Serikali: Waliosababisha maumivu kwa watumishi washughulikiwe
Baadhi ya watumishi wakimsikiliza Profesa Riziki Shemdoe wakati wa kufunga wiki ya utumishi Viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma
Muktasari:
- Profesa Shemdoe amesema wako watumishi ambao wanajifanya kuwa miungu watu na kufanya wengine waendelee kuumizwa na kuumia.
Dodoma. Serikali imemuagiza Katibu Mkuu Utumishi kuwachulia hatua za haraka maofisa utumishi waliosababisha watumishi wengine kutopandishwa vyeo.
Agizo hilo limetolewa leo Jumanne Juni 23, 2026 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Moses Kusiluka wakati akifunga wiki ya utumishi.
Profesa Shemdoe amesema wako watumishi ambao wanajifanya kuwa Miungu watu na kufanya wengine waendelee kuumizwa na kuumia.
"Katibu Mkuu Utumishi, nakuagiza hapa kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, nenda ukawachukulie hatua za haraka waliosabsbisha watu wasipande madaraja kwani wamepeleka maumivu kwa wenzao," amesema Profesa Shemdoe.
Ametolea mfano kuwa aliwahi kupitia maumivu makali akiwa mtumishi ambapo alisahaulika kupandishwa daraja na kusababisha ashindwe kupanda cheo wakati huo hivyo akasema na wengine wavae viatu vya maumivu hayo.
Katika hatua nyingine Waziri amemtaka Katibu wa Wizara ya Utumishi Juma Mkomi kufanya tathmini ya faida ya maonyesho ya wiki ya utumishi kwa kipindi cha miaka mitatu nyuma na waajiri pia watenge fedha kuhakikisha Taasisi zao zinashiriki wakati mwingine.
Waziri Shemdoe amewapongeza Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha ambao kwenye maonyesho hayo wamewakilishwa na watendaji wa Vijiji ambao ndiyo watumishi wa ngazi ya chini.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amemwambia Waziri kuwa, wiki ya utumishi imesaidia kutatua changamoto mbalimbali za wananchi waliotembelea na kupata huduma kwenye mabanda hayo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi Juma Mkomi amesema maonyesho ya mwaka huu yamefana kutokana na idadi ya washiriki na ubunifu waliokwenda nao katika kuwahudumia wananchi.