Ripoti: Tanzania inakopesheka vizuri
Muktasari:
- Fitch Rating imetoa ripoti ikionyesha Tanzania bado ina uwezo wa kukopa zaidi na kulipa madeni hayo.
Dar es Salaam. Wakati kukiwa na hofu juu ya mwenendo wa deni la Serikali, ripoti ya Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na ufanyaji tathmini kwa nchi kujua uwezo wake wa kukopesheka, Fitch Rating, inaeleza Tanzania bado ina uwezo wa kukopa zaidi na kulipa madeni hayo vizuri.
Fitch imetoa ripoti hivi karibuni ikiwa ni miezi mitatu tangu kampuni ya Moody’s Analytics inayofanya kazi kama yao kutoa ripoti iliyoeleza kwa mwenendo wa uchumi iliona Tanzania, inakopesheka na ina uwezo wa kulipa madeni.
Moody’s baada ya kufanya mapitio ilipandisha daraja la uwezo wa kukopesheka Tanzania kutoka B2 ikiwa na mtazamo chanya (Positive Outlook) hadi B1 ikiwa na mtazamo thabiti (Stable Outlook). Daraja hilo ni la juu kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.
Katika tathmini yake, Fitch imeeleza daraja la ukopaji la Tanzania sasa ni B+ ambalo linaashilia uhimilivu mzuri, ikisema hayo ni matokeo ya kuwa na ukuaji mzuri wa pato la Taifa (GDP), kiwango kidogo cha mfumko wa bei na deni la Serikali lililopo katika kiwango cha kati.
Fitch inaamini uchumi wa Tanzania kwa mwaka wa asilimia 5.4 kama ambavyo Serikali inatarajia ukibebwa na ukuaji mzuri wa sekta ya kilimo, madini, utalii, miundombinu na kukamilika kwa miradi mikubwa ya uchukuzi na nishati.
“Tunatarajia uchumi utakua kwa kasi ya asilimia 5.9 katika mwaka unaofuata (2025) kutokana na utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania (EACOP). Na kwa siku zijazo pato linaweza kukua zaidi kama mradi wa gesi asilia ya kimiminika (LNG) utatekeleza,” alieleza ripoti hiyo.
Kadhalika ripoti hiyo ya Fitch inaelezea kuwa na mwenendo mzuri wa akiba ya fedha za kigeni hadi kufikia Dola 5.7 bilioni mwaka 2025 kutokana na sera zilizopo ambazo zinavutia uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji kutoka nje (FDI).
Kuhusu ripoti hiyo, Mhadhiri wa masuala ya fedha wa Chuo Kikuu cha Dar es Saam, Dk Thobias Swai amesema maana ya ripoti hiyo ni kuwa sasa Tanzania ina uwezo wa kukopa zaidi na hayo ni matokeo ya mwenendo mzuri wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya Serikali, kama Reli ya Kisasa (SGR) na Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere na miradi mingineyo.
“Kunapokuwa na utekeleza mzuri wa miradi ya mendeleo, hususan iliyotumia fedha za mikopo, inaongeza imani kuwa hata pesa zikitolewa tena,zitatumika vyema lakini pia kuna imani kuwa miradi hiyo itakuza uchumi na kuongeza kipato, hivyo uwezo wa kulipa madeni zaidi unaongezeka,” amesema Dk Swai.
Amesema kwa kuwa na daraja la juu maana yake sasa Tanzania ikitaka kukopa mkopeshaji anakuwa na imani nayo kwani anakuwa na uhakika kuwa fedha zake zitarejeshwa kwa kuwa zinafanya kazi sahihi na zinachangia ukuaji wa uchumi.
“Kuna nchi nyingi zinazokopo halafu matumizi yanakuwa tofauti, hiyo sifa nzuri kwa wakopeshaji lakini pia wapo wale wanaokopa na kutumia kwa matumizi hayohayo lakini hayana matokeo chanya, nao sio wakopaji wazuri,” amesema.
Aidha kampuni hizo zinatoa tathmini hiyo wakati ambao deni ya Serikali limefikia Sh91.7 trilioni hadi Machi mwaka huu na katika hilo deni la nje ni Sh60.9 trilioni, la ndani likiwa Sh30.7 trilioni.
Akiwasilisha bungeni bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/2025, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema faida za kupandishwa daraja na kampuni hizo za kimataifa ni kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje; na kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Serikali na sekta binafsi katika masoko ya fedha ya kimataifa.
Kuhusu deni la Taifa Dk Nchemba alisema debni hilo ni himilivu na Serikali inaendelea kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha kwamba mikopo inayochukuliwa inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa manufaa ya Taifa.
“Hatua hizi zinaenda sambamba na juhudi zetu za kulipa madeni kwa wakati, hali inayotuweka katika nafasi nzuri ya kifedha na kuendeleza uaminifu wetu kimataifa,” alisema Dk Nchemba.