watapatiwa mbinu za kujiandaa kabla ya mtihani, wakati wa mtihani na baada ya kumaliza kufanya mtihani.

Mbali na wanafunzi, walimu pia watanufaika kwa kupata mafunzo kuhusu mbinu za kisasa za ufundishaji zinazozingatia mfumo wa umahiri, utungaji wa maswali yanayokidhi viwango vya sasa vya mitihani pamoja na namna bora ya kufundisha mada mbalimbali kwa lengo la kuongeza ufaulu.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mikanjuni, Kasim Mwagilo, amesema mpango huo utawasaidia wanafunzi kuelewa namna bora ya kujiandaa kwa mitihani ya taifa na kuongeza kujiamini wanapokabiliwa na maswali ya mitihani.

"Tunaamini kupitia mpango huu wanafunzi wetu wataongeza uwezo wa kujibu maswali kwa usahihi, kujiamini zaidi na hatimaye kuboresha matokeo ya shule yetu. Pia, utawapa mwelekeo mzuri wa namna ya kuyatafsiri na kuyajibu maswali ya mitihani," amesema Mwagilo.

Mwanafunzi wa shule hiyo, Radhed Omari, amesema mpango huo umewapa matumaini mapya ya kufanya vizuri katika mitihani yao kutokana na mbinu mpya za kujifunza na kuwajengea walimu uwezo wa kufundisha kwa ufanisi zaidi.

"Tunaamini mpango huu utatusaidia kuongeza ufaulu kwa sababu umetupa mbinu za kujifunza na kujibu maswali ya mitihani, huku walimu wetu wakipata mafunzo yatakayowawezesha kutufundisha kwa ufanisi zaidi," amesema Omari.

Utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuwa chachu ya kuboresha matokeo ya mitihani katika shule husika, huku wadau wa elimu wakiamini kuwa ushirikishwaji wa wanafunzi, walimu, wazazi na viongozi wa elimu utasaidia kuimarisha ubora wa elimu na kuongeza kiwango cha ufaulu katika Jiji la Tanga.