Serikali yanyoosha mikono, yaondoa kodi ya Sh382 ya gesi kwenye magari

Dodoma. Serikali imekubali mapendekezo ya wabunge ya kuondoa ushuru ya Sh382 kwenye gesi asilia inayotumika katika magari.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Oran Njeza amesema hayo leo Alhamisi Juni 27, 2024 wakati akiwasilisha maoni ya kamati yake kuhusu Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2024.

Tangu kuanza kwa mjadala ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25, wabunge wamekuwa wakilalamikia kuhusiana na kodi hiyo kuwa inarudisha nyuma jitihada za Watanzania kuingia katika matumizi ya gesi asilia ambayo inapatikana nchini.

Amesema kamati hiyo ilikubaliana na mapendekezo ya Serikali ya kuelekeza mapato ya ziada (windfall profit) kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Barabara.

Hata hivyo, Kamati haikukubaliana na uanzishwaji wa ushuru Sh382 kwa kila kilo ya gesi asilia inayotumika kwenye magari.

Amesema kamati imefikia uamuzi huo kwa kuzingatia kuwa sekta ya gesi bado ni changa na inaendelea kukua taratibu na hadi sasa haijaweza kutumika kikamilifu nchini kutokana na gharama za kufunga mfumo wa kutumia gesi pamoja na uhaba wa vituo vya kujazia gesi.

“Hivyo, Kamati iliishauri Serikali kuondoa pendekezo hili na Serikali iliridhia,”amesema.

Awali, wananchi na baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano waliitaka Serikali kuondoa ongezeko la Sh382 kwenye bei ya gesi inayotumika kwenye magari badala yake iongeze vituo vya utoaji wa gesi na kuweka ruzuku kwenye vifaa vya matumizi ya gesi.

Wabunge walitoa maoni hayo wakati wakichangia makadirio ya bajaeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo Serikali iliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha Sh49.35 trilioni.

Ongezeko hilo lilitangazwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/2025, akisema hatua hiyo imefikiwa ili kuleta usawa kwa kuwa magari yanayotumia mafuta tayari yanachangia mapato kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara.

Kutokana na ongezeko kilo moja ya gesi asilia ilitangazwa ingeuzwa Sh1, 932 kutoka Sh1, 550 ya awali.