Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yanunua ambulance 663

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel (wa kwanza kulia) akiwa kwenye makabidhiano ya vifaa tiba wilayani Handeni mkoani Tanga,ambavyo vitatumika kwa ajili ya kuwahudumia watoto watakaozaliwa njiti.Picha na Rajabu Athumani.

Muktasari:

Magari hayo ya wagonjwa yatapelekwa kwenye hospitali zote nchini ili kuweza kusaidia kusafirisha wagonjwa wanaopata rufaa.

Handeni. Wizara ya Afya imesema kutokana na kuonekana uwepo wa uhitaji wa magari ya kubebea wagonjwa katika hospitali nchini, tayari imeshalipia magari 663 ambayo yatapelekwa katika hospitali kwa ajili ya kubebea wagonjwa.

 Hayo yamebainishwa leo Jumapili Septemba 18, 2022 na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel wilayani Handeni mkoani Tanga wakati wa kukabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya Sh130 milioni, vilivyotolewa na kampuni ya Vodacom.

Amesema mpaka sasa Serikali tayari imeshatoa fedha kwa ajili ya kulipia ambulance hizo na lengo ni kuhakikisha changamoto ya kukosekana magari hayo kwenye hospitali inapungua.

Dk Mollel amesema mpango huo utawezesha hospitali zote za wilaya zitakuwa na gari la kubebea wagonjwa, hali ambayo itawawezesha wananchi kuweza kupata huduma hiyo kwenye hospitali zao.

"Wabunge na wenyeviti wa halmashauri wote wanazungumza uhitaji wa ambulance kwenye maeneo yao ila tunapozungumza hii leo, tayari Serikali imeshalipia magari 663 ya wagonjwa ambayo yanakwenda kupelekwa kwenye hospitali mbalimbali za wilaya ili kulabiliana na hali hiyo ", amesema Dk Mollel.

Awali Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano Vodacom, Rosalyn Mworia akikabidhi vifaa tiba hivyo amesema kwa upande wao wanaendelea na kuisaidia Serikali kugawa vifaa tiba, ambapo wamegawa vifaa vya Sh130 milioni katika wilaya ya Handeni na Kilindi.

Amesema wamegawa vifaa vyenye thamani ya Sh76 milioni kwa hospitali ya wilaya Handeni na Sh54 milioni Kilindi kwaajili ya watoto njiti, ambavyo vitawezesha kuwahudumia watoto wanaozaliwa kwenye maeneo hayo.

Mganga mkuu wa halmashauri ya Mji Handeni, Dk Feisal Said amesema vifaa hvyo vitasaidia kuwapunguzia wazazi wanaojifungua watoto njiti safari hasa kuwaepusha na safari za kwenda hospitali za mikoani.

Ameongeza kuwa baadhi ya wazazi ambao wanajifungua watoto njiti hushindwa gharama za usafiri, hivyo uwepo wa vifaa hivyo hawatakuwa tena na gharama za kwenda huko.