Serikali yajitenga mpango wa chakula mashuleni

Muktasari:
- Naibu Katibu Mkuu Tamisemi amesema pamoja na mambo hayo, lakini kazi kubwa ni kuhamasisha wazazi waone umuhimu wa kuchangia chakula mashuleni.
Dodoma. Mambo manne yametajwa kuwa kikwazo katika utekelezaji wa muongozo wa Kitaifa wa utoaji wa chakula na lishe kwa wanafunzi wa elimu msingi, ingawa tayari umeandaliwa mpango wa kumaliza tatizo hilo.
Hata hivyo Serikali imetangaza leo Alhamisi Novemba 16, 2023 kuwa jukumu la kuchangia chakula kwa wanafunzi wa sekondari na msingi ni la wazazi wenyewe.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi anayeshughulikia Miundombinu, Rogatus Mativila wakati akizindua mpango wa Utelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa chakula na lishe kwa wanafunzi wa elimu msingi.
Miongoni mwa maambo yaliyotajwa kama kikwazo ni mwamko mdogo wa wazazi katika uchangia chakula mashuleni, umasikini, uzalishaji mdogo wa chakula katika baadhi ya mikoa na tofauti ya viwango vya kuchangia kati ya shule moja na nyingine.
Uzinduzi huo umefanyika kwa ufadhiri wa Shirika la Umoja wa mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo viongozi wa Wizara ambazo ni mtambuka kwenye masuala ya elimu na lishe.
Mativila amesema kwa sasa wazazi wengi wameelekeza nguvu kwenye kuchangia chakula kwa madarasa ya mitihani pekee huku wakisahau kuwa msingi wa kufika huko wanafunzi ni mandalizi ya kuanzia ngazi ya chini katika kujifunza kwao ambako tafiti zinasema lazima wale chakula mashuleni ili wawe na upeo wa kufikiri vyema.
Amesema ni lazima kwa wazazi kuchangia chakula cha mchana mashuleni na kwamba mpango huo hauwezi kuwaumiza kwani wanachokula shuleni ndicho kiwango walichopaswa kula kama muda huo ungewakuta majumbani.
“Tafiti zinatuambia kuwa, uchangiaji wa chakula mashuleni unafanyika kwa madarasa ya mitihani zaidi, tunasahau kuwa kila mwanafunzi anatakiwa kula chakula anapokuwa shuleni ili ajifunze kama wenzake wengine na kwa kufanya hivyo itatusaidia, hebu tujifunze kwa mikoa ya Njombe, Kilimanjaro na Manyara ambao wao wamefikia asilimia 95 kwenye uchangiaji wa chakula mashuleni,” amesema Mativila.
Naibu huyo ameagiza utekelezaji wa mwongozo aliouzindua kwa niaba ya Waziri wa Tamisemi Mohamed Mchengerwa, ukatasfiriwe na kusomwa na makundi yote kwani utekelezaji wake utakuwa chachu ya kuinua kiwango cha elimu huku Serikali ikiendelea kuongeza nguvu kama ilivyofanya miaka mingine na kwa mwaka huu 2023/24 zilitolewa zaidi Sh145 bilioni kama sehemu ya kuunga mkono juhudi hizo.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Profesa James Mdoe amesema bila chakula shuleni mpango wa maendeleo kwa mwanafunzi utaendelea kuwa kazi ngumu kwenye utekelezaji wake kutokana na tafiti nyingi kubainisha hilo.
Profesa Mdoe amesema mambo yanayotajwa kwa baadhi ya maeneo yanaweza kuwa na ukweli ingawa yote dawa yao ni uamuzi wa wazazi kwani wakisema tutafanya hakuna kitakachoshindikana na kwamba mpango huo utakuwa na matokeo chanya.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sara Gibson amesema ni muhimu kuangalia mpango huo kwa kuwa katika maeneo ambayo yamehamasika matokeo yake yamekuwa ni mazuri hata kwenye viwango vya kitaaluma hivyo wao wanaendelea kuunga mkono mpango huo.
Gibson amesema tangu ulipozinduliwa rasmi mpango huo Julai 2022 na kutarajia kufikia malengo Julai 2027, umekuwa ya udugu na mshikamano na hivyo wangetamani kuona mafanikio makubwa yakipatikana ikiwemo kuwa na mazingira mazuri hata kwenye shule wanazojifunza watu.