Saba mbaroni wakiwemo wanaopora kwa pikipiki

Muktasari:
Jeshi la Polisi mkoani Tabora linawashikilia watu saba kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo ya wizi wa kupora kwa kutumia pikipiki nyakati za usiku.
Tabora. Jeshi la Polisi mkoani Tabora linawashikilia watu saba kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo ya wizi wa kupora kwa kutumia pikipiki nyakati za usiku.
Akizungumza leo Ijumaa Julai 21, 2023 na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisa mkoani humo, Richard Abwao amesema kati ya watu hao saba, watatu walikamatwa Julai 19 mwaka huu kwa tuhuma za kupora kwa kutumia pikipiki zilizobandikwa namba bandia ama zisizoonekana kirahisi.
“Katika msako huo tulikamata watuhumiwa watatu waliokuwa wanatumia usafiri huo hasa maeneo ya posta kupora watu simu wakati wa usiku,”amesema
Amesema wengine watatu walikamatwa siku hiyo hiyo Mtaa wa Mapolomoko wakiwa na luninga nne za inch 32, rimoti za luninga na mali zingine ambazo zinadhaniwa kuwa ni za wizi zilizoibiwa eneo la Kariakoo kata ya Kitete Manispaa ya Tabora huku mmoja akishikiliwa kwa madai ya kukutwa na noti bandia 10 za Sh5,000 na tisa za Sh10,000 mtaa wa Msoma mjini Nzega.
Kamanda Abwao amewataka watu walioibiwa mali zao kwenda kituo cha polisi kuangalia pengine wanaweza kuzitambua huku akidai noti bandia zilizokamatwa zimepelekwa tawi la Benki Kuu mkoani Mwanza kwa utambuzi zaidi na kwamba watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.