Safari ya MCL kuelekea mustakabali endelevu wa mazingira

Mkurugenzi wa Kampuni ya MwananchI Communications Ltd, Bakari Machumu (kulia) akizungumza kwenye Kongamano la Mabadiliko ya Tabianchi lililoyofanyika katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam leo. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Jukwaa la Fikra la Mwananchi limejadili mada isemayo: “Safari kuelekea mustakabali wenye urafiki na mazingira,” lengo likiwa ni kuleta suluhu ya pamoja ya changamoto za kimazingira.

Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imeahidi kuendelea kutoa maudhui kwa njia ya dijitali kupunguza athari za uharibifu wa mazingira.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu amesema kampuni imejitathmini na sasa imejikita zaidi katika mitandao ya kijamii ingawa bado inaendelea na uchapishaji wa magazeti.

Machumu amesema haya kwenye Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na MCL linalofanyika leo Juni 14, 2024, Dar es Salaam likijadili mada isemayo: “Safari kuelekea mustakabali wenye urafiki wa mazingira.”

Lengo ni kuunga mkono juhudi za nchi na dunia, hasa kwenye lengo namba 13 la Maendeleo Endelevu (SDGs) la “Hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”

“Tunatumia bidhaa zinazotokana na miti kutengeneza karatasi, tulifikiria ni nini tunafanya kupata malighafi muhimu, tukaamua kuchukua hatua za makusudi kuwa suluhisho. Tukapata miongozo ya kutosha kupitia harakati za maendeleo endelevu zipatazo 17,” amesema Machumu.

Ameongeza kuwa hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan amekuja na kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na MCL ilitafakari jinsi ya kuchangia kampeni hiyo.

“Tukaanzisha Idara ya Mahusiano na Maendeleo Endelevu kuangalia matumizi yetu ya uzalishaji na kuhakikisha tunazingatia mazingira, tukaanza kupunguza vitu vinavyochangia kuchafua mazingira,” amesema Machumu.

Amesema kampuni ina ushirikiano na kampuni ndogo ndogo zinazoleta mabadiliko chanya katika jamii.

Machumu amesema MCL imeahidi kuendelea kutoa maudhui yanayohamasisha uelewa wa mabadiliko ya tabianchi kidijitali.

Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Victor Mushi amesema kampuni ilianza safari ya kuelekea mustakabali wenye urafiki na mazingira kupitia mijadala ya mabadiliko ya tabianchi mwaka jana.

“Ni vizuri kwetu tukazungumzia masuala ya usalama wa chakula na uchumi himilivu kwa kuwezesha Watanzania kupata maudhui kupitia mitandao yetu ya kijamii na magazeti ya Mwananchi na The Citizen.

“Tumeendelea kuzalisha maudhui yenye kuelimisha juu ya mabadiliko ya tabianchi na athari zake. Zaidi tunalenga kuwafikia Watanzania wengi kupitia dijitali, ndio maana tumeweka nguvu kubwa kutoa habari zetu kwa njia hii,” amesema.

 “Nawaahidi wote mliohudhuria mkutano huu mtapata ufikiaji wa maudhui ya mitandao yetu bure kwa muda wa wiki moja. Kwenye tovuti zetu yapo baadhi ya maudhui ambayo ni ya kulipia."

Mushi amesema usomaji wa magazeti mtandaoni unasaidia kupunguza uchafuzi na athari kwa mazingira kwa kuwa magazeti yanazalishwa kutoka kwenye miti.