Shahidi adai barua ya msamaha wa wafungwa, haikuwa na saini ya waziri

Aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama (aliyejifunika shuka) akiwa na aliyekuwa ofisa Tehama wa gereza hilo, Sibuti Nyabuya ( mwenye t-shirt nyeupe) pamoja na mfanyabiashara, Joseph Mpangala (mwenye shati la dark blue) wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, baada ya kusomewa hoja za awali katika kesi ya kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa na kujipatia Sh 45 milioni. Picha na Sunday George
Muktasari:
- Hii ni kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga na wenzake wawili wanaodaiwa kughushi barua ya Msamaha wa Rais, akionyesha imetolewa kwa wafungwa watatu raia wa China na kujipatia Sh45 milioni.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wafungwa kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Tanzania, Boid Mwambingu, ameieleza Mahakama namna alivyotumwa kwenda kufanya uchunguzi wa malalamiko ya wafungwa watatu katika Gereza la Ukonga.
Amedai katika uchunguzi huo alibaini barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa hao, aliyoonyeshwa na aliyekuwa Mkuu wa gereza hilo, Josephat Mkama ilikuwa haina saini ya Waziri wa Mambo ya Ndani na kubaini ilikuwa imeghushiwa.
Mwambingu alitumwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) kwa wakati huo ambaye ni Mzee Ramadhan Nyamka kwenda kufuatilia malalamiko yaliyotolewa na wafungwa watatu raia wa China dhidi ya Mkuu wa Gereza la Ukonga, ambapo wafungwa hao walikuwa wanataka kuonana na balozi wa Chini hapa nchini, ili wamueleze malalamiko yao.
Hata hivyo, kwa sasa Mzee Nyamka ni mstaafu wa Jeshi la Magereza.
Shahidi huyo ametoa ushahidi wake leo, Aprili 10, 2025 katika kesi ya kughushi msamaha wa Rais kwa wafungwa inayomkabili aliyekuwa mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama na wenzake wawili.
Mwambingu amedai taratibu za kibali cha msamaha wa wafungwa wanaotumikia kifungo gerezani kinachotolewa na Rais, huwa kinaelekezwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye hukisaini na kisha kukituma kwa Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, ambaye naye hukitawanyisha kwa Wakuu wa Magereza wa mikoa, ambao nao hutawanya katika vituo( gereza) husika kwa ajili ya utekelezaji.
Mkama na wenzake, Sibuti Nyabuya, aliyekuwa ofisa Tehama wa Gereza la Ukonga na mfanyabiashara, Joseph Mpangala, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2024.
Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka manne, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa, kuwasilisha nyaraka ya kughushi na kujipatia Sh45 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Wanadaiwa kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa ajili ya wafungwa watatu raia wa China, Song Lei, Xiu Fu Jie na Haung Quin, waliofungwa katika kesi tofauti kwa makosa ya nyara za Serikali.
Inadaiwa Machi 18, 2016 wafungwa watatu wenye asili ya China waliohukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo katika Gereza la Ukonga.
Wafungwa hao walihukumiwa vifungo tofauti kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kukutwa na nyara za Serikali na wote walikuwa hawajuani.
Hata hivyo, Desemba 21, 2022, Mkama kwa wakati huo alikuwa Mkuu wa Gereza hilo na Nyabuya ambaye alikuwa ofisa Tehama wa gereza hilo kwa kipindi hicho , walitengeneza nyaraka ya kughushi yenye kichwa cha habari ‘'Nyongeza ya Msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru."
Nyaraka hiyo ambayo ni barua ya Desemba 21, 2022, iliyosainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya, kuwa wafungwa hao watatu wameongezwa katika idadi ya wafungwa waliopewa msamaha na Rais.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na Mawakili wawili Waandamizi wa Serikali, Edger Bantulaki na Daisy Makakala, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, shahidi huyo alidai Juni 16, 2023 akiwa ofisini kwake Dodoma, alipigiwa simu na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Mzee Nyamka.
"Aliniambia niende ofisi kwake, nilienda na nilipofika aliniambia kuna wafungwa watatu raia wa China wameleta malalamiko yao, wanataka kuonana na balozi wao aliyepo hapa nchini," alidai Shahidi na kuongeza
"Kamishna Nyamka aliniambia wafungwa hao walimpelekea malalamiko mbalimbali dhidi ya Mkuu wa Gereza la Ukonga kwa wakati huo (Josephat Mkama), yakiwemo ya kuhamishwa gereza, hivyo aliniagiza kwenda kuyafanyia kazi malalamiko hayo, kwa kukutana na wafungwa hao lakini pia kukutana na mkuu huyo wa gereza," alidai Mwambingu.
Alidai kuwa mfungwa Song Lei, alipelekwa Gereza la Isanga, lililopo mkoani Dodoma.
Mfungwa mwenye Fu Jie alipelekwa Gereza la Maweni lililopo mkoani Tanga, wakati mfungwa Haung Quin alibaki Gereza la Ukonga lililopo mkoani Dar es Salaam.
Mwakambingu ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka aliendelea kudai kuwa malalamiko yao ya msingi ya wafungwa hao yalikuwa ni kwamba walipewa msamaha na Rais wa kutoka gerezani, lakini bado walikuwa hawajaachiliwa.
