Sh9.3 bilioni kupunguza tatizo la maji maeneo tambarare Rombo

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Momwe, Kata ya Mrao Keryo, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wakiwasikiliza viongozi wao walipokutana kijijini hapo.
Muktasari:
- Serikali imetoa zaidi ya Sh9.3 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji utakaopunguza tatizo la maji katika vijiji 31, vilivyopo maeneo ya ukanda wa tambarare Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.
Rombo. Serikali imetoa zaidi ya Sh9.3 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji utakaopunguza tatizo la maji katika vijiji 31, vilivyopo maeneo ya ukanda wa tambarare Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.
Mradi huo ambao chanzo chake cha maji kinatokana na Ziwa Chala utasaidia kupunguza changamoto ya maji kwa kiasi kikubwa.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo, Aprili mosi, 2025 wananchi wanaoishi maeneo ya tambarare wilayani humo, wamesema changamoto ya maji bado ni tatizo katika maeneo hayo na wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji safi na salama.
Ulirka Tesha, mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Momwe, wilayani humo amesema maeneo ya tambarare ni kama vile yamesahaulika, hivyo akaiomba Serikali iharakishe mradi huo ili waondokane na changamoto hiyo ya maji ambayo imekuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu.
"Wakati mwingine unaacha kufanya shughuli za kiuchumi na kwenda kutafuta maji, sehemu yenyewe unayoenda kuchota maji ni zaidi ya kilomita 10 tunaomba Serikali itusaidie wananchi wa huku tambarare tuweze kupata maji kama watu wengine, tunateseka na shida ya maji," amesema.
Josephat Shao, mmoja wa wananchi wa wilaya hiyo, amesema tatizo la maji katika maeneo ya tambarare haijawahi kupatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu hivyo wamekuwa wakitaabika kwa muda mrefu.
"Ni kama vile tumezoea shida ya maji, wakati mwingine unaacha familia usiku wa manane kwenda kusaka maji, ukiwa na baiskeli huwezi beba zaidi ya ndoo mbili za maji na hata ukifikisha maji nyumbani mnatumia kama vile dhahabu, Serikali itusaidie maana tumeteseka mno," amesema.
Akizungumzia tatizo hilo la maji, Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda amesema tayari Serikali imetoa fedha zaidi ya Sh9.3 bilioni kwa ajili ya mradi wa maji wa Ziwa Chala ambao utapunguza tatizo la maji maeneo ya tambarare.
"Rombo bado hatujamaliza tatizo la maji, mradi wa maji Chala tumeshapata fedha Sh9.3 bilioni na mradi huu utafaidisha wananchi wa vijiji 31 vilivyo upande wa chini (tambarare)," amesema Profesa Mkenda
Amesema kwa sasa kinachosubiriwa ni mkandarasi atakayetekeleza mradi huo apatikane kwa kuwa fedha zipo.
"Fedha tayari zimekuja na tayari mkandarasi anatafutwa na kazi itaanza muda sio mrefu, kikubwa wananchi muendelee kuwa na subira Serikali yenu kupitia Wizara ya Maji ipo kazini kuhakikisha wananchi mnapata maji usiku na mchana," amesema Profesa Mkenda.
Mhandisi wa maji kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Rombo (Rombowsa), Festo Joseph amesema mradi huo wa maji umepangwa kukamilika Julai mwaka huu, ili kupunguza adha ya maji kwa wananchi waishio maeneo ya tambarare.
"Kwa sasa tupo katika mchakato wa manunuzi ya mabomba ili mkandarasi aweze kuanza mradi huu na kazi hii inatakiwa ikamilike kabla ya Julai mwaka huu wa fedha 2024/2025," amesema mhandisi huyo.
Hivyo, akawataka wananchi kuendelea kuwa na subira na kwamba Serikali inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wanapata maji safi na salama.