"Hivyo kamishna alinituma kwenda kusikiliza malalamiko hayo na mimi nilienda gereza la Isanga na kuonana na mfungwa Lei raia wa China, ambaye alinieleza kuwa ni kweli anataka kuona na balozi wa China hapa nchini, ili apeleke malalamiko yake kuwa wamepewa msamaha wa Rais wa kutoka gerezani lakini hawajatoka na pia wametoa pesa kwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, lakini mpaka sasa hawajatolewa," amedai Mwambingu ambaye amestaafu kutumia jeshi hilo tangu Juni 12, 2024.
Alidai wafungwa hao baada ya kutoa fedha hizo, ndipo yaliibuka malalamiko hayo kuwa hawajatolewa gerezani wakati wamepata msamaha wa Rais.
Ofisa huyo mstaafu alidai moja ya majukumu yake katika kitengo hicho cha huduma kwa wafungwa ambacho alikihudumu kwa zaidi ya miaka mitatu, ilikuwa ni kuangalia haki za wafungwa magerezani pamoja na haki nyingine ikiwemo ya chakula.
"Nilienda pia Tanga katika Gereza la Maweni na kuonana na mfungwa Jie ambaye naye alinielezea kama alivyoeleza mwenzake na baada ya kutoka Tanga, ilibidi niende Dar es Salaam kwa ajili ya kuonana na mfungwa Quin katika Gereza la Ukonga na kumuhoji mkuu wa gereza hilo pamoja na baadhi ya maofisa wa gerezani hapo," alidai.
Alidai kuwa alipofika kwa Mkama alimueleza kuwa kuna malalamiko ya wafungwa watatu raia wa China ambao walidai kuwa wamesomewa barua ya msamaha wafungwa na Mkuu huyo wa gereza, lakini hawajatolewa.
"Nilimtaka anionyeshe hiyo barua ya msamaha wa wafungwa iliyotolewa na Rais, ambapo Mkama (Mkuu wa gereza la Ukonga) aliniletea faili (jalada) nikaliona," alidai.
Amedai jalada lilikuwa na barua yenye anuani iliyoandikwa Kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza na ilikiwa na kichwa cha habari kilichosomeka kama 'Msamaha wa nyongeza wa wafungwa watatu'
"Nilivyoiona ile barua, niligundua ilikuwa haijafuata taratibu za msamaha kwa wafungwa," alidai.
Alipoulizwa barua za msamaha kwa wafungwa huwa zinakuwa utaratibu gani? Shahidi huyo alijibu kuwa barua za msamaha, Rais ndio anatoa kibali ambacho kinaenda kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchini.
"Baada ya kibali hicho kwenda kwa Waziri atasaini na kisha atakituma kwa Kamishna Jenerali wa Magereza na ataituma kwa wakuu wa magereza wa mikoa husika na wakuu wa magereza wa mikoa nao wataipeleka kwenye vituo husika( gereza husika) kwa ajili ya utekelezaji," alidai
Alipoulizwa kuhusu barua aliyoonyeshwa na Mkuu wa gereza la Ukonga iwapo ilikuwa imekidhi vigezo hivyo, shahidi huyo alijibu kuwa ilikuwa haijakidhi vigezo kwa sababu kibali hicho kilikuwa kimesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, badala ya Waziri wa Mambo ya Ndani.
Shahidi huyo alidai kuwa alipomuuliza Mkama kuhusu usahihi wa barua hiyo, alikaa kimya.
"Pia nilipomuuliza suala la hela aliyopewa na wafungwa ili watoke gerezani, Mkama alinijibu kuwa wafungwa hao wanataka kumuharibia kazi tu," alidai shahidi na kuongeza
"Nilienda pia kuuliza watumishi wenzake wachache akiwemo Sekretari wa Mkuu wa Gereza la Ukonga ambao wote walinieleza kuwa wanafahamu malalamiko ya raia hao wa China yapo," alidai Mwambingu.
Baada ya kuwahoji watu hao alipeleka taarifa kwa Kamishna Jenerali wa Magareza.
"Nilimwambia bosi wangu kuwa nimewahoji wahusika ni kweli malalamiko yapo na yanahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina na wa kisheria," alidai Mwambingu ambaye pia alimtambua mahakamani hapo mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo.
Shahidi huyo alipoulizwa na mawakili kuhusu barua ya msamaha kwa wafungwa aliyopewa na Mkama ambayo ilikuwa kwenye jalada ilikuwa imekuwa na saini ya nani? Alijibu kuwa ilikuwa imesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa wakati huo, aitwaye Kaspar Mmuya.
Pia aliulizwa maswali kadhaa na wakili wa utetezi Nehemia Nkoko, kuhusiana na ushahidi wake, ambapo aliuliza nani aliyekwenda kufungua kesi Polisi?
Shahidi huyo alijibu kuwa ni Kamishna jenerali wa magereza.
Nkoko: Shahidi Kamishna Jenerali wa Magereza alienda kufungua kesi hiyo kituo gani cha Polisi?
Shahidi: Siwezi kujua.
Nkoko: Shahidi utakubaliana na mimi kuwa kwa mujibu wa sheria, wafungwa hawaruhusiwi kuwa na pesa gerezani?
Shahidi: Ni sahihi
Nkoko: Ni sahihi mfungwa yoyote hawezi kuonana na mtu bila ruhusa ya bwana jela?
Shahidi: Ni sahihi
Shahidi huyo baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Mhini aliahirisha kesi hiyo na kupanga siku tatu mfululizo za kuisikiliza kuanzia Mei 13 hadi Mei 15, 2025.